Home » » TAMKO LA VIJANA DHIDI YA CHOKOCHOKO NDANI YA KANISA LETU NA USHARIKA WETU

TAMKO LA VIJANA DHIDI YA CHOKOCHOKO NDANI YA KANISA LETU NA USHARIKA WETU

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Saturday, July 28, 2012 | 2:51 PM

Kanisa la KKKT usharika wa kanisa kuu
Askofu Dkt Mdegella

A: UTANGULIZI

”BWANA yuko mbali na waovu, bali husikia maombi ya wenye haki” (Mith 15:29)

1. Awali ya yote kama vijana wa Kanisa Kuu tumefikishwa mahali ambapo lazima tuseme na kutenda. Tumechoshwa kabisa na chokochoko zisizoisha. Tumechoshwa kuona matusi yasiyotamkika kwenye mitaa, mabango, mitaro na kwenye vituo vya makusanyiko ya watu dhidi ya Askofu wetu. Mambo hayo mabaya yamefikia hatua ya kutufungia lango la Kanisa sisi tusiohusika, eti kwa kisingizio cha kumfungia Askofu ambaye hakuwepo kanisani wala hata ndani ya mji.

2. Sisi tunapenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai na kutuimarisha zaidi na zaidi katika kumtumikia Mungu kupitia vipawa mbalimbali tulivyojaliwa na Mungu. Pamoja na tofauti ya vipawa hivyo mbalimbali, sote kwa pamoja kama Wakristo tunashirikiana vyema katika kueneza Injili na kuujenga mwili wa Kristo, kwa maana ndilo kusudi la Mungu katika wito wetu.

3. Kwa kuzingatia misingi ya Neno la Mungu (Ezekiel 3:17-58), Mungu anamtaka kila mwanadamu bila kujali umri wake awe mwangalizi wa Kanisa dhidi ya watenda mabaya. Kama vijana tunatumia fursa hii na wajibu huu kusimamia na kukemea maovu yote yanayotendeka yenye lengo la kutaka kuharibu na kusambaratisha kanisa la Mungu.

4. Chokochoko ndani ya kanisa letu zina historia ndefu iliyojigawa sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni lile vuguvugu la kudai Dayosisi ya Ilula ambalo halikuweza kufaulu kwa kukosa sifa mahususi za kupewa hadhi ya kidayosisi. Sehemu ya pili inaonekana wazi kuwa ni njia mbadala ya sehemu ya kwanza. Wale wale waliodai Dayosisi sasa wameingiwa na tamaa ya kupata madaraka bila kutumia katiba na njia halali za Kanisa. Njia wanazotumia hazitofautiani na njama za kumpindua kwa njia ya kumchafua na kumtupia madongo kiongozi aliyepo. Kundi lile lile la kutaka kuupindua uongozi wa Dayosisi la miaka ya nyuma ndilo linashawishi watu kwa kusema uwongo uliokithiri ili nafasi hizo zichukuliwe na hao watu. Jambo hili limedhihirika kwa vikao vilivyofanyika Image, Ilula, na katika maeneo kadhaa ya Manispaa ya Iringa kama vile Mkimbizi, Mkwawa, Kijiweni, Chuo Kikuu Tumaini (maofisini na majumbani kwa watu), Gangilonga B na maeneo mengine kadhaa tunayoyafahamu.

5. Baada ya kuona msimamo wa Halmashauri Kuu ni kinyume chao wahusika waliamua kukaidi maamuzi ya Halmashauri Kuu na kutaka kufanya maandamano ambayo yalikuwa na nia ya kuendeleza chokochoko na kupinga maamuzi halali ya chombo cha Kikatiba. Waliposhindwa kufanya maandamano waliendelea na matusi yenye masingizio yasiyotamkika kinywani mwa Mkristo. Matusi na masingizio hayo yalisambazwa kwa nyaraka na matangazo barabarani na popote walipoweza kutawanya. Kwa wakazi wa Iringa mtu anayetukana kwa mtindo wa hao wanamtandao huwa tunasema amekosa hoja kabisa. Kwahiyo sisi vijana tunasema hivi: Hali tukiwa tumekwisha onywa nafsini mwetu kwa nguvu ya Neno la Mungu lisemalo ”Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu, au kumnyima asiye na hatia haki” (Mithali 18:5), basi kwa nguvu zote tunainua sauti zetu pamoja na vijana wengine wote kukemea uovu unaotendwa na wanamtandao na wote wanaowasaidia kwa kuwa wanalitesa Kanisa la Yesu Kristo.

B: KIBURI CHA WANA MTANDAO

6. `Wahusika wa chokochoko hizi wako kwenye mtandao unaowapa fedha, kiburi na ujeuri wa kuzimu. Kiburi cha waasi wa kanisa kinaonekana kusaidiwa kwa karibu na Mkuu wa KKKT na kwa msaada wa baadhi ya Maaskofu. Wao wenyewe wamekiri kwenye vikao rasmi vya Dayosisi kwamba Mkuu KKKT anashiriki kwa njia ya kuwaita kwenye mikutano ya Baraza la Maaskofu, Mikutano rasmi ya KKKT kama vile ule Mkutano Mkuu wa Morogoro wa July 2011. Pia amehusika kwa kuwawezesha kifedha ili kumudu mipango yao ikiwa ni pamoja na kuwagharamia safari, malazi na kujikimu.

7. Kwa upande wa Maaskofu, hatukuona mwelekeo wa namna jambo lilivyoingia katika Dayosisi. Tafsiri tuliyopata ni wao kuunda tume ya kumtenga Askofu na vyombo vya maamuzi vya Dayosisi ili kumshambulia Askofu kwa kusudi la kumng’oa. Wanamtandao walitangaza zaidi ya mara kumi tangu mwaka 2010 kwamba tarehe fulani Askofu atang’olewa na wao na maaskofu wenzake. Wanamtandao hao waliotumika pia kutoa mahubiri yenye kuhamasisha watu wamng’oe Askofu wao. Walipitisha fomu ya kujaza majina ya kumkataa Askofu hata vilabuni. Mara zote walikuwa wanajua kabisa ni tarehe ipi maaskofu watakaa wapi na agenda ninini halafu walitangaza mjini na baadhi ya vijiji. Ujio wa kwanza na wa pili wa Maaskofu Dkt Hance Mwakabana, Dkt Martin Shao na Elisa Buberwa ulitangazwa mjini na baadhi ya vijiji siku kadhaa kabla ya ujio wenyewe. Tangazo hilo lilienda sambamba na unabii wa uwongo wa kung’olewa kwa Askofu.

8. Haikuwa ni jambo rahisi kutambua azma yao kwa wazi lakini kupitia nyaraka, matamko na matukio yanayohusu wao na uhusiano wao na Mkuu KKKT na mikutano ya Baraza la Maaskofu azma yao ilijulikana na siyo siri tena. Iko wazi kabisa kuwa Wanamtandao na baadhi ya Maaskofu wanaojulikana kwa wazi kabisa wamedhihirika kwa wazi kwamba lengo lao ni kufanya mapinduzi katika Dayosisi ya Iringa na mahali pa kuanzia ni kumng’oa Askofu Dkt. Owdenburg Moses Mdegella.

9. Hili limetuuma sana na ni kitu ambacho ni kuikosea Dayosisi ya Iringa na ni kinyume kabisa cha taratibu za kimaongozi na za Kikatiba, kiuongozi na kiutawala. Yaani Dayosisi ya Iringa ichague Askofu halafu watokee watu wachache wenye nia mbaya, wenye hila na fitina kisha wamwondoe Askofu bila maelezo ya wazi ya huko kumng’oa! Baadhi ya nyaraka za siri za Baraza la Maaskofu ambazo wanamtandao waliwaonyesha au kuwatamkia marafiki zao zilikuwa na kejeli za ajabu kama vile kumwita Askofu wetu Ibilisi mwenye mapembe. Ifuatayo ni sehemu tu ya nukuu katika waraka mmojawapo wa siri.

Ukiamua kupambana na ibilisi na kazi zake unamkabili vilivyo kwa kumwendea moja kwa moja kwa kumshika mapembe yake yote mawili kwa ujasiri mpaka unamwangusha chini. Sio kumwendea kama kwa kunyatianyatia hivi huko uwoga umekujaa na unaendelea kumtishia kwa sauti hafifu ya mbali…(Waraka huu ulipatikana kwa Mfanyabiashara wa Soko Kuu Iringa mwenye kibanda mkabala na Kanisa Kuu na uliandikwa na kutiwa saini na Maaskofu watatu waliokuja Iringa).

10. Hii sio kauli ya Kiaskofu wala Kichungaji dhidi ya mtu ambaye hujathibitishiwa tuhuma zake. Maaskofu hao watatu walikuja Iringa mara zote wakiwa na maamuzi mabaya dhidi ya Askofu wetu ila hawakutuambia. Ndiyo maana agenda yao haikueleweka na walitumia njia za kificho na udanganyifu kama siyo wana wa nuruni. Walijifanya wanachunguza jambo ambalo hatima ya jambo hilo walikuwa nayo tayari mikononi mwao. Wao walikwisha toa hukumu kabla kesi haijafika mahakamani na bila kuleta mshitaki na mshitakiwa pamoja ili wajibizane. Kwa mfano wanaposema ana watoto nje ya ndoa, mbona hawakuwaleta hao wenye watoto ambao baadhi ya wanaotajwa wapo hapa Iringa au hawakutaka Msaidizi wa Askofu na Wakuu wa majimbo wawape taaarifa za msingi? Wanaposema kuna ubadhirifu wa fedha, mbona hawakuonyesha hata mfano mmoja wa wakaguzi wanaoweza kuthibitisha hilo? Je, huo siyo uzushi na majungu? Wanapotaja upendeleo kwenye ajira, mbona hawakuuliza wanaohusika na ajira? Kwetu sisi vijana haikuwa rahisi kuamini kuwa waraka huo umetoka kwa Maaskofu. Tunaogopa sana kupewa huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti na kutangaziwa msamaha kwa watumishi wa Mungu wenye hila kiasi hiki maana wanazijua haki za msingi za Kibiblia, Kisheria, Kikatiba na kibinadamu lakini walizivunja kwa wazi na badala yake wakatetea watu waliofanya madhambi makubwa kama akina Betson Sevetu.

11. Haki za mtu zinatafutwa kwenye Baraza la Maaskofu? Je, Uibilisi ni upi kati ya kutoheshimu vyombo halali vya udhibiti wa taratibu za Kanisa, katiba na kiutendaji au mtu akionewa ndiyo anakuwa Ibilisi? Kwahiyo Baraza la Maaskofu ni mahakama, ni chombo cha ukaguzi na ni mamalaka ya kuamrisha Halmashauri Kuu ya DIRA? Je, Baraza hilo ndicho chombo cha ukaguzi wa ndani na wa nje wa DIRA na Chuo Kikuu pamoja na Taasisi za DIRA? Kwanini Baraza la Maaskofu linafumbia macho uwongo na ulaghai wa wazi? Uibilisi wa Mdegella haujawahi kupelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya Dayosisi au kwenye Bodi ya Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa ama kwenye Taasisi kubwa zenye Bodi kama vile hospitali ya Ilula na Bodi za Shule. Kwahiyo kwa mawazo ya hao Maaskofu hata Halmashauri Kuu na watendaji wasaidizi wa Askofu na wasimamizi wa taasisis zote ni Maibilisi? Uibilisi huo haujawahi kuzungumzwa na kikao chochote cha DIRA kwakuwa wana DIRA wote ni Maibilisi? Tunabainisha kuwa mpaka sasa Maaskofu hujiona wao kuwa ni miungu watu. Kwamba kwa hao Maaskofu anayetukanwa ndiye Ibilisi ila wao wanaotukana na mtandao wao ndio malaika. Tunaomba kujua kutoka kwa hao Maaskofu. Kwani matusi ni ya nani, ni ya Mungu au Shetani? Hivi kumwita Askofu mwenzao Ibilisi siyo tusi? Sisi hatujawahi kuona dharau kubwa ya namna hii inayofanywa na watu wakubwa namna hii (ambao hawakudhaniwa) dhidi ya Askofu wa Iringa na vyombo vyake vya kimaamuzi.

12. Mpaka sasa hakuna hata tuhuma moja iliyothibitishwa. Tarehe 15/1/2012 tulidhani Maaskofu wale watatu wangewaleta wale wanaopatanishwa na Akofu Dkt. Mdegella. Kinyume chake walipatanisha watu hewa. Sisi tunaamini hata hizo tuhuma ni hewa. Siasa hizi hazifai kanisani. Kutokana na kutothibitishwa kwa tuhuma hata moja na njama za mtandao kugonga mwamba inatufanya sisi tuthibitishe kwamba hizi zote ni hila za kimapinduzi dhidi Askofu Dkt. Mdeglla na uongozi wa Dayosisi ya Iringa. Na hiki ni kielelezo cha uwakili mbaya wa uongozi, mamlaka na sadaka na rasalimali watu fedha na wakati. Huku ni kuwaumiza maskini na kutumia vibaya sadaka zao.

13. Chombo kikuu kinachotumiwa na maaskofu ni ule mtandao dhalimu ambao miongoni mwao ni pamoja na wale waliovuliwa uchungaji. Cha ajabu na cha kusikitisha sana ni pale kuona Mkuu KKKT anapoamua kufanya kazi na watu waliopoteza mwelekeo kiimani, wanaohubiri chuki na matusi. Waongo, wafitini na wazushi. Sisi vijana tunashangaa kuona Maaskofu wanashirikiana na mtandao huo bega kwa bega na kufanyia kazi mambo ya kizushi yanayowasilishwa mezani pake Mkuu KKKT kinyume na taratibu za Kikristo na kisheria kwa wazi kabisa.

14. Kwa utaratibu wa Kikristo kiongozi yeyote wa Kanisa hufanya mambo yake kwa kuheshimu Neno la Mungu, taratibu zilizokubaliwa na Wakristo wote na Katiba ya mahali husika na sheria ya nchi ambayo huwalinda raia wote. Unashangaa kuona watu wasomi kama Maaskofu wakishindwa kumshauri Mkuu KKKT juu ya makosa ya wazi anayofanya. Jambo lolote linalowasilishwa kwa Mkuu wa Kanisa ni lile ambalo limefanyiwa kazi na kuwekewa patano la kimaamuzi kupitia Halmashauri Kuu ya Dayosisi, ndipo sasa kwa idhini ya mamlaka hiyo jambo hilo lisimamiwe na Mkuu wa Kanisa moja kwa moja, au kupitia wajumbe wake. Lakini hatua hii hufikiwa endapo tu jambo linalo lalamikiwa linakuwa na walalamikaji wa wazi. Siyo mtandao wala barua za matusi mitaani na kwenye mitandao na zenye majina ya kujibandika kama Nyaruke Amani na mengineyo. Halmashauri Kuu ya Dayosisi ilikataa kujiingiza kwenye uchunguzi wa barua zisizo na sahihi na majina ya uwongo. Ungetazamia Mkuu aiombe Halmashauri Kuu ichunguze na kuthibitisha tuhuma zinazotajwa. Ungetazamia siku Maaskofu walipokutana na Halmashauri Kuu waseme ni nini kilichunguzwa na Halmashauri hiyo pamoja na wao na kuthibitika kwamba tuhuma zinazo mkabili mlalamikiwa ni za kweli na ni ukweli mtupu. Hii ni aibu sana kwa Kanisa kufanyia kazi mambo ya kizushi na majungu na kuacha mambo ya msingi ambayo kwayo Kanisa liliitiwa.

15. Baadhi ya vijana walihisiwa kwamba ni kikundi cha Askofu Dkt. Mdegella cha kufanya fujo. Tunaomba tueleweke kwamba sisi kwa muda wote wa chokochoko tulikuwa tunawatafuta hao waandishi wa makala, vipeperushi na barua pepe na zile zisizo sainiwa. Tunasema kwa uhakika kabisa kwamba sisi tulijiunda wenyewe kwa siri hata bila Askofu kujua. Alitujua tulipokuwa na hasira na akatusaidia sana tusitende kwa hasira Mara nyingi alisema,”Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu” (Yakobo 1:20), ”hasira ni hasara’ na ”hasira za mkizi ni kujiumiza mwenyewe”. Wakati mwingine tulipochachamaa alitupeleka kwa viongozi wa usalama wa raia ili kutushauri. Kwahiyo tunajulikana na agenda yetu siyo ya siri. Mwacheni Mdegella wa watu. Kanisa linapaswa kumshukuru Askofu Dkt. Mdegella kwa Uchungaji wake wa hali ya juu. Vinginevyo Iringa ingekuwa na hadithi tofauti. Ikumbukwe kwamba chokochoko ndani ya Dayosisi ya Iringa zimeenezwa kwa njia ya vipeperushi, barua zisizosainiwa wala kutaja majina ya waandishi. Barua pepe zimekuwa na majina ya bandia. Mambo yaliyoenezwa kwenye vyombo vya habari yamekithiri kwa uchafu na uwongo. Sisi vijana tulijiuliza; Mbona Kanisa halijawahi kukemea huo uchafu na uwongo wa wazi? Mbona halijawahi kuwakemea hao waandishi? Tulichoshangaa ni pale ambapo tulilazimika kuamini kwamba Mkuu KKKT na baadhi ya maaskofu ni wadau wa huo uchafuzi. Tumeumia zaidi tulipofahamu kwamba kiongozi wa mtandao huo alikwenda Dar-Es- Salaam kukutana na wanamtandao wenzake ikiwa ni pamoja na Mkuu KKKT ili kujisifia kwamba walitufungia Kanisa. Mkuu KKKT na Maaskofu wanataka sisi vijana wachanga wa imani tuwaelewe vipi? Ni nini tofauti yao sasa na wanamtandao? Mbona hawana huruma? Sisi tunaamini kuwa mambo yote yaliyoandikwa na kusemwa bila majina halisi wala sahihi za waandishi, au mambo yaliyosemwa na Lawrence Mtatifikolo na Redio Ebony FM na yale yaliyotangazwa kwenye vyombo vingine vyovyote vya habari ni uchafu wa Kishetani uliovuka mipaka na uliotungwa kuzimu. Kinachotuuma sana ni kwamba viongozi wetu wanaamini hayo mambo machafu. Tumefika hatua ya kukosa imani kabisa na uongozi wa Kanisa letu. Tutairudisha mioyo yetu kanisani kwa kulitetea Kanisa na si mtu wala kikundi. Tunabaki kanisani na hatukimbii. Tutaitetea imani yetu na Dayosisi yetu dhidi ya laana na unajisi unaoenezwa na kikundi kidogo kilichofundishwa na mamalaka ya kuzimu kwa gharama zozote zile.

16. Kwa wasomaji wa Biblia, habari ya watu kulichafua Kanisa si jambo lililo geni. Yalikuwepo matukio mengi Kibiblia yanayodhihirisha haya yote. Kwa mfano Wafilisti waliokuwa wakilitukana taifa la Israeli (1Samweli 17:20-58) - Mungu hakuacha kuwaadhibu watu wale. Pia mtumishi wa Mungu Elisha alidhihakiwa kwa kuambiwa paa we mwenye upaa (2Wafalme 2:23-24). Na kama tu haitoshi, hata Yesu alipambana na waasi wa mbali na wakaribu. Yesu alisalitiwa na kisha kulazimisha auawe na kazi hiyo ilifanywa na viongozi wa dini. Yakobo, Askofu wa kwanza Yerusalemu aliuawa kwa ushawishi wa Kuhani Mkuu wa Wayahudi, yaani kiongozi wa dini. Huyo aliyemtuma Lawrence Mtatifikolo kufunga kanisa hana tofauti kabisa na Yuda Iskariot. Amehongwa au anatumia vipesa alivyookoteza kwa kulihujumu Kanisa na miradi ya wafadhili. Kwa mantiki hiyo kusaliti na kusalitiwa si jambo geni ila lina gharama kubwa sana kwa msaliti. Mtu anayefanya hivyo tunamuonya kuwa asidhani watu wanaoomba hawasikilizwi na Mungu. Sisi vijana tumeona wazazi wetu na babu zetu na nyanya zetu wakiugua hata kulazwa hospitalini kwa ajili ya matusi na uchafuzi huu uliokithiri. Kitendo cha kufunga Kanisa karibu kisababishe vifo vya Wakristo wazee hapa Iringa mjini na vijijini. Ndiyo maana tumesema hatuko tayari kuona jambo hili linaendelea na tunasema liliisha tarehe 15/1/2012. Kinachoendelea sasa ni uhuni tu na tutakabiliana nao kwa hali yoyote na kwa njia yoyote iliyo ya haki na halali, lakini siyo mikutano na Maaskofu. Maamuzi ya halmashauri Kuu DIRA ni ukomo wa njia na tunasubiri kwa hamu kuona Mkutano Mkuu ukituunga mkono. Tunahakika na tunaomba kwa Mungu kwamba endapo mtu au mwanamtandao ataendelea kufanya hayo machukizo kwa hila zake mwenyewe, hakika hatakosa kupatwa na ghadhabu ya Mungu.

C: HATUA ZA KIDAYOSISI KUDHIBITI CHOKOCHOKO

17. Vipo vikao vingi vilivyokaliwa kwa ngazi za Dayosisi kuweza kujifunza chanzo cha chokochoko hizo ambazo mpaka sasa msingi wake hautambulikani. Mlolongo wa kutafuta suluhu za tofauti zilizokuwapo ni kama ifuatavyo:

(i) Mnamo mwezi Agosi 2010, Askofu aliiarifu ofisi yake na Dayosisi nzima juu ya choko choko zilizoanza mwaka 2009. Ofisi kuu kwa kupitia andiko lililosema ‘NJOONI MTOFAUTISHE KATI YA WANA WA MUNGU NA WANA WA IBILISI’ ilisemwa kwamba mwenye malalamiko aje aseme kwa utaratibu. Hakuna aliyejitokeza.

(ii) Tarehe 15/09/2010 kupitia Mkutano wa Wachungaji uliokuwa Pommern wito huo ulirejewa tena na Wachungaji waliamua kwa pamoja na hao wasaliti wakiwepo na wakaweka patano kwamba mwenye hoja ajitokeze kwa wakuu wa majimbo au msaidizi wa Askofu la sivyo jambo likome. Lakini hakuna aliyejitokeza.

(iii) Tarehe 17-18/5/2011 Uongozi wa Ofisi Kuu ulikutana na Wachungaji wa Chuo Kikuu cha Tumaini ili kutaka kujua kama kuna neno lolote toka huko Chuoni. Kilichotokea ni kwamba mazungumzo yote yaliyofanyika siku hiyo yalipelekwa kwenye mtandao na hao akina Nyaruke Amani. Nia yao ni kutaka Kanisa liunde tume. Kikao kile kiliamini kwamba chanzo na msingi wa mambo yote ni chuki binafsi.

(iv) Tarehe 9/6/2011 waliokuwa wachungaji, Lambert Mtatifikolo, Betson Sevetu na wachungaji wengine wawili waliitwa na kuhojiwa na walikiri kuhusika na baadhi ya nyaraka na matusi. Lambert alikiri kuwa aligawa barua zinazomkashifu Askofu kwa baaadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu na wazee wa kanisa. Alikiri pia kwamba alisema “Askofu na Itiweni Luhwago ni wapumbavu. Hakuchukuliwa hatua kwa sababu aliomba msamaha kwa machozi, akapiga magoti akaombewa na kukumbatiana na Askofu kwamba yamekwisha. Betson Sevetu pia alikiri kushiriki kutoa taarifa zisizothibitishwa kama vile kusema Askofu ana watoto nje ya ndoa na kueleza kuwa alikuwa na ugomvi au chuki binafsi na Askofu. Maelezo yake yalionyesha wazi kuwa ni mshiriki wa matusi na uchafuzi. Huyu pia alikiri kufanya makosa na kuomba radhi kwa machozi. Alikiri pia juu ya matatizo yake ya ndoa na kusema wazi kuwa alikuwa amepoteza sifa za Kichungaji. Kwa namna alivyokiri kwa machozi alisamehewa. Lakini baadaye aliendelea kurudia kufanya uchafuzi. Bila shaka kuna nguvu iliyokuwa inamtia moyo nyuma yake na si nyingine zaidi ya ile iliyomtetetea alipofukuzwa kazi.

(v) Tarehe 29/9/2011 Mkutano wa Uongozi wa Dayosisi na Uongozi wa Chuo Kikuu ulikaa Chuo Kikuu cha Tumaini- Tawi la Iringa. Lambert Mtatifikolo alipohojiwa juu ya chokochoko zinazoendelea alikataa kujibu lolote isipokuwa kusema kwamba ataenda kujibia Polisi. Hata hivyo kikao kilitoa maazimio mawili. Kwamba Betson Sevetu arudishwe DIRA na Lambert alishauriwa akutane na Askofu wakiwa wao wawili na wamalize tofauti zao. Kikao kilipangwa kiwe tarehe 4/10/2011 River Side Camp kwa gharama ya Chuo. Lambert alikataa kwa dharau kubwa bila shaka kwa ushauri wa wanamtandao wake.

(vi) Tarehe 10/10/2011 Mkutano wa Maaskofu uliofanyikia pale Huruma Centre uliomba haya mambo yote yamalizwe na Dayosisi kwa kushirikiana na Maaskofu watatu ambao walitumwa tena na Mkuu KKKT.

(vii) Tarehe 11 – 14/01/2012 Maaskofu watatu walichunguza jambo hili na kushindwa kupata sababu za msingi, na tarehe 14/1/2012 usiku wa manane waliiambia Halmashauri Kuu kwamba jambo limeisha. Wahusika wamesameheana na kwamba watatoa tangazo kanisani kwa Ibada maalum tatu. Tarehe 15/01/2012 lilotolewa tamko kwamba mambo yote yamekwisha na kwamba hatua zingine zitakamilishwa na Dayosisi husika. Hitimisho lake lilikuwa ni kwamba atakayeendelea na mambo ya namna hii ya kizushi “Huyo si mwenzetu, siyo mwana KKKT na tumkatae”. Cha ajabu ni kwamba tulioshiriki tuliona mambo yamefika mwisho maana tuliungama, tukaomba na kuimba pamoja wimbo wa “Bwana Uliyewaita Watakatifu Wako” ulioimbwa na Wachungaji na Maaskofu wote wanne yaani Askofu wetu na wale Maaskofu watatu.

(viii) Tarehe 11/07/2012, kwa bahati nzuri tulikutana na Hophman Kihonza pale Readio Ebony FM ili atueleze wazi sababu za kueneza uwongo kwamba aligawanya waraka kwa kutumwa na Msaidizi wa Askofu DIRA ili kuwajulisha watu uovu wa Askofu Dkt. Mdegella na kasha awasainishe watu kura ya kutokuwa na imani na Askofu Dkt. Mdegella. Lakini madai yake hayakuasilika na Msaidizi awa Askofu. Kadhalika tulimwuliza kuhusu kujihusisha kwake na mtandao dhalimu? Alijubu kwamba ni kwa sababu ameachishwa masomo na Askofu Dkt. Mdegella. Jibu hilo uwongo mkubwa maana alikwisha jihusisha na mtandao hata kabla ya kuachishwa masomo. Na aliyemwachisha siyo Ask. Dkt. Mdegella bali ni utovu wa nidhamu aliouonyesha kuanzia pale Usharikani Ipogoro ambapo hakuweza kukubaliwa kutokana na sifa za chokochoko alizokuwa akizifanya dhidi watumishi wenzake pale usharikani. Hakuweza kufumbua haya isipokuwa kusema kuwa amekasirishwa na Mdegela kwa kumfukuza masomo kitu ambacho mwenye akili ya kawaida kamwe hawezi kudanganyika kwa kuwa ukweli upo wazi kuanzia kwa wazee wa Kanisa pale Ipogoro kwamba Hopman Kihonza hafai kuwa mchungaji. Lakini pia unaona ufinyu wa mawazo yake na dharau kubwa kwamba eti amefukuzwa na Mdegella. Angalau ungefikiri atambue kuwa amefukuzwa na vikao halali vya Dayosisi na angeheshimu hata kusema amefukuzwa na Askofu kuliko kusema Mdeglla. Lakini pia unashangaa kuona mwanafunzi wa mazoezi ya uchungaji hatambui kuwa yuko chini ya mamalaka na pia hatambui kuwa kuna Halmashauri Kuu. Kama haitoshi, vijana tulichukua hatua ya kuonana na Lambert Mtatifikolo ili tujifunze toka kwake pia. Alitupeleka alipopachagua yeye. Hasty Tasty. Hakuwa na jipya zaidi ya kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Askofu, na kudai kwamba yeye hajawahi pewa kufanya ibada Kanisa Kuu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Tukajiuliza moyoni, hivi anayepanga utaratibu wa ibada Kanisa kuu ni Askofu? Kama haitoshi, alichukua hatua gani kujifunza hilo? Na mwishoni pia tukajiuliza, Je, hiyo ndiyo sababu ya msingi kwake kufanya madhambi yote hayo? Kweli haikutuingia vichwani mwetu. Tulibakiwa na mshangao kwa mtu huyu mwenye shahada ya uzamili jinsi alivyoamua kuwa jinsi alivyo hata sasa! Pasipo ubishi uwao wowote ule, aina hii ya watu ndiyo waliokaribu sana na Mkuu KKKT na baadhi ya Maaskofu.

17. Cha kushangaza sana tarehe 30/05/2012 Halmashauri Kuu iliyokutana Huruma Centre ilisomewa waraka wa Mkuu KKKT wenye maamuzi ya kiimla wa kumtaka Askofu wa Dayosisi ya Iringa kufupisha muda wa uongozi. Maelezo yalikuwa ni kwamba wale wale maaskofu watatu waliliamsha jambo walilosema lisiendelee na kwamba watakaoliendeleza si wana KKKT na siyo wenzetu. Halmashauri Kuu ilitupilia mbali hoja ya waraka huo kwa kuwa hakukuwa na hoja ya msingi kufanya hivyo. Halmashauri Kuu ilipiga kura kwa maamuzi yake mbele ya maaskofu wawili waliotumwa na Kanisa kushiriki Mkutano huo. Maamuzi ya Halmashauri Kuu yamepelekwa sharika zote za DIRA na taasisi zake. Hayo hatuyarudii kuandika maana yako juu ya mamalaka yetu lakini yamesomwa kwenye sharika zote. Sisi tunachojua ni kwamba tunachosema kina nguvu ya Halmashauri Kuu. Tunajua ilisema jambo liliisha tareh 15/1/2012 na kwamba lisiendelee kabisa. Na hapo hatuondoki. Tunajua pia kuwa Halmashauri Kuu ilisema kilichofungwa na Mungu kwa ibada hakitenguliwi na binadamu. Kwahiyo tuna uhakika kwamba kilichofanywa na Baraza la Maaskofu tarehe 15/3/2012 ni uasi kwa Mungu, ni udanganyifu mbele ya Wakristo na ni hila, wivu na chuki binafsi. Na hizo Halmashauri Kuu ilisema zimalizwe na Maaskofu huko kwenye vikao vyao na mambo hayo yasije kwa wakristo wanaotaka kwenda mbinguni. Tunajua halmashauri Kuu ilipiga kura kwamba Askofu Mdgella ataendelea mpaka muda wake wa kustaafu kikatiba utakapofika. Tena tunajua kwamba Halmashauri Kuu iliunda kamati maalumu ya kutaka mwenye malalamiko alete hoja na kwamba iwe mara ya mwisho kuunda kamati za aina hiyo. Mwenyekiti wa kamati ile alikuwa ni Mkuu wa Jimbo na wajumbe walikuwa Wachungaji na Wakristo raia wa kike na wa kiume. Mpaka hapo hakuna aliyejitokeza kuchunguza jambo hilo ili ione kama kuna ukweli kuhusu tuhuma zozote. Hata hivyo, wanamtandao waliazimia kufanya maandamano yaliyozuiliwa na vyombo vya Dola lakini walipeleka taarifa za uwongo kwenye vyombo vya habari kwamba walianza maandamano wakasambaratishwa. Kumbe mchukua picha alichukua maamndamano ya Kanisa la Katholiki ya Uamsho na kudai kuwa ni maamndamano dhidi ya Askofu Dr. Mdegella kitu ambacho ni uwongo mtupu. Katika hatua hizo zote Lambert Mtatifikolo hakutaka kuonyesha ushirikiano. Kamati ya Theolojia na Kamati ya Utendaji walipokaa kutaka kupata mrejeo, Lambert Mtatifikolo alikwepa kwa kisingizio kwamba alikwenda kutibiwa Dar es Salaam.

18. Kutokana na jitihada hizo zote pamoja na vikao vingine vilivyoendelea baadaye inadhihirisha kwamba mtu huyu pamoja na wenzake wameamua kutukana zaidi na zaidi ikiwa ni sambamba na kutaka kuandaa maandamano yaliyotajwa hapo juu ambayo hayakufanikiwa kwa sababu za kiusalama, na hatimaye wakafikia hatua ya kutaka kuzuia ibada kwa njia ya kufunga geti bila mafanikio. Sababu ya kufunga geti la Kanisa kwa mnyororo ilikuwa ni kutaka kupandikiza hasira kwa washarika wanaosali hapa usharikani ili itokee fujo ambapo hatima yake ni kufanikisha mpango wa kutaka kumkataa Askofu Dkt. Mdegella. Lakini hata hivyo, mpango huo ulilaaniwa vikali na washarika waliopata habari hizi kwa kuwa yote haya yanatokana na mtandao dhalimu unaoungwa mkono na baadhi ya viongozi wa KKKT. Jamani angalieni mbinu za shetani zilizo ndani ya watu hawa. Ndiyo maana tunasema hizi ni mbinu za kuzimu. Hata wanasiasa hawafanyi hivi.

19. Kama watafiti na vijana wenye nguvu, tumelichunguza jambo hili kwa ukaribu sana na kugundua kuwa katika chokochoko hizo hakuna maslahi ya kanisa yanayopiganiwa na wale waliofunga geti, isipokuwa ni chuki binafsi kwa tamaa zao za kishetani. Kwa sababu hiyo basi, sisi kama vijana wenye nguvu za kumshinda shetani na watu wake walio katika mwili; sisi tutapambana kiroho, kiakili na hata ikibidi kimwili. Kiroho tutaomba na tunatoa wito kwa Wakristo wote na watu wote wenye mapenzi mema na Dayosisi yetu kuomba. Kiakili tutaweka watu wakutafiti kila mbinu za kila mtu na kila eneo ambalo tunaowahisi kuwa wako washiriki wa jambo hili katika nchi nzima na hasa Dar-Es-Salaam. Kimwili tutakuwa macho kudhibiti wahusika wa chokochoko na uzushi huo ambao unalengo la kutaka kulichafua kanisa letu na kutugawa kiukanda na hatimaye kuleta mafarakano ambayo hayataishia tu makanisani bali hata katika maeneo yetu tunayoishi. Tupo tayari kudhibiti haya yote ndani ya Dayosisi yetu na kwamba, hatutamuacha adui aendelee kufanya maovu hayo hata kama yupo nje ya Dayosisi.

20. Pia tupo tayari kupambana na aina yoyote ile ya kibaguzi inayofanywa na waliotamani Uchungaji na Uaskofu kwa maslahi yao binafsi. Kwakuwa Kanisa la Mungu linatakiwa kuwakusanya watu wote bila kujali dini, rangi, kabila, ukanda wala tofauti za namna iwayo yoyote ile. Hatutaacha jiwe juu ya jiwe kwa kumwonea haya mtu yeyote anayeendelea kujificha na kulichafua Kanisa la Mungu hata kama jiwe hilo limefunikwa na kofia ya kimamlaka. Maadam amethibitika kuharibu utaratibu wa Kikristo na Kisheria, ni lazima mtu huyo ashughulikiwe.

21. Tunauchungu kwa sababu Kanisa la Mungu lilitumwa kwa ajili ya kuwaita watu wote “Mataifa yote” na kuwaleta kwa Kristo. Yesu Kristo alisema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi……” (Mathayo 28:19) Inatia shaka juu wito na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa Kanisa kwa kutotafakari hili maana yanayofanyika hayalengi kuwakusanya watu kama Kanisa la Kristo, bali kutaka kulisambaratisha kwa chokochoko zao za kizushi ili kulinda vyeo au kupandia ngazi za madaraka. Yeyote anayeligawa na kulichafua kanisa la Kristo bila shaka hata kosa hukumu ya Mungu kama ambavyo tumeonyesha hapo awali. Tupo tayari hata kama ni mahakamani maana ushahidi tulionao unajitosheleza kupambana vyema, kamwe hatutasinzia tena.

D: MAAZIMIO YA VIJANA WA KANISA

22. Afrika kusini ilipokuwa ikipigania uhuru wake, wazee na wanasiasa wengi waliwekwa ndani (gerezani) kwa lengo kuzimisha jitihada za mapambano dhidi ya wakoloni katika nchi yao. Lakini wazee wachache waliobakia waliweza kuwatumia vijana wao walioko mashuleni na hata mitaani kuendeleza michakato kama kielelezo cha kutokukubali kuzimisha moto wa mapambano dhidi ya mkoloni. Kadiri vijana walivyodhibitiwa na serikali ya kikoloni yenye itelijensia ya hali ya juu, katili na kali sana, ndivyo ambavyo mapambano yalivyopamba moto zaidi na zaidi. Hatima ya jitihada hizo ilipelekea kufanikisha uhuru wa nchi hiyo mwaka 1994 (kielelezo kizuri kinatolewa kupitia mkanda wa SARAFINA kwa wanaoufahamu na vyanzo vingine pia). Hakuna mtu wa kutuzuia maadam hatuvunji sheria, ila kuisimamia. Kwa hiyo sisi si watu wa kudharauliwa na kuchezewa, bali ni watumishi wa Kanisa sawasawa na mwingine yeyote yule na tunataka kanisa liwe nguzo ya mwelekeo wa maisha yetu katika Taifa letu.

23. Daudi kama kijana aliyedharauliwa na ndugu zake na baba yake na hata mfalme Sauli kwamba asingemuua Goliati. Sisi tunajipa moyo kama Daudi kwamba licha ya kudharauliwa aliweza kufanya yaliyo makubwa kuliko mfalme na jeshi lake katika umri wake huo huo wa ujana na sisi tunamwomba Mungu usiku na mchana tufikie azma hiyo. Tutaliadhibu jeshi la Wafilisti waliolitukana taifa (Kanisa) na Mungu (1Samweli 17:20-58). Ushindi huo upo mbele za Mungu hata kama tutadharauliwa machoni pa wanadamu,

Kutokana na hayo yote, kama vijana tumeazimia yafuatayo:

(i) Kutojihusisha na mambo hayo ya laana kwa sababu yapo kinyume na mpango wa Mungu kwa Kanisa na hata Kisheria;

(ii) Kuyadharau mambo hayo na kuwaelimisha watu wa Dayosisi yote kwamba watu wanaofanya hayo ni watu wale walioshindikana na ni wa ukoo ule wa Yuda Iskariote;

(iii) Kuwatia moyo Wakristo wa sharika zote na hata wengineo ambao wamesikitishwa kutokana na chokochoko na uchafuzi ulifanywa kwa Kanisa na uongozi wake, na kushuhudia kuwa ’Kamwe Mungu hatamwachia shetani ajifiche Kanisani hata aweze kuharibu kanisa lake’;

(iv) Kwamba vijana wote tunaungana kwa pamoja kuzuia mipango yote yenye kuleta machafuko ndani na nje ya Kanisa. Kwa mfano maandamano yenye nia ya kuleta fujo, na vurugu ndani ya Kanisa letu na migawanyiko kwa itikadi za namna iwayo yoyote ile;

(v) Kuwa tayari kuitikia wito wa dharula kukabiliana jambo lolote lililo baya linaloweza kujitokeza katika Kanisa letu;

(vi) Kupeana taarifa juu ya usambazaji wa nyaraka chafuzi ambazo huwa zinafanywa na mtandao huo dhalimu kwa lengo la kulivuruga Kanisa letu, jamii ya watu wa Iringa na Taifa kwa ujumla;

(vii) Kuomba bila kuchoka tukikemea roho mchafu mwenye lengo la kulivuruga kanisa letu.

(viii) Kufanya utafiti kila mahali ndani na nje ya Dayosisi kuwabaini wachafuzi ambao wasipoonekana kwa macho ya mwilini wataonekana kwa macho ya rohoni.

E: HITIMISHO:

24. Tungependa kukiri wazi kwamba, si kwamba tumedharau vyombo halali vilivyoundwa Kidayosisi kushughulikia jambo hili ili kufikia mwisho, bali tunavitia nguvu. Hii ni kwa sababu tumechoshwa na chokochoko za watu hao ambazo zinaendelea kusambaza sumu ya chuki, fitina, na magomvi ambayo yameendelea kuwepo ndani ya Kanisa na hata kutishia usalama kwa baadhi ya familia za watumishi, tukiwemo sisi vijana, Usharika wetu, Dayosisi, Chuo chetu, hata Taifa kwa ujumla.

Kama Wakristo tunajua na ni hakika tunazohaki za Kibiblia na Kisheria za kulinda na kutetea Usharika wetu, Dayosisi na Kanisa letu kadhalika kulinda heshima na amani ya jamii ya Taifa letu. Tunashanga kama Wakristo vijana kwamba anayevunja haki hizi ni Wachungaji wakiamini kabisa kwamba watatetewa na baadhi ya Maaskofu. Wanasemaje juu ya Neno hili Ezekieli 3:17?

25. Hivi tueleweje? Mkuu KKKT aliyekuwa akiwakumbatia hawa watu wa ajabu anajiweka wapi katika sakata hili. Tukimtafsiri kwamba anafanya kazi kinyume na tarartibu za kimaongozi ya Kikristo zilizowekwa na kanisa tutakuwa tumekosea? Tunasita kusema mengi lakini tunaamini wapo Maaskofu wenye hekima. Tunashauri kuwa Maaskofu waone kuwa ni lazima kukemea hila zinazofanywa kwa wazi na Kiongozi yeyote yule hata kama ni wa ngazi ya juu.

26. Sisi huwa hatuendi Kanisani kusoma Katiba ya DIRA au ya KKKT bali huwa tunaenda kusali, kumwabudu Mungu na kumsifu. Tunapofungiwa Kanisa na mtu ambaye amekuwa Karibu na Mkuu KKKT tunaumia sana. Ifahamike kwamba wenye kufunga Kanisa walikuwa watu sita wasioabudu nasi ila waliamini kuwa watalindwa na Baraza la Maaskofu. Kwahiyo kwa mawazo yao, Wakristo wote zaidi ya 4,500 wanaoabudu hapo walikuwa hawana umuhimu ila hao watu sita na waliowatuma takriban watu kumi (10) walionyuma ya kundi hilo. Huu ni ukiukwaji wa sheria ya nchi ya haki ya kuabudu.

27. Kama vijana wa Kanisa Kuu tunaapa kuwa hatupo tayari mambo haya yanaendelea hivi. Na tutashawishi vijana wengine nje ya Dayosisi ili kuhakikisha kuwa heshima ya Kanisa letu inalindwa kuanzia Sharikani mwao. Ni heri kufa katika Kristo maaana kuna fahari (Zaburi 116:15) kuliko kuishi kama wanafiki, wenye hila, wenye njama, wenye wivu, waoga na waongo. Tena hatuko tayari kwa gharama zozote zile kufanya urafiki na shetani kama wale walio katika mtandao huo mchafu. Sasa tumefikia mwisho wa kuona hili jambo linaachiliwa na kuendelea kuliumiza kanisa la Kristo, raslimali zake na azma ya kuhubiri Injili.

28. Kwa kuwa hatima ya kanisa imo mikononi mwa Yesu Kristo na wanakanisa wake, sisi vijana kama wanakanisa, kwa waraka huu tunawaambia washarika wote katka ngazi za mitaa, Sharika, Majimbo, Dayosisi na KKKT kwa ujumla na Watanzania wote wanaosoma habari za Iringa na Askofu wake kwenye magazeti; kama tulivyowaambia wale maaskofu watatu Ask. Dkt. Hans Mwakabana, Askofu Dkt. Martin Shao na Askofu Elisa Buberwa kuwa

(i) Tumechoka. Hatutaki kuona wala kusoma matusi na masingizio mahali popote.

(ii) Hatuko tayari kusikia wala kuambiwa jambo lolote kuhusu Askofu Dkt. Owdenburg Moses Mdegella lenye mwelekeo wa fujo na ghasia zozote kwenye mitaa na sharika zetu. Na tukisikia hatutanyamaza.

(iii) Hatutaki kikao wala mazungumzo. Hatutafumbia macho jambo lolote na tunashughulikia kila ukaidi dhidi ya Halmashauri Kuu kwa ukamilifu bila kufumbia macho tukio lolote wala kumwonea haya mtu yeyote.

(iv) Tunasimama kidete katika kulilinda na kulitetea Kanisa la Kristo na Dayosisi yetu dhidi ya maadui wote wanaoturudisha nyuma kiroho na kimwili.

(v) Tunaona wazi kuwa huu ni mkakati wa Mkuu KKKT na ukanda wa Kaskazini kuturudisha nyuma.

(vi) Hatuko tayari kuingia hatiani na kwenye laana kwa kumwachia Shetani Kanisa la Mungu katika Yesu Kristo kwa ulaghai wa Maaskofu waliotangaza kanisani, kwa toba madhabahuni kuwa yameisha halafu wakaenda kuanza jambo baya zaidi kwa njia ya Baraza la Maaskofu.

29. Kwa wanaofanya maovu ya namna hiyo ujanja wao ni sawa jogoo kukificha kichwa chake akidhani kuwa ameuficha mwili mzima lakini kumbe anaonekana. Ni jambo la kuaminika kwamba kamwe Mungu hatamwachia Shetani aendelee kujificha hivyo hata aweze kuliharibu Kanisa lake. Ni lazima atakamatwana tu na kupata adhabu sitahiki kwa mabaya yake anayoyatenda kwa Kanisa la Kristo.

30. Tunahitimisha kwa kusema kuwa, hali tunajua kuwa vipo vikao vya kidhalimu vinavyoendelea hata sasa, ni hakika kwamba hatutatikisika wala kusita katika hili. Tuko tayari kutetea Kanisa letu na Dayosisi yetu na viongozi wake na wachungaji wetu pia wanapotendewa ubaya kama huu tuliouona. Maadui wa Kanisa hususan Dayosisi yetu tumekwisha watambua na tutakabiliana nao vyema.

Pia tunamtia moyo Askofu wetu kwa kumuomba ajisomee mwenyewe Neno la Mungu kutoka Zaburi Zaburi 119:23-24. lakini kwafaida ya wengine Neno hili linasema: ”Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako. Shuhuda zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu”.

Kwa niaba ya vijana Usharika wa Kanisa Kuu, ni sisi tuliotumwa na Bwana Kushiriki kazi ya Bwana ikiwa ni pamoja na ’Kulia Pamoja na Waliao’

...............................................................................

Disma Mwagamge – M/Kiti Idara ya V/E/K Usharika wa Kanisa Kuu

...........................................................................

Mchg. Joshua Chussy – Mratibu wa Tamko kwa niaba ya Katibu wa Idara ya V/E/K Usharika wa Kanisa Kuu

NAKALA:

Mkuu - KKKT

Katibu Mkuu KKKT

Askofu – KKKT Dayosisi ya Iringa

Msaidizi wa Askofu – KKKT Dayosisi ya Iringa

Katibu Mkuu KKKT – Dayosisi ya Iringa

Mkuu wa Jimbo la Magharibi – KKKT Dayosisi ya Iringa

Katibu wa Idara V/E/K – Dayosisi ya Iringa

Kasisi – KKKT Usharika wa Kanisa Kuu Dayosisi ya Iringa

Wachungaji wa Sharika – KKKT Dayosisi ya Iringa.

KUPATA HABARI MPYA BOFYA HAPA

Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA