Home » » MAREKANI,UJERUMANI ZATAKA MURSI AACHILIWE

MAREKANI,UJERUMANI ZATAKA MURSI AACHILIWE

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Sunday, July 14, 2013 | 9:42 AM

Kundi la Udugu wa Kiislamu limeitisha maandamano makubwa ya umma nchini Misri siku ya Jumatatu huku Marekani ikiungana na Ujerumani kutaka kuachiliwa huru kwa rais aliyepinduliwa na jeshi, Mohamed Mursi.
Wito wa Udugu wa Kiislamu umetolewa masaa kadhaa baada ya maelfu ya wafuasi wa Mursi kuingia mitaani kwenye maandamano ya amani ya kudai kuachiliwa kwa kiongozi wao mjini Cairo.
"Jumatatu ijayo, Mungu akipenda, umma mkubwa utakusanyika kwenye viwanja vyote vya Misri dhidi ya mapinduzi haya ya kijeshi. Misri huamua kupitia kura na maandamano maandamano ya amani. Hakuna yeyote, kundi lolote au taasisi ya kijeshi itakayolazimisha maamuzi yake kwa watu wa Misri," amesema Essam El-Erian wa chama cha Uhuru na Haki, ambacho ni tawi la kisiasa la Udugu wa Kiislamu.
Kundi la Udugu wa Kiislamu limekataa aina yoyote ya mazungumzo ya kisiasa tangu wakati huo, likishikilia kwamba ni lazima Mursi arejeshwe madarakani.
Marekani, Ujerumani zataka Mursi aachiliwe
Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013. Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013.
Siku ya Ijumaa, Marekani ilitoa wito kwa jeshi la Misri kumuachia Rais Mohamed Mursi, ikisema inaungana na Ujerumani ambayo ilitangulia kutoa wito kama huo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Jen Psaki, alisema nchi yake inakubaliana na Ujerumani katika hilo na kwamba ilitoa ombi hilo hadharani. Licha ya serikali ya mpito kusema kwamba Mursi yuko salama, lakini hajaonekana hadharani tangu alipopinduliwa na jeshi tarehe 3 Julai.
Psaki alisema Marekani inataka kuondolewa kwa usiri juu ya taarifa za wapi alipo Mursi, ambapo Ujerumani ilipendekeza kwamba taasisi inayoaminika, kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu, ipewe fursa ya kumuona na kumuhudumia Mursi.
Maandamano yapamba moto
Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013. Maandamano ya kumuunga mkono Mohamed Mursi mjini Cairo siku ya tarehe 12 Julai 2013.
Maandamano tafauti ya kumuunga mkono na kumpinga Mursi yalifanyika mjini Cairo siku ya Ijumaa (tarehe 12 Julai), kwa njia ya amani licha ya hofu za awali kwamba yangelikumbwa na machafuko.
Magharibi ilipoingia, maelfu ya wafuasi wa Mursi kwenye mitaa kadhaa ya Cairo waliswali na kukata swaumu zao, ikiwa ni Ijumaa ya kwanza tangu kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo katika uwanja maarufu wa Tahriri na nje ya kasri ya rais ya Ittihadiyya, mamia ya waandamanaji wanaompinga Mursi walifutari pamoja.
Wafuasi wa Mursi wamekuwa wakiandamana pia nje ya msikiti wa Rabaa al-Adawiya katika mji wa Nasr, ambako wakiwa wamebeba Qur'an na bendera za Misri, wanasikikana wakipiga mayowe ya kuyalaani mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia.
"Tutaendelea kupambana," kiongozi wa ngazi za juu wa Udugu wa Kiislamu, Safwat Hegazi aliuambia umma siku ya Ijumaa. "Tutakaa hapa kwa mwezi mmoja au miwili, au hata mwaka mmoja au miwli. Hatutaondoka hadi rais wetu, Mohamed Mursi, arudi."
Hayo yanatokea katika wakati ambapo waziri mkuu wa serikali ya mpito, Hazem el-Beblawi, anatarajiwa kuliapisha baraza jipya la mawaziri wiki ijayo.
Baraza hilo lina jukumu la kuutekeleza mpango wa jeshi kuelekea utawala wa kiraia, baada ya jeshi kumpindua rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia hapo tarehe 3 Julai.
SC.DW
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA