Home » » MWONGOZO KUHUSU MUUNDO, UTARATIBU WA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA (MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA) NA UENDESHAJI WAKE

MWONGOZO KUHUSU MUUNDO, UTARATIBU WA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA (MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA) NA UENDESHAJI WAKE

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Tuesday, February 26, 2013 | 11:26 PMJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MWONGOZO KUHUSU MUUNDO, UTARATIBU
WA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA (MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA) NA UENDESHAJI WAKE

 1.0. UTANGULIZI
Kwa mujibu wa Kifungu cha 18 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Tume inawajibu wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Muundo wa Mabaraza ya Katiba unapaswa kuzingatia mgawanyiko wa kijiografia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabaraza ya Katiba yatawashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii kwa lengo la kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba. Aidha, kifungu cha 17 (8) kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utatumika kila upande wa Muungano.
Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba. Kwa mujibu wa Kifungu kidogo cha (6), Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
Kwa Msingi huo, Tume imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili yafuatayo:-
1.1      Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa).

1.2      Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu).
Mwongozo huu unaainisha Muundo, Utaratibu wa kuwapata Wajumbe na Utaratibu wa Uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yatakayoendeshwa na kusimamiwa na Tume.
 2.0. MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA
Kwa kuzingatia mgawanyiko wa kijiografia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yataundwa kwenye kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika ngazi ya Halmashauri za Jiji, Manispaa, Mji, Wilaya na Mabaraza ya Miji.
Kwa upande wa Tanzania Bara, Katika Mikoa yote ngazi ya kupata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) itakuwa ni Ngazi ya Kata. Wajumbe watapigiwa kura za kupendekezwa kwenye ngazi za Kijiji/Mitaa na kuchaguliwa kwenye ngazi ya Kata.
Kwa upande wa Zanzibar, Katika Mikoa yote ngazi ya kupata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) itakuwa ni Shehia. Wajumbe watapigiwa kura kwenye ngazi za Shehia.
Muundo na utaratibu huu umezingatia changamoto mbalimbali zikiwemo; ukubwa wa Mabaraza ya Katiba, utaratibu wa kuwapata wajumbe, ufanisi katika uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba, gharama ya kufanikisha shughuli ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, na tofauti ya Mfumo wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar.
Kutokana na changamoto hizo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya haufanani kwa pande zote za Muungano.
 3.0. WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

3.1        Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba.
Mabaraza ya Katiba katika ngazi ya Halmashauri za Jiji, Manispaa, Mji, Wilaya na Mabaraza ya Miji yataundwa na Wajumbe wafuatao:-

3.1.1.    Kwa Tanzania Bara.
3.1.1.1      Wajumbe wanne kutoka kila Kata watachaguliwa kwautaratibu utakaofafanuliwa na Mwongozo huu.
3.1.1.2      Wajumbe wanane kutoka kila Kata kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

3.1.2.    Kwa Zanzibar.
3.1.2.1.    Wajumbe watatu kutoka kila Shehia watachaguliwa kwa utaratibu utakaofafanuliwa na Mwongozo huu.

3.1.3.    Kwa pande zote za Muungano.

3.1.3.1.    Madiwani wa kuchaguliwa kwenye Kata / Wadi.

3.1.3.2.    Madiwani wa Viti Maalum.

3.1.3.3.    Madiwani wa kuteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa pande zote za Muungano [Madiwani waliopo kazini kwa sasa].
3.2        Ngazi ya Msingi ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba

3.2.1.    Kwa upande wa Tanzania Bara
Kwa Mikoa yote ya Tanzania Bara, ngazi ya msingi ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba itakuwa Kata.

3.2.2.    Kwa upande wa Zanzibar
Kwa Mikoa yote ya Zanzibar, ngazi ya msingi ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba itakuwa Shehia.

3.3        Idadi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Idadi ya Wajumbe itakuwa kama ifuatavyo:-

3.3.1.  Kwa Tanzania Bara, idadi ya Mabaraza ya Katiba yatakayoendeshwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni 163 ambapo kila Mamlaka moja ya Serikali za Mitaa ngazi ya Wilaya itakuwa na Baraza moja la Katiba ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kila Halmashauri itakuwa na Mabaraza mawili ya Katiba. Hivyo, jumla ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa itakuwa 163 (zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 160).

3.3.2.    Katika Mikoa 24 ya Tanzania Bara, kila kata itawakilishwa na Wajumbe wanne (4) ambao wataungana na Madiwani wa Kata na Viti Maalum. Idadi ya Kata ni 3,339 ukiondoa kata 90 za Mkoa wa Dar es Salaam, zinabaki kata 3,249 [utaratibu wa kuwapata wajumbe kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni tofauti na Mikoa mingine ya Tanzania Bara na umefafanuliwa katika aya ya 3.3.3]. Hivyo, Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutoka kwenye Kata zote isipokuwa kata 90 za Mkoa wa Dar es Salaam, watakuwa 12,996 na idadi ya Madiwani wote ni 4,453.

3.3.3.  Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wenye Kata 90 utawakilishwa na Wajumbe wanane (8) kutoka kila Kata. Kwa hiyo, idadi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutoka Mkoa Dar es Salaam Watakuwa 720 watakaoungana na Wajumbe wengine kama ilivyofafanuliwa kwenye aya ya 3.3.2.

Jumla ya Wajumbe wote wa Mabaraza ya Katiba kwa Tanzania Bara watakuwa 18,169 kwa mchanganuo ufuatao:-

3.3.3.1.  Idadi ya Wajumbe 4 kutoka kila Kata                                12,996

3.3.3.2.  Idadi ya Wajumbe 8 kutoka Kata za Mkoa wa
                               Dar es salaam                                                                        720

3.3.3.3.  Idadi ya Madiwani wote ni:                                                  4,453
18,169
  JUMLA:                         


3.3.4.  Kwa upande wa Zanzibar, idadi ya Mabaraza ya Katiba yatakayoendeshwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni 13 ambapo kila Mamlaka moja ya Serikali za Mitaa itakuwa na Baraza moja la Katiba (zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 13).

3.3.5.  Katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 13 za Zanzibar, kila Shehia itawakilishwa na Wajumbe watatu (3) ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Viti Maalum, na Wakuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Idadi ya Shehia ni 335. Hivyo, Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutoka kwenye Shehia zote watakuwa 1,005 na idadi ya Madiwani wote ni 193.

Jumla ya Wajumbe wote wa Mabaraza ya Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198 kwa mchanganuo ufuatao:-

3.3.5.1.Idadi ya Wajumbe kutoka kila Shehia:                               1,005
                                               
3.3.5.2.Idadi ya Madiwani Wote ni:                                                     193
1,198
            JUMLA                

Mchanganuo wa idadi ya Wajumbe kwa kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kama ilivyo  kwenye Jedwali “1” kwa upande wa Tanzania Bara na Jedwali “2” kwa Zanzibar.


 4.0. SIFA ZA WATAKAOCHAGULIWA KUWA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA.

Wajumbe wanne kutoka kila Kata kwa Tanzania Bara na wanane kutoka kila Kata katika Mkoa wa Dar es Salaam na Wajumbe watatu kutoka kila Shehia kwa Zanzibar wanapaswa kuwa na sifa zifuatazo kwa pamoja:-

4.1        Awe ni Raia wa Tanzania.
4.2      Awe na umri wa miaka 18 au zaidi.
4.3      Awe na uwezo wa kusoma na kuandika.
4.4      Awe ni mkazi wa kudumu wa Kijiji/ Mtaa / Shehia husika.
4.5      Awe ni Mtu mwenye hekima, busara na uadilifu.
4.6      Awe ni Mtu mwenye uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.

 5.0. MAMBO YA KUZINGATIWA
Licha ya sifa zilizotajwa katika aya ya 4.0., utaratibu wa kuwapata Wajumbe kwa Tanzania Bara na Zanzibar uzingatie mambo yafuatayo:-
5.1        Uwakilishi wa watu wazima.
5.2        Uwakilishi wa wanawake.
5.3        Uwakilishi wa vijana, yaani kati ya miaka 18 hadi 35.
5.4        Jiografia ya Kata/ Wadi / Kijiji / Mtaa / Shehia husika.

 6.0. UTARATIBU WA KUWAPATA WAJUMBE KWENYE MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA NGAZI YA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

6.1        Kwa upande wa Tanzania Bara utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-

Kwa Mikoa yote isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam.

6.1.1.  Kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, kila Mwananchi wa Kijiji / Mtaa husika anayependa kuwa Mjumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa atawasilisha jina lake kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa. Uwasilishaji huo uambatane na taarifa zifuatazo:-
6.1.1.1.    Majina kamili ya mwombaji.
6.1.1.2.    Jinsi yake.
6.1.1.3.    Umri wake.
6.1.1.4.    Elimu yake.
6.1.1.5.    Kazi yake.
6.1.1.6.    Sehemu anayoishi katika Kijiji / Mtaa husika.

6.1.2.  Wakati wa uwasilishaji wa jina, kila mwananchi anayependa kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya, atawasilisha nakala mbili za barua kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa. Nakala moja ibaki kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa; na nakala ya pili iwekwe Mhuri na saini ya Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa. Nakala hiyo abaki nayo mwanachi husika kwa uthibitisho kuwa barua yake ilipokelewa.

6.1.3.  Orodha ya majina ya Wananchi wote wanaotaka kuwa Wajumbe yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi / matangazo ya kila Ofisi za Kijiji / Mtaa siku saba (7) kabla ya Mkutano ili wananchi wapate fursa ya kuyapitia na kujiridhisha kama walioomba wana sifa zilizoanishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0.
6.1.4.  Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa ataitisha Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa ambao utakuwa na agenda moja tu ya kuwapendekeza kwa kuwapigia kura watu wanne ambao majina yao yatawasilishwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata. Mkutano huu utaendeshwa na Mwenyekiti wa Kijiji / Mtaa, ambapo Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa atakuwa Katibu wa Mkutano huo na ndiye atakayewasilisha majina ya wananchi wote walioomba kuingia kwenye Baraza la Katiba la Wilaya.

6.1.5.  Kwa kuzingatia Sifa zilizoainishwa katika aya za 4.0. na 5.0,  Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa utayapigia kura ya siri majina ya wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

6.1.6.  Utaratibu wa kupiga kura za kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa kuwachagua Wananchi wanne wanaopendekezwa kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya utakuwa kama ifuatavyo:-

6.1.6.1.    Kwanza, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu mzima mmoja [anaweza kuwa mwanamke au mwanamme].
6.1.6.2.    Pili, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya kumchagua Mwanamke mmoja.
6.1.6.3.    Tatu, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya kumchagua Kijana mmoja [anaweza kuwa Mwanamme au Mwanamke].
6.1.6.4.    Nne, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu mwingine yeyote kutoka miongoni mwa Wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Baraza la katiba la wilaya.

6.1.7.  Orodha ya majina ya wananchi wanne waliopigiwa kura nyingi za kupendekezwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi/ matangazo ya kila Ofisi ya Serikali ya Kijiji / Mtaa.

6.1.8.  Majina ya watu wanne yatakayokuwa yamepata kura nyingi kuliko mengine yatawasilishwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji / Mtaa kwa Afisa Mtendaji wa Kata yakiwa yameambatanishwa na Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji / Mtaa uliosainiwa na Mwenyekiti wa Kijiji /Mtaa pamoja na orodha ya wananchi waliohudhuria.

6.1.9.  Afisa Mtendaji wa Kata baada ya kupokea majina yaliyopendekezwa kutoka kwenye Mikutano Mikuu Maalum ya Vijiji / Mitaa ya Kata husika, ataitisha Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, ambacho kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0 kitachagua majina manne kwa kura ya siri kwa utaratibu ufuatao:-

6.1.9.1.    Kwanza, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu mzima mmoja [anaweza kuwa mwanamke au Mwanamme].

6.1.9.2.    Pili, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua Mwanamke mmoja.

6.1.9.3.    Tatu, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua Kijana mmoja [anaweza kuwa Mwanamme au Mwanamke].

6.1.9.4.    Nne, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu mwingine yeyote kutoka miongoni mwa wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya.

6.1.10.     Jina la Mwananchi atakayekuwa amepata kura nyingi kutoka kila kundi [Mtu mzima, Mwanamke, Kijana na Mtu mwingine yeyote] yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa yakiwa na Muhtasari uliosainiwa na Mwenyekiti na Katibu wa Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata kilichoyapigia kura majina hayo pamoja na orodha ya Wajumbe waliohudhuria.

6.1.11.     Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sifa na utaratibu ulioainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, atawasilisha majina kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa Uteuzi.

6.1.12. Endapo Diwani wa kata ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata hatakuwepo [Kwa sababu zozote ikiwa ni pamoja na kuwa safarini kwa kipindi ambacho Mabaraza ya Katiba yatafanyika, kuwa mgonjwa na kutoweza kutekeleza majukumu ya Udiwani, Kifo au sababu nyingine], utaratibu wa kawaida wa kumpata mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata wakati Diwani hayupo utatumika, ambapo Mwenyekiti wa Kijiji/Mtaa atakayependekezwa na Wajumbe wenzake wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kuendesha Kikao hicho ndiye atawakilisha kata badala ya Diwani.

6.2        Kwa Mkoa wa Dar es Salaam utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-

6.2.1.  Kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, kila Mwananchi wa Mtaa husika anayependa kuwa Mjumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa atawasilisha jina lake kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa. Uwasilishaji huo uambatane na taarifa zifuatazo:-

6.2.1.1.    Majina kamili ya mwombaji.
6.2.1.2.    Jinsi yake.
6.2.1.3.    Umri wake.
6.2.1.4.    Elimu yake.
6.2.1.5.    Kazi yake.
6.2.1.6.    Sehemu anayoishi katika Mtaa husika.

6.2.2.  Wakati wa uwasilishaji wa jina, kila mwananchi anayependa kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya, atawasilisha nakala mbili za barua kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa. Nakala moja ibaki kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa; na nakala ya pili iwekwe Mhuri na saini ya Afisa Mtendaji wa Mtaa. Nakala hiyo abaki nayo mwanachi husika kwa uthibitisho kuwa barua yake ilipokelewa.

6.2.3.    Orodha ya majina ya Wananchi wote wanaotaka kuwa wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, itawekwa kwenye maeneo ya wazi / matangazo ya Ofisi za Mtaa kwa siku saba (7) kabla ya Mkutano ili wananchi wa Mtaa husika wapate fursa ya kuyapitia na kujiridhisha kama walioomba wana sifa zilizoanishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0.

6.2.4.    Afisa Mtendaji wa Mtaa ataitisha Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa ambao utakuwa na agenda moja tu kuwapendekeza kwa kuwapigia kura ya siri watu Wanane watakaokuwa wajumbe wa Mabaraza ya katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

6.2.5.    Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa wa kuwachagua wananchi wanane (8) kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa utaendeshwa na Mwenyekiti wa Mtaa ambapo Afisa Mtendaji wa Mtaa atakuwa Katibu, na ndiye atakayewasilisha majina ya wananchi wote kwenye Mkutano huo walioomba kuingia kwenye Baraza la Katiba la Wilaya.

6.2.6.  Utaratibu wa kupiga kura za kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa wa kuwachagua Wananchi wanane wanaopendekezwa kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya utakuwa kama ifuatavyo:-

6.2.6.1.    Kwanza, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura ya siri ya kuwachagua Watu Wazima Wawili [wanaweza kuwa Wanawake au Wanaume].

6.2.6.2.    Pili, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura ya siri ya kuwachagua Wanawake wawili.

6.2.6.3.    Tatu, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura ya siri ya kuwachagua Vijana wawili [wanaweza kuwa Wanaume au Wanawake].

6.2.6.4.    Nne, Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa watapiga kura za siri kuwachagua Watu wengine wawili wowote kutoka miongoni mwa majina  yaliyowasilishwa kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa.

6.2.7.  Orodha ya majina ya Wananchi wanane waliopigiwa kura nyingi za kupendekezwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi/ matangazo ya kila Ofisi ya Serikali ya Mtaa.

6.2.8.  Majina ya watu wanane yatakayokuwa yamepata kura nyingi kuliko mengine, yatawasilishwa na Afisa Mtendaji wa Mtaa kwa Afisa Mtendaji wa Kata yakiwa yameambatanishwa na Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum wa Mtaa uliosainiwa na Mwenyekiti wa Mtaa pamoja na orodha ya Wananchi waliohudhuria.

6.2.9.  Afisa Mtendaji wa Kata baada ya kupokea majina yaliyopendekezwa kutoka kwenye Mikutano Mikuu Maalum ya Mitaa ya Kata husika, ataitisha Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, ambacho kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0 kitachagua majina manane kwa kura ya siri kwa utaratibu ufuatao:-

6.2.9.1.          Kwanza, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri ya kuwachagua Watu wazima wawili [wanaweza kuwa Wanawake au Wanaume].

6.2.9.2.    Pili, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri kuwachagua Wanawake wawili.
6.2.9.3.    Tatu, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri kuwachagua Vijana wawili [wanaweza kuwa wanaume au wanawake].

6.2.9.4.    Nne, Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watapiga kura ya siri kuwachagua watu wawili wengine wowote, kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwenye Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata.

6.2.10.               Majina ya Wananchi watakaokuwa wamepata kura nyingi kutoka kila kundi [Watu wazima wawili, Wanawake wawili, Vijana wawili na Watu wawili wengine] yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa yakiwa na Muhtasari uliosainiwa na Mwenyekiti na Katibu wa Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, kilichoyapigia kura majina hayo pamoja na orodha ya Wajumbe waliohudhuria.

6.2.11. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sifa na utaratibu ulioainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, atawasilisha majina kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa Uteuzi.

6.2.12. Endapo Diwani wa Kata ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata hatakuwepo [Kwa sababu zozote ikiwa ni pamoja na kuwa safarini kwa kipindi ambacho Mabaraza ya Katiba yatafanyika, kuwa mgonjwa na kutoweza kutekeleza majukumu ya Udiwani, kifo au sababu nyingine], utaratibu wa kawaida wa kumpata Mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata wakati Diwani hayupo utatumika, ambapo Mwenyekiti wa Mtaa atakayependekezwa na Wajumbe wenzake wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kuendesha Kikao hicho ndiye atawakilisha kata badala ya Diwani.


6.3        Kwa upande wa Zanzibar utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-

6.3.1.  Kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, kila Mwananchi Mkaazi wa Shehia husika anayependa kuwa mjumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa atawasilisha jina lake kwa Sheha. Uwasilishaji huo uambatane na taarifa zifuatazo:-

6.3.1.1.  Majina kamili ya mwombaji.
6.3.1.2.  Jinsi yake.
6.3.1.3.  Umri wake.
6.3.1.4.  Elimu yake.
6.3.1.5.  Kazi yake.
6.3.1.6.  Sehemu anayoishi katika Shehia husika.

6.3.2.  Wakati wa uwasilishaji wa jina, kila Mwananchi anayependa kuwa Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya, atawasilisha nakala mbili za barua kwa Sheha. Nakala moja ibaki kwa Sheha; na nakala ya pili iwekwe Mhuri na saini ya Sheha. Nakala hiyo abaki nayo Mwanachi husika kwa uthibitisho kuwa barua yake ilipokelewa.

6.3.3.  Orodha ya majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yatabandikwa kwenye maeneo ya wazi (mfano Skuli) / matangazo katika Shehia husika siku saba (7) kabla ya Mkutano ili Wananchi wapate fursa ya kuyapitia na kujiridhisha kama walioomba wana sifa zilizoanishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0.

6.3.4.  Sheha ataitisha Mkutano wa Shehia husika ambao utakuwa na agenda moja tu ya kuwapigia kura ya siri watu watatu [3] ambao majina yao yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri Mji/ Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo.

6.3.5.  Mkutano wa Shehia utachagua Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano huo kutoka miongoni mwa Wananchi waliohudhuria Mkutano. Katibu ndiye atakayewasilisha kwenye Mkutano majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

6.3.6.    Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano wa Shehia watakaochaguliwa sharti wawe na sifa kama za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba zilivyoainishwa katika aya ya 4.0.

6.3.7.  Utaratibu wa kupiga kura kwenye Mkutano wa Shehia wa kuwachagua Wananchi watatu kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya utakuwa kama ifuatavyo:-

6.3.7.1.    Kwanza, Wananchi wote waliohudhuria Mkutano wa Shehia watapiga kura ya siri ya kumchagua Mtu mzima mmoja [anaweza kuwa Mwanamke au Mwanamme].

6.3.7.2.    Pili, Wananchi wote waliohudhuria Mkutano wa Shehia watapiga kura ya siri ya kumchagua Mwanamke mmoja.

6.3.7.3.    Tatu, Wananchi wote waliohudhuria Mkutano wa Shehia watapiga kura ya siri ya kumchagua Kijana mmoja [anaweza kuwa Mwanamme au Mwanamke].

6.3.8.    Matokeo ya upigaji kura wa siri yatatangazwa kwenye Mkutano baada ya mchakato wa kupiga kura kukamilika na kuwekwa kwenye maeneo ya wazi / matangazo katika Shehia husika.

6.3.9.    Katibu wa Mkutano wa Shehia, atawasilisha majina ya watu watatu (3) waliochaguliwa katika Mikutano ya Shehia kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji / Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo katika muda wa siku moja tangu Mkutano ulipofanyika. Mawasilisho hayo yaambatane na muhtasari wa Mkutano uliotiwa saini na Mwenyekiti na Katibu pamoja na orodha ya majina ya wananchi waliohudhuria.

6.3.10. Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri Mji/ Wilaya kwa kuzingatia sifa na utaratibu ulioainishwa kwenye aya za 4.0 na 5.0, atawasilisha majina kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa uteuzi.

Baada ya kupokea orodha ya majina ya watu waliochaguliwa kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Katibu atatoa barua rasmi za kuwateua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

 7.0. TARATIBU ZA KUFANYA MIKUTANO YA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA.

Ili kuendana na muda wa kuwapata Wajumbe na kufanyika kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na maandalizi yote muhimu, vikao vya kupendekeza majina na kufanya uchaguzi vitafanyika kwa utaratibu ufuatao:-

7.1        Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wawasilishe majina yao kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji / Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa Sheha kwa Zanzibar kati ya tarehe 08 Machi, 2013 hadi 20 Machi, 2013.

7.2        Orodha ya majina ya Wananchi wote wanaotaka kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya  ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa iwekwe kwenye maeneo ya wazi / matangazo katika Ofisi za Vijiji / Mitaa kwa Tanzania Bara; na katika maeneo ya wazi / matangazo kwenye Shehia husika kwa Zanzibar tarehe 22 Machi, 2013 na majina hayo yaendelee kuwepo hadi tarehe 28 Machi, 2013.

7.3        Kwa Tanzania Bara, Vikao vya Vijiji / Mitaa vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri wananchi wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba vifanyike kati ya tarehe 30 Machi 2013 hadi 03 Aprili, 2013.

7.4        Kwa upande wa Tanzania Bara, Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata cha kuwachagua wajumbe wanne kutoka miongoni mwa Wananchi waliopigiwa kura na Mikutano Mikuu ya Vijiji / Mitaa kifanyike kati ya tarehe 05 Aprili 2013  hadi 09 Aprili, 2013.

7.5        Kwa Tanzania Bara, majina ya Wajumbe wanne waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya tarehe 13 Aprili, 2013 hadi 17 Aprili, 2013.

7.6        Kwa Mkoa wa Dar es Salaam,
7.6.1.  Vikao vya Mitaa vya kuwapigia kura ya kuwapendekeza wajumbe wanane wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 Machi, 2013 hadi 03 Aprili, 2013.

7.6.2.  Vikao Maalum vya Kamati za Maendeleo za Kata vya kuwachagua wajumbe wanane kutoka miongoni mwa wananchi waliopigiwa kura na Mikutano Mikuu ya Mitaa vifanyike kati ya tarehe 05 Aprili, 2013 hadi 09 Aprili, 2013.

7.6.3.  Majina ya Wajumbe wanane waliochaguliwa na Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika kati ya tarehe 13 Aprili 2013  hadi 17 Aprili, 2013.

7.7        Kwa Zanzibar,
7.7.1.              Vikao vya Shehia vya kuwachagua kwa kuwapigia kura za siri Wananchi watatu kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba  ya Wilaya vifanyike kati ya tarehe 30 Machi, 2013 hadi 03 Aprili, 2013. 
7.7.2.               Majina ya Wajumbe watatu, waliochaguliwa na Mikutano ya Shehia, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji / Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo kati ya tarehe 13 Aprili 2013 hadi 17 Aprili, 2013.

Majina ya watu wote waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, pamoja na majina ya Madiwani wote wa Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika yawasilishwe kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutumia Fomu maalum iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa madhumuni hayo kwa njia ya nakala tete (soft Copy) na nakala mango (hard copy) kati ya tarehe 25 Aprili 2013 hadi 30 Aprili, 2013.

 8.0. MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA MCHAKATO WA KUWAPATA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA
Ni Jukumu la Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia, kuratibu na kuhakikisha Mikutano hiyo inafanyika.

8.1       Kwa Tanzania Bara isipokuwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam

8.1.1.Mikutano yote ya Vijiji / Mitaa itaendeshwa na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji / Mitaa na Maafisa Watendaji wa Vijiji / Mitaa watakuwa ni Makatibu na wasimamizi wa Mikutano hiyo.

8.1.2.Mikutano Mikuu yote ya Vijiji / Mitaa itakayoitishwa kwa lengo la kuwapigia kura ya siri watu wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya vifanyike katika tarehe moja kwenye Vijiji / Mitaa yote iliyopo kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.

8.1.3.Vikao vyote vya Kamati za Maendeleo za Kata vitakavyokuwa na jukumu la kuwachagua watu wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa vifanyike katika tarehe moja kwenye Kata zote za Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.8.1.4.  Kwa Mkoa wa Dar es Salaam:

8.1.4.1.    Mikutano Mikuu yote ya Mitaa itakayoitishwa kwa lengo la kuwapigia kura watu wanane wanaopendekezwa kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ifanyike katika tarehe moja kwenye Mitaa yote iliyopo kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.

8.1.4.2.     Vikao vyote vya Kamati za Maendeleo za Kata vitakavyokuwa na jukumu la kuwachagua watu wanane kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa vifanyike katika tarehe moja kwenye Kata zote za Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.
8.2                    Kwa Zanzibar

8.2.1.  Ni jukumu la Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji / Wilaya kusimamia, kuratibu na kuhakikisha Mikutano hiyo inafanyika.

8.2.2.  Mikutano yote ya Shehia itaendeshwa na Wenyeviti na Makatibu watakaochaguliwa na Mikutano hiyo.

8.2.3.  Jukumu la Sheha ni:-

8.2.3.1.    Kupokea majina ya Wananchi wanaoomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.

8.2.3.2.    Kubandika katika maeneo ya wazi / matangazo majina yote ya watu walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.

8.2.3.3.    Kuitisha Mkutano wa Shehia utakaochagua Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano.

8.2.4.  Majukumu ya Katibu wa Mkutano atakayechaguliwa:-
8.2.4.1.    Kupokea orodha ya majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutoka kwa Sheha.

8.2.4.2.    Kuwasilisha majina ya Wananchi wote walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwenye Mkutano.
8.2.4.3.    Kuratibu mchakato wa uchaguzi kwenye Mkutano.

8.2.4.4.    Kubandika kwenye maeneo ya wazi / matangazo matokeo ya kura kwa kila mwombaji alivyopata baada ya Mkutano.

8.2.4.5.    Kuandaa Muhtasari wa Mkutano.

8.2.4.6.    Kuwasilisha majina ya Wananchi walioshinda pamoja na Muhtasari wa Mkutano kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa iliyopo kwenye Shehia husika.
 9.0. MABARAZA YA KATIBA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI YA WATU

Kama ilivyoelezwa hapo awali, Kifungu cha 18 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba.  Tume inaruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume si zaidi ya tarehe 14 Agosti, 2013.

Mabaraza hayo yatajiendesha yenyewe na kuwasilisha maoni yao kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Orodha ya Mabaraza hayo ni pamoja na:
1.1.      Jumuiya ya kidini.
1.2.      Chama cha siasa.
1.3.      Asasi ya kiraia.
1.4.      Taasisi ya elimu ya juu.
1.5.      Chama cha wafanyakazi.
1.6.      Chama cha wakulima.
1.7.      Chama cha wafugaji.
1.8.      Chama cha Wanahabari.
1.9.      Mabaraza ya Watoto, Taasisi za Kitaaluma, Vijana na Wazee.
1.10.   Kundi au makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kama Sheria inavyoelekeza.
1.11.    Kundi au makundi ya watu wenye mahitaji maalum katika jamii.
 
10.0.   TAREHE YA KUANZA KUTUMIKA
Mwongozo huu utaanza kutumika kuanzia tarehe 01 Machi, 2013.


Joseph S. Warioba
Mwenyekiti
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA