Home » » HOTUBA YA UFUNGUZI WA KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA KULINDA TEMBO TAREHE 04.10.2013 IRINGA

HOTUBA YA UFUNGUZI WA KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA KULINDA TEMBO TAREHE 04.10.2013 IRINGA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Friday, October 4, 2013 | 5:41 AMNdugu zangu,
Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa kutupatia neema ya kuiona siku hii ambayo tunafanya matembezi ya kulinda tembo, ikiwa ni jitihada zinazofanywa na watu mbalimbali ambao wanajitolea ulimwenguni kuhakikisha kuwa kila kiumbe kinapata haki yake ya kuishi.

Pili, nachukua nafasi hii kuwashukuru waandaji wa matembezi haya ya kuzuzia ujangili dhidi ya tembo dunia nzima ambayo leo hii wanafanya matembezi yao hapa Iringa ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya tembo ambayo karibu miji 40 duniani yanafanya tukio kama hili.

Nikiwa kama mdau katika suala zima la vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori hasa kwa tembo hapa nchini, ninafarijika kuona juhudi na nia ya dhati ya watu mbalimbali duniani ambao wanasikitishwa lakini pia wanaumizwa na ukatili unaofanywa na watu wachache kwa maslahi  yao binafsi huku wakiteketeza na kuweka rehani baadhi ya viumbe hai hasa tembo.
Leo hii , si ajabu kusoma magazeti ama kupata habari kupitia vyanzo mbalimbali vikitoa taarifa juu ya ukatili wa tembo unaofanywa na mtandao hatari wa majangili nchini . 

Tumesema sana, tumepiga kelele sana na hata tumekuwa mstari wa mbele wa kuzungumzia juu ya ukatili huu wa tembo lakini vyombo vya dola pamoja na Serikali vimekua vikirushiana mpira hali inayofanya suala hili la ujangili wa pembe za ndovu kuonekana kama jambo la kawaida kwa wananchi.

Ndugu zangu, ni jambo la kusikitisha pia kuona kuwa Tanzania sasa ipo katika ramani ya dunia kutokana na matukio ya ujangili dhidi ya tembo ambapo takwimu mbalimbali kati ya mwaka 2009-2011 zinaonesha kuwa katika zaidi ya kila kilo 800 za pembe za ndovu zilizokamatwa, asilimia 37 ni Tanzania. Hii ni kengele ya hatari.

Watanzania wenzangu, ni masikitiko makubwa kuona kuwa mkutano mkuu wa wanachama wa Mkataba wa Biashara wa Viumbe walio hatarini (The Convention on Trade in Endangered Species - CITES) uliofanyika Bangkok, mwaka huu Tanzania na Kenya zilitajwa kati ya nchi nane duniani, ambazo zinaongoza kwa biashara haramu ya wanyamapori na hivyo mkutano ule ulipendekeza kuwa nchi hizi lazima ziwekewe vikwazo vya biashara

Leo hii katika nchi tunayojivunia kuwa kisiwa cha amani, tunajenga kizazi kisichokuwa na woga wa kutunza na kuzilinda rasilimali zake hasa wanyamapori waliopo hatarini kutoweka, huku wajanja wachache wakilindwa kwa maslahi yao binafsi. 

Hali ya ujangili nchini imefika pabaya na ina kiasharia kibaya kwa miaka michache ijayo. 

Takwimu zinaonedha kuwa mwaka 2010, jumla ya tembo 10000 waliuliwa Tanzania, ikiwa ni sawa na wastani wa tembo 27 kwa siku. Mwaka 2012 pekee, tembo takribani 23000 wameuliwa kwa mwaka ambayo ni sawa na tembo 63 wa siku. 

Hii ni sawa na ongezeko la 57% kwa kipindi cha miaka 2. kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na tembo kati ya 150,000 na 170,000.  Kutokana na takwimu hizi , ikiwa Tembo 63 wanauliwa kwa siku, hivyo basi, kwa kipindi cha miaka 7 ijayo  Tembo hawa watakuwa wameuawa wote.

Wakati dunia nzima ikiwa imeamka na kuanza vita thabiti dhidi ya ukatili huu kwa tembo, Tanzania pamoja na nafasi tuliyonayo ,  Serikali imeshindwa kujibu masuala ya msingi ikiwemo kutoa kigugumizi ilicho nacho katika kutaja hadharani kama ilivyoahidi mtandao wa majangili na wafanyabiashara haramu wa pembe za ndovu.

Kwa kifupi, ujangili dhidi ya tembo si tu kuwa unaliletea hasara kubwa taifa kwa kuwa unatishia uhai wa sekta ya utalii inayoingiza Serikali mabilioni ya fedha lakini pia inahatarisha uwepo wa tembo katika taifa letu ambalo linasifika duniani kwa kuwa na vivutio vya asili vyenye kila aina ya wanyama ikiwemo Tembo ambao sasa wapo katika hatari ya kutoweka.

Napenda kutoa rai kwa kupitia hadhara hii kumshinikiza Raisi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa dhamana aliyopewa kwa kupitia katiba, aweze kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola na kuwatendea ipasavyo watuhumiwa wote wa ujangili hasa wa tembo.

 Natoa shinikizo hili kwa kuwa mara kadhaa, mawaziri wenye dhamana wameendelea kukiri kuwa wanawafahamu majangili mpaka sehemu wanazokaa lakini imeendelea kuwapa muda. Swali la kuuliza, je tunasubiri tembo watoweke ndio tuanze kumtafuta mbaya/mchawi wetu? Ama ndo msemo wa waswahili kuwa 'La kuvunda halina ubani?'.

Moja kati ya maazimio ambayo leo hii ningependa kuashirikisha ni pamoja na kumtaka Raisi kuwachukulia hatua maafisa na watendaji wote wa Serikali na vyombo vya usalama ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishukiwa na kushutumiwa kwa ushiriki wao hasa katika kulinda ama kusaidia mtandao wa ujangili nchini.

Watanzania wenzangu, Raisi hana budi kulichukulia jambo hili la ujangili wa tembo kwa uzito mkubwa na kulipa nafasi katika moja ya mambo ya msingi ambayo kama Taifa lazima tuyazungumze bila kificho wala kulinda maslahi ya watu wachache  tena kwa uwazi na ukweli kwa kushirikiana na umma wa watanzania.

Mapambano dhidi ya ujangili na ukatili wa tembo lazima yafanywe kwa dhamira ya dhati na si kwa nia ya kuwapumbaza wananchi huku watu waliopo katika mtandao wa ujangili wakilindwa na kujinufaisha kwa maslahi yao binafsi. 

Na mpaka sasa ni dhahiri kuwa ukimya wa Serikali na kigugumizi chake cha kuwachukulia hatua watuhumiwa kunatokana na ubinafsi, uozo na kutojali maslahi ya taifa kwa ujumla.

Napenda kuwahakikishia waandaji kuwa , nitaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali hizi muhimu na urithi huu mkubwa wa taifa letu kwa moyo wangu, nafsi yangu,nguvu zangu na akili zangu kwa kushirikiana na watanzania wote kwa ujumla bila kujali tofauti za kiitikadi na misimamo.

Ningependa kuongea mengi, ila kwa leo napenda kumalizia kwa kuwakumbusha wananchi pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda haki za wanyamapori hasa tembo hata pale tunapoona kuwa Serikali inafanya jitihada hafifu katika mambo ya msingi.

Nachukua nafasi hii tena kuwapongeza waandaji kwa kuandaa matembezi haya ambayo yanalenga kulinda tembo na  kuhakikisha pia kuwa Tanzania tunakua mabalozi wazuri wa vita dhidi ya ukatili wa tembo.

Mwisho, napenda kuwatakia maadhimisho mema ya siku ya Tembo ya kimataifa kwa kuwaambia kuwa 'Pamoja Twaweza'.
Wenu,

...................................
Mch.Peter Simon Msigwa(MB)
Iringa Mjini,
Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA