Home » » MAENDELEO YA TEKNOHAMA KWA SASA IKILINGANISHWA NA HAPO MWANZO.

MAENDELEO YA TEKNOHAMA KWA SASA IKILINGANISHWA NA HAPO MWANZO.

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Tuesday, September 16, 2014 | 7:34 AM


Na Benedict Liwenga, MAELEZO-DSM.

TEHAMA ni moja kati ya Sekta zinazokua kwa kasi hapa nchini na duniani kote na imekuwa ikichangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa na pia imekuwa ikiwezesha sekta nyingine kukua na kuboresha maisha ya wananchi na huduma za jamii kwa ujumla.
 
Kutokana na ukuaji wa Sekta hii, jitihada za makusudi zinahitajika katika kusimamia na kuratibu shughuli za TEHAMA ili nchi iweze kunufaika zaidi kwani mchango wa sekta hiyo unaweza kuwa mkubwa kama TEHAMA na matumizi yake yataratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema zaidi kuliko hali ilivyo sasa.
 
Katika kuhakikisha masuala ya TEHAMA nchini yanaratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema, Serikali iliona ni vema ikaundwa Tume ya TEHAMA (ICT Commission).
 
Tarakilishi “Computer” katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita.
 
Kutokana na kuwepo kwa kifaa hiko dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake.
 
Bila shaka kila mwanadamu katika dunia hii anafahamu ukuaji mkubwa na uwezo wa mawasiliano ambao umeleta mapinduzi makubwa katika ukuaji wa chumi za nchi na mwingiliano wa jamii moja kutoka jamii nyingine.
 
Ni maendeleo haya ya kiteknolojia ambayo yamesababisha utandawazi ambao hakika umeifanya dunia kuonekana kama kijiji kidogo kilicho na jamii nyingi zenye taratibu, maendeleo, mila na desturi na siasa tofauti.
 
Kwa kimombo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inafahamika kama Information Technology au IT kwa kifupi na Kwa Kiswahili teknolojia hiyo inafahamika kama TEKNOHAMA.
 
TEHAMA duniani imeanza kupiga hatua ya kasi sana toka mwishoni mwa Karne ya ishirini na imeleta mabadiliko makubwa katika nyanja za mawasiliano, uchumi, tafiti na ukusanyaji wa takwimu mbalimbali.
 
Pamoja na uwepo wa sheria ya 1974 iliyokuwa ikipinga uagizwaji wa vifaa vya tarakilishi zenyewe na seti za runinga, mfumo wa mabadiliko mbalimbali ndio uliopelekea Tanzania kupiga hatua ya kutosha katika kuboresha mfumo wa habari.
 
Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 inaelekeza kuundwa kwa chombo cha TEHAMA ikiwemo juhudi na programu mbalimbali zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji utaratibu wenye ufanisi.
 
Jitihada za kuanzisha Tume zililenga kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA pamoja na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo maagizo ya Mkutano wa Dunia wa Jamii Habari (World Summit on Information Society).
 
Aidha, jitihada mbalimbali zimefanywa na Serikali katika kuhakikisha Sekta ya TEHAMA inakua nchini na miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uanzishwaji wa vituo vya Mawasiliano vya Jamii (Community Telecentres), ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone-NICTBB), Uanzishwaji wa Wakala wa Serikali wa Mtandao, Uanzishwaji wa Vituo vya Kutunzia kumbukumbu za TEHAMA (Data centres), na Mradi wa Anwani za Makazi na Simbo za Posta.
 
Tume hii inalenga kutambua na kuvutia fursa za uwekezaji katika TEHAMA, kutoa ushauri, kuendeleza rasilimali watu kitaifa kwenye sekta ya TEHAMA, kuendeleza program za kitaifa za TEHAMA na kushiriki katika kuendeleza miundombinu mbalimbali ya TEHAMA yenye sura ya kitaifa kwa kushirikisha wadau wa sekta zote.
 
Kwa sasa, Idara za Serikali, Mashirika, na Asasi za aina zote zimejitahidi kuwa na tovuti zao, ili wananchi wapate habari za vyombo hivyo kupitia mtandao huo wa kompyuta.
 
Serikali imeanzisha uhamasishaji na uendelezaji wa wataalam wa TEHAMA (ICT Professionals) katika taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kujenga rasilimali watu nchini itakayowezesha kutumia fursa na rasilimali za TEHAMA vizuri na kwa manufaa zaidi.
Kwa upande wa Serikali, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine wa TEHAMA imekamilisha Muundo wa Utumishi wa teknohama ambao tunaamini utatoa fursa mahsusi katika kuendeleza watumishi wa fani hiyo ambao ina jukumu kubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu katika zama hizi za TEHAMA.
 
Mafanikio katika jitihada hizo yamekabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutokuwepo kwa chombo mahususi kinachoratibu, kusimamia na kuendeleza TEHAMA nchini.
 
Ni dhahiri kuwa sekta ya Mawasiliano inakuwa kwa kasi kubwa sana duniani kote na hapa nchini kwetu, na hivyo kufanya baadhi ya mambo kuwa na changamoto katika utekelezaji wake hususan kutokuwepo na uratibu wa kitaifa katika miradi na program zenye sura ya kitaifa.
 
Kukosekana kwa mpango wa Kitaifa wa usimamizi wa kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inawasiliana na hatimaye kuepuka upotevu wa rasilimali unaotokana na taasisi mbalimbali kufanya kitu kile kile.
 
Changamoto nyingine ni kutokuwapo na usimamizi, usajili wa kitaifa wa kuendeleza weledi kwa wataalamu wa TEHAMA na kuhakikisha utoshelevu wa rasilimali watu utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya TEHAMA, pia kutokuwepo chombo mahususi chenye majukumu ya kisheria.
 
Tume ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano itasaidia kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kukua kwa sekta ya TEHAMA na kuchochea uzalishaji, ukuaji wa sekta zingine kiuchumi na usambazaji wa huduma za jamii; kuwa na taifa la jamii habari, lenye wataalam wanaotambulika kitaifa na Kimataifa, na wajasiriamali katika Nyanja mbalimbali za TEHAMA kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani; kuwa na uhakika wa usalama katika matumizi ya TEHAMA na kuwepo na mfumo unaoainisha na kuendeleza uwekezaji katika sekta ya TEHAMA kitaifa.
 
Tume hii inatarajia kuondoa changamoto nyingi na kujenga mfumo utakaowezesha uwekezaji wa kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano na TEHAMA yenye sura ya kitaifa; Kuwepo mfumo utakaowezesha wabunifu na wajasiriamali kuendeleza sekta ya TEHAMA; na kuweka utaratibu na miongozo ya namna bora ya kuhifadhi vifaa chakavu vya TEHAMA (e-waste management).
 
“Miongoni mwa mambo muhimu na ya msingi katika kuratibu sekta ya TEHAMA nchini, tume ya TEHAMA inatakiwa ihakikishe inaunda Bodi ya Wataalamu wa TEHAMA ambao watasajiliwa na kufahamika kisheria ili kulinda weledi na maadili ya usambazaji na ubora wa huduma za TEHAMA zinazotolewa kwa jamii”, alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mhe. January Makamba alisema
 
Kwa namna hiyo, tume itakuwa imesaidia kuwa na Taifa Habari lenye wataalam waliounganishwa na chombo kimoja na hivyo basi kuongeza wigo na dhamana ya uwajibikaji kwa huduma zitolewazo kwa jamii.
 
Mhe. Makamba aliongeza kuwa Tume ya Teknnolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na mambo mengine itatakiwa iendelee kuleta  mabadiliko na maboresho katika nyanja ya mawasiliano na habari kwa kuhakikisha inafuta na kuondoa uwepo wa vyuo visivyo na hadhi (feki) vinavyotoa elimu ya sayansi na teknolojia isiyokidhi viwango vinavyotakiwa katika kuboresha sekta ya TEHAMA.
 
Tatizo la kuwepo na uanzishwaji wa vyuo vya masuala ya habari ambavyo kimsingi havina ubora na havifuati Sera ya Habari na Mawasiliano iliyoanzishwa 2003 na hivyo basi kutengeneza wataalamu wasioweza kuendana na kasi ya mabadiliko katika nyanja ya mawasiliano nchini.
 
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilikabidhiwa  dhamana ya kuhakikisha kwamba Teknolojia ya Habari  na Mawasiliano, Sayansi,  Teknolojia na Ubunifu vinachangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi yetu.
 
Pamoja na  jukumu hilo, Wizara hii imepewa dhamana ya kusimamia Taasisi, Mashirika, Tume na  Kampuni ambazo zinachangia juhudi za Wizara katika  kuyafikia malengo na matarajio ya  wananchi. Taasisi hizo ni: Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT); Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST),Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela - Arusha (NM-AIST); Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC); Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Shirika la Posta Tanzania (TPC); Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL); Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo, Serikali imeendelea kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ujenzi ambao ulianza rasmi mwezi Februari 2009. Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa mkongo wa mawasiliano imekamilika na huduma za mawasiliano zimeanza kutolewa. Katika awamu hii, jumla ya kilometa 4,300 za Mkongo katika Mikoa 16 zimejengwa. Mikoa hiyo ni: Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Mara na Kagera.
 
Taarifa zilisema kuwa, kabla ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwepo na kabla ya Mikongo ya Baharini kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, gharama za simu kwa sekunde moja zilikuwa kati ya shilingi 2.50 na shilingi 3.00.  
Aidha, gharama za mtandao wa intaneti zilikuwa shilingi 12,400,000 kwa kiwango cha sita (6) mega bits/sec dedicated internet bandwidth ambapo hivi sasa, gharama ya simu na matumizi ya mtandao zimepungua.
 
Serikali kupitia wizara husika imekamilisha tathmini ya uanzishwaji wa Mtandao wa Elimu na Utafiti (National Education and Research Network-NREN) utakaounganisha vyuo vikuu na vituo vya utafiti 27 katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia Mradi wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia  katika jitihada za Serikali kupeleka huduma za mawasiliano hadi vijijini, Serikali imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).
 
Madhumuni ya Mfuko huu ni kusaidia juhudi za upelekaji mawasiliano ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kupeleka huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini na baadhi ya maeneo ya mjini yasiyokuwa na mvuto kibiashara.
 
Hadi sasa Mfuko umeainisha vijiji 239 katika mikoa 17 ambayo ni Dodoma, Arusha, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Singida, Tabora, Rukwa, Shinyanga, Kagera, Mara, Manyara na Kigoma (Kiambatisho Na.10). Aidha, vijiji 139 vimechaguliwa kwa ajili ya mradi wa majaribio (pilot project). Uhakiki wa maeneo mengine unaendelea.
 
Mabadiliko na maboresho katika teknologia ya habari na mawasiliano Tanzania yametokana juhudi madhubuti zilizofanywa na serikali sambamba na hitaji na malengo ya millenium na Dira yake ni  kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania katika nyanja mbali mbali yanafikiwa ifikapo 2025.
-MWISHO-
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA