Home » » HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA MAPAT

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA MAPAT

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Tuesday, June 19, 2012 | 12:03 AM______________________

I. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha.

Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa sana na juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu ni kuvumilia mpaka uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili kuweka Serikali itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili changamoto za sasa na za baadaye.

Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.

  1. UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA

Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa namna gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika kufanya hivyo, tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya Upinzani tunaona kuwa hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.

Kupunguza Makali ya Maisha

Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula kwa Wakala wa Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi bilioni 27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko.

Mheshimiwa Spika, licha ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka 2011/12 iliitaka Serikali kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa nchini ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya kapu la bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25 mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza hatua zilezile ilizofanya mwaka wa fedha unaokwisha kwa kutoa vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza Mchele na Sukari. Katika hotuba yake Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9 ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya Sukari ilipanda kutoka tshs 1700 mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini. Waziri wa Fedha katika hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za haraka ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari na mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo lile lile ikitegemea matokeo tofauti.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea pendekezo lake la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa wingi. Miongoni mwa vivutio hivyo ni:

i. Kuwekeza kwenye barabara za vijijini ili mazao yao yafike kwenye masoko na kupata bei nzuri,

ii. Kuwekeza kwenye Usambazaji wa Maji vijijini ili kina mama wasitembee mwendo mrefu kutafuta maji na hivyo kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji,

iii. Kuwekeza kwenye Umeme vijijini ili wafanyabiashara wa vijijini waongeze thamani ya mazao. Kwa mfano, kuuza Unga badala ya Mahindi.

iv. Kuwekeza kwenye miundombinu ya Umwagiliaji vijijini ili wakulima wazalishe muda wote wa mwaka.

v. Kuwekeza kwenye Elimu vijijini na pia Afya vijijini ili wananchi wetu wawe na Afya bora na waelimike katika mbinu za uzalishaji bora.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa, hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa Manamba na vibarua ndani ya nchi yao. Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa Bei ya chakula utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa Kilimo.

Mhesimiwa Spika, Tunatambua kuwa hatua tunazotaka Serikali ifanye ni za muda wa kati. Kwa muda mfupi tunataka Bodi ya Mazao mchanganyiko, Wakala wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Sukari zipewe fedha kuagiza Mchele na Sukari na pia kununua kutoka kwa wakulima na kusagisha Mahindi. Wafanyabiashara waagizaji wa Chakula washindane na Taasisi hizi za Umma badala ya kuwapa vibali ambavyo hutolewa kwa rushwa na hivyo kuongeza bei za bidhaa hizo.

Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira.

Mheshimiwa Spika, Serikali imesema kwamba ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo la Ajira kwa kuongeza fursa za ajira. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp. Pia Serikali imetangaza kwamba imeajiri walimu, maafisa ugani na watumishi wa Afya. Hatua kama hizi pia zimetangazwa kwa mwaka wa Fedha wa 2012/13 ambapo pia Serikali imetangaza kuajiri watumishi 71,756.

Mheshimiwa Spika, Duniani kote Serikali haizalishi ajira bali ajira huzalishwa na Uchumi mzima ambapo Serikali ni sehemu tu ya Uchumi (Jobs are created by the economy). Takwimu zinaonyesha kwamba kila mwaka Tanzania inaingiza kwenye soko la Ajira watu takribani laki saba. Shughuli za Uchumi zikiongezeka ndio Ajira zinatengenezwa. Serikali inafikiria nini kuhusu vijana takribani milioni nane walio shule za Msingi hivi sasa, Vijana milioni 1.7 walio katika Shule za Sekondari hivi sasa, Vijana 200,000 waliopo vyuo vya Ufundi na Wanachuo 180,000 walio katika Vyuo vya Elimu ya Juu (takwimu kutoka kitabu cha hali ya uchumi, 2012 sura ya 19). Serikali ambayo bado inategemea takwimu za Ajira za Mwaka 2006 inajitamba kwa kuajiri watu 70,000.

Mheshimiwa Spika, Jukumu la Serikali ni kujenga mazingira ya wananchi kupata ajira ama kwa kujiajiri au kwa kuajiriwa na shughuli za uchumi. Lakini ukweli ni kwamba Serikali imeshindwa kushughulikia tatizo la Ajira na hasa ajira kwa vijana. Tatizo la Ajira kwa Vijana ni Bomu litakalokuja kutulipukia vibaya sana kama hatutakuwa makini nalo. Hii ni nchi ya Vijana. Kutoshughulikia masuala yao ni kutoshughulikia masuala ya nchi.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya ajira kwa vijana Bajeti mbadala imeiwekea mikakati mipana ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi mikubwa ya Umma itakayomeza vijana waliopo mtaani na kuanzisha kwa makusudi na kwa kasi Vyuo vya Ufundi stadi na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo vingi. Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Uwekezaji wa Miundombinu Vijijini kama njia ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Vilevile tunapendekeza Miradi mikubwa ya kuongeza mazao ya Kilimo hasa Pamba, Korosho na Katani ili kupanua Ajira. Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kujenga VETA katika kila Halmashauri ya Wilaya na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa ili kutoa ujuzi kwa vijana ili waweze kukabili maisha yao. Badala ya Serikali kukopa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida, Serikali ikope kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi na vyuo vya Ufundi na Mafunzo. Ni Lazima viongozi sio tu tuwe makini bali tuonekane kuwa makini tunaposhughulikia suala la Ajira kwa Vijana.

Sera ya Mapato

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilitangaza vipaumbele katika sera ya Mapato ambavyo ni pamoja na kukusanya Mapato ya Serikali mpaka zaidi ya asilimia 20 ya Pato la Taifa ili kuwezesha kujitegemea kupata fedha za miradi ya maendeleo. Pia Kambi ya Upinzani inakusudia kufanya marekebisho mbalimbali ya sheria za kodi ili kulinda viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za kilimo na mifugo za hapa nchini, kupanua wigo wa Mapato kwa kutunga sheria ya kulazimu kila Mtanzania kujaza fomu za marejesho ya kodi na kurekebisha viwango vya kodi ya Mapato (PAYE). Vile vile tunapendekeza kufanya marekebisho ya sheria za kodi kwenye sekta za madini na mawasiliano ili kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2011/12 Serikali ilichukua hatua mbalimbali katika masuala ya Kodi. Katika Bajeti mbadala pia tulipendekeza hatua mbali mbali ambazo tuliona zitaongeza mapato ya Serikali na hivyo kutuwezesha kuendeleza nchi yetu. Baadhi ya hatua mbalimbali tulizopendekeza Serikali imetangaza kuzitekeleza.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika Bajeti Mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza masuala yafutayo ili kuongeza mapato ya Serikali.

  1. Hatua zifuatazo zilipendekezwa ili kuweza kukabiliana na ukwepaji wa kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa (Multinational Corporations) na hatimaye kulipunguzia taifa mapato:

(i) Kutunga sheria kwa kuimarisha zaidi sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwamba, mikopo ya makampuni kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi, isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja bila kujali mikataba iliyopo.

(ii) Kutunga sheria kuhakikisha kwamba riba kwenye mikopo kutoka Makampuni yanayohusiana (sister companies) haitaondolewa kwenye kutoza kodi (not tax deductible).

(iii) Kuhakikisha kwamba mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania yanatozwa kodi ya asilimia 30% kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital gains’).

Mheshimiwa Spika, katika mapendezo haya ni pendekezo moja tu ndilo limechukuliwa na Serikali katika Bajeti ya mwaka 2012/13 nalo ni pendekezo la ‘capital gains tax’. Hata hivyo Pendekezo la Serikali lina makosa makubwa sana ya kifundi. Waziri wa Fedha Mhe. Mgimwa amesema, ninanukuu ‘Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa rasilimali ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa HISA za kampuni mama ya nje ya nchi’

Mheshimiwa Spika, Ukisoma pendekezo letu kwa haraka utaona kama Serikali imelichukua lilivyo, lakini kwa jicho la kiuchumi pendekezo la Serikali na lile la Kambi ya Upinzani ni mambo tofauti sana. Pendekezo la Serikali linazungumzia HISA. Mamlaka ya Mapato Tanzania haitakuwa na mamlaka (jurisdiction to tax) kutoza kodi kwa Kampuni mama (as a source or even residence). Mamlaka ya Mapato Tanzania ina mamlaka na Mali (assets) zilizopo Tanzania za Kampuni mama. Kwa mfano, wakati kampuni ya Barrick inanunua mgodi wa Bulyanhulu haikuinunua Kampuni ya Kahama mining ltd bali ilinunua hisa zote za Kampuni ya Sutton Resources. Vile vile, wakati Zain inanunua Celtel, haikununua Celtel Tanzania ltd bali Celtel Africa BV ambayo ilikuwa inamiliki Celtel Tanzania BV ambayo ilimiliki Celtel Tanzania ltd. Hivyo hivyo ilikuwa kwa AirTel ilipoinunua Zain. Kukwepa mitego hii ya Mashirika ya Kimataifa (MNCs) sheria itaje kwamba Kodi hii itozwe kwa Mali zilizopo Tanzania na sio kwa HISA kama alivyopendekeza Waziri wa Fedha. Hata hivyo Kambi ya Upinzani inatambua hatua hiyo ya Serikali kuchukua wazo hili ili kuongeza Mapato ya nchi.

Misamaha ya Kodi

Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza misamaha ya Kodi mpaka kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii haikutekelezwa na Serikali na badala yake imerejea kuahidi tena. Waziri wa Fedha ameliambia Bunge katika hotuba yake, nanukuu ‘kuendelea kufanya mapitio ya sharia mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo’ (uk.39). Badala ya Serikali kutuambia hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia ngapi, imeendelea kutoa ahadi isizoweza kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Jopo la Taasisi za dini hapa nchini waliyoiita ‘The One Billion Dollar Question’ imeonekana kwamba Tanzania inapoteza takribani shilingi trilioni 1.7 kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi, utoroshaji wa mitaji nje na udanganyifu katika biashara ya kimataifa. Fedha hizi ni zaidi ya jumla ya Bajeti za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Nishati na Madini. Fedha hizi ni zaidi ya Mkopo ambao Serikali itadhamini kwa TPDC ili kujenga Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Fedha hizi zinazopotea kutokana na misamaha ya kodi ni zaidi ya gharama za Ujenzi wa Gati mpya katika Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya Upinzani inawapongeza Viongozi wa Dini kwa kufanya kazi hii nyeti sana lakini tunampongeza zaidi Mtafiti Mtanzania Dokta Prosper Ngowi kwa kushiriki katika utafiti huu. Tunaishauri Serikali kusoma Taarifa hii na kutekeleza mapendekezo yake ili kuongeza mapato ya Serikali. Lugha za kufanya mapitio kila mwaka hazisaidii, wananchi wanataka kuona misamaha ya kodi imepungua mpaka kiwango kinachostahili cha asilimia 1 ya Pato la Taifa.

Kurekebisha mfumo wa Kodi ya Mapato

Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Tunarejea pendekezo letu na kuongeza pia kwamba sehemu ya kodi ya Mapato inayotoa fursa (grandfathering) kwa Kampuni za Madini kutumia sheria ya kodi ya Mapato iliyofutwa ya mwaka 1973, ifutwe. Pendekezo letu lina lengo la kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya ‘100% depreciation’ kwenye Mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa ‘Corporate Tax’.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili kutoza kodi ya Mapato (PAYE) kutoka tshs 135,000 mpaka tshs 170,000 bila kushusha kodi yenyewe. Hii haitamsaidia mwananchi hata kidogo kwani bado kiwango cha kodi cha asilimia 14 kipo juu sana. Vile vile kiwango cha chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri wafanyakazi wa Serikali maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha Mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa Sekta Binafsi ambao wengi hulipwa kiwango kidogo sana cha mishahara. Kimsingi kutokana na tangazo lake, Waziri wa Fedha ametangaza kima kipya cha chini cha mshahara kuwa kitakua tshs 170,000.

Mheshimiwa Spika, tunarejea kauli yetu kwamba kupanda kwa gharama za maisha kumepunguza uwezo wa matumizi ya wananchi walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo inakatwa kodi (PAYE). Tunapendekeza kwamba PAYE ianzie asilimia 9 kutoka asilimia 14 na kiwango cha chini cha kutoza kiwe tshs 150,000. Tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa cha Mapato kwa Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha kinatarajiwa kuingiza takribani shilingi bilioni 1,437 (asilimia 18 ya Mapato yote ya kodi yanayokusanywa na TRA) kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi wa Serikali tshs 115bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma tshs 47bn na Wafanyakazi wa Sekta binafsi tshs 312bn) na Idara ya Walipa kodi wakubwa (Wafanyakazi wa Serikali tshs 450bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma Tshs108bn na Wafanyakazi wa Sekta Binafsi tshs 406bn). Hata hivyo wananchi wanapobakia na pesa za matumizi kodi nyingine kama VAT na Ushuru wa Bidhaa huongezeka na hivyo kupunguza kiwango cha Mapato ya Serikali ambayo yangepotea kutokana na uamuzi huu.

Mheshimiwa Spika, Hata hivyo bado kuna haja ya kuangalia upya ‘tax brackets’ na kuzirahisisha kwa kuzipunguza na kuongeza kiwango cha kodi ya Mapato kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza mapato kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa kambi ya Upinzani inapendekeza mabadiliko katika viwango vya juu vya kodi ya Mapato ambapo tunapendekeza kupandisha kiwango cha juu kabisa cha kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe shilingi milioni kumi na kodi iwe asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa.

Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza kwamba mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya shilingi 10,000,000 alipe kodi ya Mapato ya shilingi 500,000 kujumlisha na asilimia 42 ya tofauti ya shilingi 10,000,000 na shilingi 3,200,000 kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini. Lengo la mapendekezo haya ni kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi zaidi kulingana na kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi nyingi zaidi kuliko wenye nacho.

Mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi

Kodi (PAYE)

Mapendekezo ya mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi

Kiwango kipya cha Kodi (PAYE)

Mapato yanayozidi shilingi 720,000

Sh. 112,500 ongeza 30% ya kiasi kinachozidi sh. 720,000

Mapato yanayozidi 720,000 lakini hayazidi sh. 3,199,199

Sh.112,500 ongeza 30% ya ziada ya sh. 720,000

Mapato yanayozidi sh. 3,200,000 lakini hayazidi sh.9,999,999

Sh.190,000 ongeza 38% ya ziada ya 3,200,000.

Mapato kuanzia sh. 10,000,000 na kuendelea

Sh. 500,000 ongeza 42% ya mapato yake.

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya hayatapunguza Mapato ya Serikali kwani wigo wa kodi utakuwa umeongezeka kwa kuwagusa wafanyakazi katika sekta binafsi na pia kupata kodi zaidi kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi ya Upinzani inaendelea kupendekeza kuwa mchakato uanze ili kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi awe anajaza fomu za kodi (tax returns) kila mwaka. Suala hili ni muhimu sana na litangazwe mwaka huu ili tuwe na mwaka mzima wa kujitayarisha ili lianze Mwezi Julai mwaka 2013. Mtanzania yeyote, awe na kipato au asiwe na kipato ajaze Tax Returns. Mfumo huu utatoa takwimu muhimu sana kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na utasaidia sana hapo baadaye kupanua wigo wa Mapato. Tunapendekeza marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato ili mfumo huu uwepo kisheria ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.

Mheshimiwa Spika, Vile vile, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Real Estate Regulatory Authority kama tulivyofanya kwa mwaka uliopita na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili. Lengo ni kuhakikisha Sekta ya Nyumba inatoa mapato ya kutosha kwa Serikali na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi inayofanywa na wenye nyumba.

Presumptive Tax

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza mwaka 2011/12 kwamba ushauri wa Mradi wa kuboresha mfumo wa kodi (Tax Modernisation Project) ambao ulishauri kwamba ipo haja ya kuainisha Kodi ya VAT na Presumptive Tax, utekelezwe. Tunashauri kuwa kodi anayotozwa mfanyabiashara ndogondogo kabla hajaanza kufanya biashara ifutwe kabisa. Uamuzi huu utapunguza mapato ya Serikali (Shilingi bilioni 21.6 kwa mujibu wa Kitabu cha Bajeti Vol. I) katika kipindi cha muda mfupi lakini itakuwa ni chanzo kikubwa sana cha mapato katika kipindi cha muda mrefu.

Vyanzo vipya vya Mapato

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kupitia vyanzo vya mwaka jana na kulinganisha na mapendekezo ya Serikali, Kambi ya Upinzani bado inapendekeza vyanzo vya ziada mwaka huu ili kuboresha Mapato ya Serikali.

Kupanua wigo wa Skills Development levy

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunapenda kushukuru kuwa wazo letu la kutoza kodi ya skills development levy tuliyopendekeza katika hotuba yetu ya mwaka uliopita lilifanyiwa kazi na serikali lakini kwa mwaka ujao wa fedha tunaitaka serikali kuipitia upya kodi kwa kuongeza wigo wa wachangiaji ili kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kiwango cha tozo ya kuendeleza stadi (skills development levy – SDL) kishuke kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka asilimia 4. Tunapendekeza kuwa Waajiri wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Lengo ni kupunguza mzigo kwa Waajiri na kuondoa ubaguzi kwani wanaofaidika na tozo hii (wanafunzi wa elimu ya Juu) pia huajiriwa na Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali ilipanga kukusanya tshs 161bn kutoka katika tozo hii kwa mfumo wa sasa.

Mheshimiwa Spika, Marekebisho ambayo Kambi ya Upinzani inayapendekeza yataongeza mapato ya Serikali mpaka tshs 320bn.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha katika tozo hii amesema Serikali ‘itapitia upya maudhui ya viwango vya tozo’ hii. Kambi ya Upinzani imetamka maudhui na viwango na tunaiomba Serikali itekeleze pendekezo hili.

Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza mgawanyo wa tozo hii urekebishwe kwa kuongeza mapato yatakayokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi mchundo.

Mheshimiwa Spika, kama wanafunzi wetu watasomeshwa na kodi hii basi tuangalie upya mfumo wa Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Fedha inayopatikana kwenye Kodi hii itumike kusomesha kwa ‘grant’ wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi darasani na kuwapunguzia mzigo wa mikopo. Vile vile tuangalie kama tunaweza kukopesha wanafunzi malazi na chakula tu na kutoa bure ada na mafunzo kwa vitendo pamoja na vitabu.

Kulinda kazi za Wasanii

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani mara kwa mara tumekuwa tukieleza jinsi wasanii wanavyoshindwa kunufaika na kazi zao kutokana na kukosekana mfumo rasmi wa kiserikali unaozuia wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na serikali kukubali kuahidi kuwa na mfumo rasmi wa kuzuia wizi wa kazi hizo, serikali haijaweka wazi mfumo rasmi utakaokuwa unatumika kuzuia wizi huo na hatimaye wasanii kunufaika na kazi zao.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani katika hotuba ya Wizara ya Habari Vijana na Michezo kwa mwaka uliopita tulingumzia suala hili na tulishauri kwamba kuwe na utaratibu wa kuweka sticker maalumu zinazotolewa na mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi za wasanii. Serikali imetekeleza pendekezo letu. Hata hivyo tuna maoni tofauti kuhusu namna ya kutekeleza pendekezo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, serikali mwaka 2006 kupitia gazeti la Serikali Na. 18 la tarehe 10 Mwezi wa Februari, ilianzisha utaratibu wa HAKIGRAM kama stiker maalumu za kazi halali za wasanii zinazotolewa na COSOTA. Kambi ya Upinzani tunapendekeza utaratibu huo uendelee na Mamlaka ya Mapato TRA ihusike kukusanya mapato kwa ajili ya kazi hiyo na COSOTA wataratibu utoaji wa HAKIGRAM. Hii itaenda sambasamba na kuzuia uchakachuaji wa HAKIGRAM hizo ili kutopoteza lengo la kuweka mfumo huo. Stiker zisitolewe na TRA bali zitolewe na COSOTA na TRA isimamie eneo la Mapato tu. Hii itasaidia kwani stiker hizi hazitatumika kupata mapato peke yake bali pia kuweka kumbukumbu muhimu za kazi za wasanii.

Mapato kutoka Sekta ndogo ya Mawasiliano ya Simu

Mheshimiwa Spika, serikali imekuja na pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa bidhaa kwenye masuala ya huduma ya mawasiliano ya simu, jambo ambalo litamgusa mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni mwananchi wa kawaida na hivyo kuongeza gharama za simu. Kambi ya Upinzani inapinga kabisa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa Maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi.

Mheshimiwa Spika, Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi kodi ya kutosha na hasa kodi ya Makampuni (corporate tax). Waziri Mkuu alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza Kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Katika orodha hiyo kulikuwa na Kampuni moja tu ya Simu za Mkononi (Kampuni ya AirTel).

Mheshimiwa Spika, wakati wananchi wanataka kodi zaidi kutoka Kampuni za simu, Serikali inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu. Kampuni zilipe kodi ya Mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa bidhaa ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora.

Mheshimiwa Spika, vilevile wananchi wanalalamika kwamba Kampuni za simu za Mkononi hajiweki wazi mapato yake yote hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya POAC kuiagiza TCRA kufunga mtambo utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote ambayo kampuni za Simu zinapata. Serikali ya Ghana ilifanya hivi na kupandisha maradufu mapato yanayotokana na sekta ndogo ya simu. Hivi sasa Ghana, nchi yenye watumiaji wa simu milioni 17 ukilinganisha na Tanzania yenye watumiaji 23 milioni, inakusanya asilimia 10 ya Mapato ya Serikali kutoka kwenye kampuni za Simu peke yake. Iwapo Tanzania ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya Mapato ya ndani ya Serikali kutoka kwenye kampuni za simu, Tanzania itaweza kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke yake. Hata hivyo mazingira ya Ghana na Tanzania ni tofauti na hivyo tunapendekeza kiwango kutokana na hali yetu.

Mheshimiwa Spika, Shirika la TCRA kupitia zabuni nambari AE-020/2010-11/C/04 imetangaza ‘request for expression of interest for design, development, installation and Management of Telecommunication monitoring system under build, operate and transfer’ ili kupata chombo cha kufuatilia Mapato ya Kampuni za Simu. Kwa mujibu wa ratiba zilizotangazwa na TCRA chombo kitakuwa kimeanza kazi mwishoni mwaka huu wa 2012. Kwa dhati kabisa napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA na watumishi wote kwa kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Bunge kwa haraka ili kuhakikisha mapato kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kilichotushangaza ni kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi hakugusia kabisa suala hili muhimu sana kwa mapato ya Serikali badala yake Serikali imekimbilia kukandamiza wanyonge watumiaji wa Simu na kuyaacha Makampuni ya Simu yakilipa kiduchu kutoka kwenye mapato yao.

Mheshimiwa Spika, uamuzi huu wa kufuatilia mapato ya Kampuni za Simu na Marekebisho tunayopendekeza ya kujenga uwezo zaidi wa TCRA kwa kuwa na Idara ya ‘Revenue Assurance’ na kurekebisha sheria ya TCRA kwa kuweka wazi makujumu ya TRA ndani ya TCRA, utaiingizia Serikali mapato ya takribani tshs 660bn.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la Sekta ya Mawasiliano ninaomba kurejea kuitaka Wizara ya Fedha itoe maelezo hapa Bungeni namna ambavyo Hisa za serikali katika Kampuni ya MIC Tanzania ltd inayomiliki Kampuni ya Tigo zilivyouzwa. Mheshimiwa Spika Serikali ilikuwa inamiliki hisa asilimia 26 katika Kampuni hii. Kwa mujibu wa kumbukumbu nilizoziona Hisa hizi zote ziliuzwa kwa thamani ya dola laki saba kwa mwana hisa mwenza mnamo mwezi Februari mwaka 2004. Kampuni hii leo inapata mapato ya Tshs bilioni 20 kwa mwezi, tuliuza hisa zetu asilimia 26 kwa dola laki saba! Laki Saba dola! Kambi ya Upinzani inataka uchunguzi maalumu katika mauzo haya na Taifa liambiwe nini kilitokea na hatua gani za kuchukua dhidi ya waliouza mali hii ya Umma bila zabuni wala kuzingatia thamani ya fedha.

Kuzuia mauzo ya ngozi ghafi nje ya nchi

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imeshangazwa na hatua ya serikali kuja na pendekezo la kuongeza ushuru kwenye bidhaa ya ngozi ghafi inayosafirishwa nje kutoka asilimia 40 hadi 90 lengo likiwa ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hiyo na kuiongezea thamani.

Mheshimiwa Spika, kwa nchi iliyo na mianya mingi ya rushwa kama Tanzania hatua hii haitakuwa na tija kwa kuwa wafanyabiashara wengi wa ngozi ghafi wamekuwa na tabia ya kupunguza takwimu za kusafirisha ngozi ghafi na hivyo kupelekea serikali kukosa mapato mengi sana. Serikali inafahamu kwamba hata ushuru wa mauzo nje wa asilimia 40 haukuweza kutatua tatizo la viwanda vya ndani kukosa malighafi. Kambi ya Upinzani haikubaliani na Pendekezo la Serikali kwani halitatatua tatizo la kukuza sekta ndogo ya Ngozi nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kuzuia kabisa kusafirisha ngozi ghafi kwenda nje na badala yake kuwe na mpango wa kutumia ngozi ghafi hapa nchini na kuleta tija katika uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje.

Mheshimiwa Spika, hatua ya kuzuia ngozi ghafi kusafirishwa kwenda nje kwa Tanzania itakuwa sio suala jipya kwa sababu Ethiopia imezuia na kuwekeza katika kiwanda cha viatu, mikanda na bidhaa za ngozi. Kutokana na Mpango wa Mendeleo ya Ethiopia (GTP – Growth and Transformation Plan) sekta ya Ngozi itaingiza fedha za kigeni za thamani ya dola za Kimarekani bilioni 4 kwa mwaka. Hii ni sawa na fedha za kigeni ambazo Tanzania inapata kutoka kwenye Dhahabu na Utalii kwa pamoja. Ethiopia nchi iliyokuwa inatembea na bakuli na kulia njaa leo inakuwa nchi ya kupigiwa mfano na sisi Watanzania! Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pia amepiga marufuku kuuza ngozi ghafi nje. Hata nchi ya Pakistani ambayo ndio ngozi zetu zinakwenda nayo imepiga marufuku mauzo ya ngozi ghafi nje. Serikali ipige marufuku Mauzo ya ngozi ghafi nje ya Nchi ili kulinda viwanda vya ngozi nchini, kuoongeza Ajira na kuongeza mapato ya Fedha za kigeni.

Kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za Maziwa

Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini inahitaji kuwekewa maazingira ya kukua ili izalishe ajira na mapato ya kodi kwa Serikali. Wakati Tanzania ndio nchi ya Afrika Mashariki inayoongoza kwa kuwa na Ng’ombe wengi lakini inaongoza kwa kuagiza maziwa kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani 3.6m. Wakati Kenya imelinda soko la Maziwa na Bidhaa za Maziwa kwa kuondoa (zero rating) kodi ya VAT kwenye bidhaa za Maziwa, Waziri wa Fedha hajaonyesha kabisa juhudi zozote za kujengea uwezo sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini na hivyo kuweza kuondolewa kabisa katika ushindani na kujikuta wafugaji wanakosa kabisa soko la kuuza maziwa yao hapa nchini. Nchi za Rwanda na Uganda pia zimelinda Maziwa na Bidhaa za maziwa kwa njia hii. Ni muhimu Serikali kuwianisha kodi hii na Nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kufanya marekebisho kwenye sharia ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kufanya ‘zero rating’ kwenye Maziwa na Bidhaa za Maziwa zinazozalishwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka 5 ili kufikisha uzalishaji wa angalau lita 500,000 za maziwa kwa siku kutoka lita 123,000 za sasa na kuweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya elfu tatu.

Mheshimiwa Spika, hatua zote za kuongeza mapato tulizopendekeza pamoja na hatua za Bajeti Mbadala iliyopita ambazo tunarudia kuzipendekeza zitaongeza Mapato ya Serikali kwa takribani shilingi bilioni 2,885 kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.

NYONGEZA YA VYANZO VYA MAPATO MBADALA 2012/2013

Chanzo cha Mapato

Makisio - Bilioni

Marekebisho ya kodi za misitu ikiwemo Mkaa

130.8

Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa Biashara ya Nje

742.74

Mauzo ya hisa za serikali

415.55

Marekebisho ya kodi Sekta ya madini (kodi ya Mapato, Kodi ya CGT na ushuru mbalimbali) (25% ya Mauzo ya Madini Nje)

578.36

Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu

502.26

Marekebisho ya Kodi ya SDL

243.52

Mapato ya wanyamapori

61.64

Kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta- kampuni za madini

44.9

Usimamizi wa mapato ya utalii

51.75

Kuimarisha biashara katika EAC kwa kuongeza mauzo

114.15

JUMLA

2,885.67

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo juu, vyanzo hivi vya mapato ni mjumuisho wa vyanzo ambavyo katika hotuba zetu mbadala za nyuma tumekuwa tukipendekeza, ambapo tumevifanyia marekebisho kulingana na hali halisi ya uchumi ulivyo kwa sasa, pamoja na kupendekeza baadhi ya marekebisho ya sheria za kodi ili kuongeza mapato zaidi kwa Serikali.

DENI LA TAIFA

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza madeni kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka 2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion 22.

Mheshimiwa Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13 inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi takribani trillion 5 mwaka 2012/13. Serikali ikubali kutekeleza mapendekezo ya Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupanua wigo wa kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na kuepuka matumizi mabaya ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa ili kuweza kubaini ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali inachukua kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au Bunge litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali haipaswi kuvuka. Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni kuliweka Taifa rehani na kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na pia wakope maisha ya watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, Ukiangali sura ya Bajeti ya Serikali, inaonyesha kuwa Serikali itakopa fedha zenye masharti ya kibiashara ndani na nje yenye thamani ya Tshs. Trilioni 2.89 kwa kipindi hiki cha 2012/13. Athari ya mikopo ya kibiashara ya ndani ni kubwa sana kwa watanzania, kwanza inawafanya wananchi hasa wajasiriamali wanaokopa kushindana na Serikali yao, kwani mabenki yatashindwa kuwakopesha wafanyabiashara au wakikopa watakopa kwa masharti magumu na hasa riba kuwa kubwa. Jambo hili linapunguza uwezo wa wazalishaji kuongeza uzalishaji hasa viwandani kwa kukosa mikopo ya uendeshaji. Kama tulivyoshauri hapo juu, Serikali ijiepushe na mikopo ya masharti ya kibiashara kwa kuongeza makusanyo ya kodi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Serikali kuwa imepata Mshauri Mwelekezi atakayeishauri katika kujiandaa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni. Serikali ilieleze Bunge ni lini na kwa namna gani zabuni ya kumpata mshauri huyu ilitangazwa na kama Sheria ya Manunuzi ilifuatwa.

Mwenendo wa Matumizi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15 trilioni(USD 8.75 Billion) katika mwaka 2012/13 kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi wiki iliyopita. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha kwamba mafungu ya juu 5 yatakayoongoza kwa matumizi kwenye Bajeti hiyo ni Kama ifuatavyo;

1. Huduma kwa Deni la Taifa Tshs 2.7 trilioni (USD 1.69 Billion)
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge

Mheshimiwa Spika, Jumla ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti yote, kwa hiyo asilimia 40% ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu 5 tu na kati ya hayo Wizara ni nne tu za Ujenzi, Elimu, Ulinzi na Nishati na Madini. Wizara ya Kilimo wala Afya hazimo kabisa katika Wizara 5 zitakazopata fedha nyingi zaidi katika Bajeti. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la Taifa. Pia sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Shilingi bilioni 40 ambazo zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kiwira katika Wizara ya Nishati na Madini ni kwa ajili ya kulipia Madeni ya Kampuni ya TanPower Resources ambayo iliuziwa Mgodi wa Kiwira na kushindwa kuundeleza.

Mheshimiwa Spika, Madhara ya Deni la Taifa yanaonekana hapa katika matuumizi ya Serikali ambapo tunapokuwa tunalipa madeni tunachukuwa rasilimali fedha nyingi kutoka kwenye Miradi ya Maendeleo. Wakati Bajeti ya Maendeleo ni shilingi trilioni 4.5, Bajeti ya kugharamia Deni la Taifa ni shilingi trilioni 2.7 (sawa na nusu ya Bajeti nzima ya Maendeleo).

Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2012/13 ni ya kulipa madeni zaidi kuliko Bajeti ya kuchochea maendeleo ya Taifa letu. Bajeti hii pia yaweza pia kuwa ni Bajeti ya kukopa zaidi maana jumla ya TZS 5.1 trilioni (USD 3.19 Billion) zitachukuliwa na Serikali kama mikopo kutoka vyanzo mbalimbali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha uliopita.

Mheshimiwa Spika, Mgawanyo wa rasilimali za nchi kwenye sekta za kipaumbele (Miundombinu ya usafirishaji kama reli, bandari, ndege viwanja vya ndege n.k), Barabara, nishati,kilimo na mifugo, ili kuinua uchumi zimetengewa fedha kidogo sana kuweza kuleta tija kulingana na malengo ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyopitishwa na Bunge lako tukufu. Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya nishati imeshuka kwa kiwango cha shilingi 40 bilioni, pia kwa mwaka uliopita fedha zilizotengwa kwa ajili ya miundombinu,reli na TEHAMA zilitengwa shilingi 2,781.4 bilioni kwa 2011/12 ikilinganishwa na shilingi 1,505.1 bilioni kwa mwaka 2010/2011,(hili lilikuwa ni ongezeko la asilimia 85). Kwa bajeti ya mwaka huu inaonesha sekta zilezile za vipaumbele; bajeti iliyotengwa ni shilingi 1.394.5 bilion ambayo ni pungufu ya asilimia 49.86 kwa kulinganisha na mwaka 2011/2013.

Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa Fedha analiambia Bunge kuwa ametenga shilingi bilioni 1,383 kwa ajili ya Usafirishaji na Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi imetengewa shilingi bilioni 1,000 kati ya hizo. Wizara ya Uchukuzi yenye Reli, Bandari, Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Maziwa ya Tanganyika, Nyasa na Viktoria imetengewa chini ya shilingi bilioni 380. Serikali pia haijasema fedha ambazo zilitengwa na Bunge katika Bajeti inayomaliza muda wake na kuzielekeza kwenye Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Uchukuzi zimetumikaje maana bado wakandarasi wanadai na fedha za Reli hazikutoka zote kama ilivyopitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, wizara nyingi hazikupata fedha za Maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge. Halmashauri za Wilaya ndio zilipata hali mbaya zaidi katika kupata fedha za Maendeleo ambapo kwa wastani ni asilimia 47 tu ya Bajeti ndio ilipelekwa katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa. Kutokana na hali hii Wabunge kama wawakilishi wa wananchi walihoji Serikali kwenye Kamati zao na kupata majibu ambayo sio ya kuridhisha hivyo kupelekea Wabunge kugomea baadhi ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, Ushahidi wa hayo ni baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge kukataa kukubali Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa baadhi ya Wizara zilizo chini ya Kamati hizo. Wizara ambazo hazikupitishiwa /Kukubaliwa makadirio yake ni pamoja na;

· Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,

· Wizara ya Uchukuzi, na (nilishangaa kumwona Waziri wa Uchukuzi akiwaahidi wananchi pale Jangwani kwamba Reli inakarabatiwa vya kutosha ilhali Kamati haijapitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa kuwa haikupewa fedha za kutosha)

· Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika

Mheshimiwa Spika, kabla Bunge lako tukufu halijajadili Makadirio ya Matumizi ya mwaka unaokuja ni vema Serikali itueleze kwanza fedha zilizotengwa mwaka uliopita na hazikufika hatima yake nini?

Mheshimiwa Spika, uwiano wa bajeti iliyotengwa kwa matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia 70% wakati bajeti ya maendeleo asilimia 30% haiwezeshi nchi kupiga hatua ya haraka ya Maendeleo. Kama ilivyoonyeshwa na Waziri Kivuli Mipango na nitakavyohitimisha hotuba hii, Serikali imetayarisha Bajeti hii bila kuzingatia masharti yaliyowekwa na Mpango wa Maendeleo uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu ibara ya 63 (3)(c) kwa kutotenga asilimia 35 ya Mapato ya ndani ya Serikali kwenye Bajeti ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo katika miradi ya maendeleo katika bajeti zake. Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), matumizi ya kawaida ya Serikali yanaongezeka huku matumizi katika shughuli za maendeleo yanapungua mwaka hadi mwaka. Takwimu katika jedwali hapa chini zinaonyesha

Fungu

2009/2010

%

2010/2011

%

Fedha za matumizi ya kawaida (Sh)

6,251,629,581,428

73

7,587,424,923,903

77

Fedha za matumizi ya maendeleo (Sh)

2,299,010,652,135

27

2,223,684,150,465

23

Jumla

8,550,640,233,563

100

9,811,109,074,368

100

Chanzo: Ripoti ya CAG, uk. 21

Aidha, kwa miaka miwili iliyopita yaani 2009/2010 na 2010/2011 kumekuwa hakuna uwiano wa fedha za Maendeleo kama bajeti zilivyopitishwa na Bunge dhidi ya fedha zinazotolewa na hazina kwa ajili ya maendeleo katika Wizara na Idara. Tazama jedwali;

Mwaka

Bajeti iliyoidhinishwa

Fedha halisi zilizotolewa

Tofauti (Sh)

%

2009/2010

2,825,431,400,000

2,299,010,652,135

526,420,747,865

19

2010/2011

3,750,684,569,000

2,223,684,150,465

1,527,000,418,535

41

Chanzo: Ripoti ya CAG, uk.22

Mheshimiwa Spika, Kutokana na takwimu hizi, jumla ya Sh. 1,527,000,418,535 au asilimia 41 ya fedha zilizoidhinishwa kwa maendeleo hazikutolewa katika mwaka wa fedha 2010/2011, na kiasi cha Sh. 526,420,747,865 au asilimia 19 ya fedha zilizoidhinishwa mwaka 2009/2010 hazikutolewa pia. Hii ina maana kuwa shughuli za maendeleo za kiasi hicho cha fedha hazikutekelezwa kwa miaka husika.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatafsiri hali hiyo kama utovu mkubwa wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa upande wa Serikali, Vilivile inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu haithamini maendeleo ndio maana kila mwaka Serikali inazidisha matumizi yake na kuhakikisha kuwa inayapata kwa wakati huku ikipunguza bajeti ya maendeleo na kutotoa fedha zote kama zilivyoidhinishwa na mbaya zaidi hata zile zinazotolewa hazitolewi kwa wakati muafaka. Hii inafanya kukaa hapa Dodoma na kupitisha Bajeti kuwe hakuna maana maana Bajeti haitekelezwi kama ilivyopitishwa.

Mheshimiwa Spika, Kiasi kinachotengwa kwa ajili ya maendeleo kimeshuka kutoka shilingi trilioni 4.9 katika mwaka wa fedha 2011/12 hadi kufikia kiasi cha shilingi trililioni 4.5 mwaka huu wa fedha 2012/13. Pamoja na serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika bajeti iliyopita, bado imeendelea kupunguza bajeti ya maendeleo katika bajeti hii. Ni dhahiri serikali haizingatii swala la maendeleo ya mwananchi, pia kutoona njia ya kuweka mkazo katika maendeleo na kuendelea kupuuzia maazimio ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, katika Bajeti mbadala, Kambi ya Upinzani imetenga asilimia 36.06 na kukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kutoka katika mapato ya ndani kwa matumizi ya maendeleo kama Mpango wa Maendeleo ya Taifa ulivyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, Tuliamua kama Taifa kwamba Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ndio safina yetu ya kuelekea nchi ya ahadi (middle income country). Mpango ukapitishwa na Bunge na kuwekwa sahihi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inasikitisha kuona kuwa Serikali inatoboa kisiri siri safina hii wakati tupo kati kati ya maji! Ninaamini wananchi wanawaona wanaotoboa safina yetu na watawatosa kabla hawajazamisha Taifa zima kwa kushindwa kutekeleza Mpango unavyoelekeza.

Ubadhirifu wa fedha zinazotengwa

Mheshimiwa Spika, pamoja na fedha za maendeleo kutolewa kidogo kulinganisha na bajeti inayopitishwa na Bunge, bado kumekuwepo na matumizi yasiyo na tija na ubadhirifu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, upotevu wa fedha za umma umeendelea kuwa kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa
na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.


MAPENDEKEZO YA KAMBI YA UPINZANI

SERA YA MATUMIZI 2012/13 KWA BAJETI MBADALA

Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Bajeti Mbadala ni kuhakikisha uchumi unakua katika maeneo ya vijijini kwa kati ya asilimia 6 na 8 ili kuleta Maendeleo ya wananchi na kutokomeza umasikini. Kwa njia hiyo ni dhahiri wananchi wapatao milioni 30 waishio vijijini watanufaika na matumizi ya raslimali zao.

Vipaumbele vya bajeti ya Matumizi.

(i) Kujenga Mazingira ya Ukuaji wa uchumi vijijini (rural growth) kwa kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, maji na miundombinu ya Umwagiliaji. Tunapendekeza kutumia shilingi bilioni 600 kila mwaka (bilioni 150 kwa kila sekta niliyotaja). Fedha hizi zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural Development Authority – to be established) itakayokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

(ii) Kukarabati Reli ya Kati na matawi yake ya Tanga/Arusha na Mpanda. Tutatenga tshs 443bn kwa RAHCO kwa ajili ya Reli. Lengo ni kuhakikisha Reli ya Kati inafikia uwezo wa kusafirisha Tani 1.5m kwa mwaka na hivyo kulipatia Taifa fedha za kigeni katika sekta ya usafirishaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Tunataka sekta ya usafirishaji iliingizie Taifa fedha za kigeni mpaka dola za kimarekani 1.5 bilioni kutoka dola 0.5 bilioni za sasa.

(iii) Kuboresha Elimu na Afya hasa kwa Shule na Zahanati/Vituo vya Afya vya Vijijini kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wa Sekta hizi walio kwenye Halmashauri za Wilaya. Tunapendekeza posho za Mazingira ya Vijijini kwa Walimu, Madaktari na Manesi sawa na mara moja na nusu ya Mishahara yao. Vile vile tutaongeza mishahara ya Walimu, Manesi na Madaktari kwa asilimia 50, pamoja na kuboresha stahili zingine za kazi ili kuvutia Watanzania wengi zaidi katika maeneo haya na kuboresha huduma zao kwa wananchi.

(iv) Kuongeza Kima cha chini cha Mshahara kwa Wafanyakazi wa Umma mpaka Tshs 315,000 kwa Mwezi

(v) Kuanzisha Pensheni ya uzeeni kwa Wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

(vi) Kujenga Uwezo wa Viwanda vya ndani ili Kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo zilizoongezewa thamani. Tutazuia kuuza nje Korosho ghafi na Ngozi ghafi kwa kuanzia. Lengo ni kufufua viwanda vyote vya nguo na kuanzisha viwanda vipya kwa kutoa motisha kwa wawekezaji watakaotumia malighafi za hapa nchini.

(vii) Kupunguza mzigo wa matumizi ya magari ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya ‘mashangingi’ na kuweka mfumo wa kukopesha Magari kwa watumishi wote wa Umma wanaostahili Magari kama alivyofanya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha alitamka, ‘….kufanya mapitio ya stahili za aina za magari kwa viongozi wa ngazi mbalimbali na kuandaa mwongozo wa kugharamia ununuzi wa vyombo vya usafiri ili kupunguza matumizi ya magari, mafuta na matengenezo ya magari…’ kama hatua za kubana matumizi. Hatua hii ya kupunguza gharama za magari Waziri hakuisema kabisa katika hotuba yake Bungeni.

(viii) Kuendelea kusisitiza kufutwa kwa posho za vikao katika mfumo mzima wa malipo na stahili kwa watumishi wa Umma. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha, Waziri wa Fedha alitamka ‘…. Kufanya mapitio ya posho na stahili zote kwa lengo la kuziwianisha….’ Suala hili nalo Waziri hakulizungumza kabisa katika Hotuba yake Bungeni.

(ix) Kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili kuzalisha wataalamu wa kutosha wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa Taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo na hivyo kufaidika na Utajiri wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu. Tunapendekeza shilingi bilioni 200 mwaka huu katika Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa ajiri ya Mradi huu.

(x) Kutunga sheria mpya ya Mashirika ya Umma (Public Corporations Act) ili kujengea uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vyema Mashirika yote ya Umma ambayo Serikali inamiliki kwa zaidi ya asilimia 100 na kutoa nguvu za kisheria kwa Shirika la CHC kuweza kusimamia hisa za Serikali katika Kampuni na Mashirika ambayo Serikali inamiliki chini ya asilimia 50.

(xi) Kupunguza gharama za safari za nje kwa kupunguza ukubwa wa misafara na madaraja ya kusafiria. Eneo hili la safari za nje limekuwa likiigharimu Serikali fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua mbali mbali za kikodi tulizozichukua Kambi ya Upinzani inapendekeza Bajeti ya shilingi trilioni 15 ambazo zitapatikana kwa Mapato ya ndani ya shilingi trilioni 11.9 na misaada na mikopo ya kibajeti ya shilingi trilioni 3.2 kama ilivyopendekezwa na Serikali. Kambi ya Upinzani inapendekeza Serikali kutokukopa kibiashara ili kudhibiti ukuaji wa Deni la Taifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba Serikali itatumia shilingi trilioni 9 katika Matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 6 kama Matumizi ya Maendeleo. Katika fedha za Maendeleo, asilimia 35 ya Mapato ya ndani yameelekezwa huko kama ilivyoagizwa na Mpango wa Maendeleo ya Taifa ulioidhinishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba.

SURA YA BAJETI MBADALA YA MWAKA 2012/2013

MAPATO

SHILINGI MILIONI

A

Mapato ya ndani

11,889,078

i)mapato ya kodi (TRA)

ii)Mapato yasiyo ya kodi

B

Mapato ya Halmashauri

C

Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)

842,487

D

Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo nay a kisekta

2,314,231

i)Misaada

1,465,461

ii)Misaada na mikopo kisekta

415,137

iii)MCC(MCA-T)

433,634

Jumla ya Misaada na mikopo ya kibajeti

3,156,718

JUMLA YA MAPATO YOTE.

15,045,796

MATUMIZI

E

Matumizi ya Kawaida

9,000,000

H

Matumizi ya Maendeleo

(i)Fedha za ndani

4,161,177

(ii)Fedha za Nje

1,884,619

Jumla ya matumizi ya maendeleo

6,045,796

JUMLA YA MATUMIZI YOTE.

15,045,796

Hitimisho

Fedha za Rada

Mheshimiwa Spika, Wakati Kamati za Bunge zilipokaa kujadili taarifa ya Serikali kuhusu Mfumo wa Mapato na Matumizi, Waziri wa Fedha na Uchumi alitoa Taarifa kuhusu Fedha za Rada zilizorejeshwa, jumla ya shilingi 72.3 bilioni ambazo zilipokelewa tarehe 26 Machi, 2012. Kwa mshtuko wa Wabunge, Waziri aliiambia Kamati kuwa mchakato wa manunuzi ya vitabu na madawati kwa kutumia fedha hizi ulikuwa umeanza chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI. Fedha hizi hazijawahi kupitishwa na Bunge lako tukufu. Kitendo cha Serikali kuzitumia kabla ya kupitishwa na Bunge ni kuvunja sheria za Fedha kuhusiana na masuala ya Bajeti. Wakati Waziri akiwasilisha Hotuba yake hakugusia kabisa suala la fedha zilizorejeshwa kutokana na Ununuzi wa Rada!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inataka maelezo ya Serikali juu ya Fedha hizi na utaratibu wa kuzitumia. Kambi inataka kufahamu vigezo vilivyotumika kuteua mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam kutumia fedha hizi. Kambi pia inapenda kufahamu Deni lililochukuliwa kununua Rada hii iliyoleta kashfa kubwa sana hapa nchini limefikia kiasi gani kulilipa na tukililipa tutakuwa tumelipa kiasi gani kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Uumbaji wa bajeti ya Serikali umekuwa ni ule ambao unapendelewa zaidi na wale wavivu wa kufikiri, yaani mfumo rahisi, wataalamu wanauita Incremental Budgeting. Mfumo huu hujikita zaidi katika kutizama ukuaji wa mapato na kugawa mapato hayo kwa mtindo wa nyongeza ya asilimia Fulani toka katika bajeti iliyotangulia. Mfumo huu huacha kuzingatia mambo mengi mtambuka. Mfano, tunaweza tizama sekta mojawapo ya umeme ambapo tukifanya uumbaji wa bajeti kwa mfumo wa kiasi cha nyongeza (incremental budget) kuna thamani halisi ambazo ukizitizama kwa bei wazi ya soko tayari zimepaa sana ndani ya miezi kumi na miwili.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni, tukiwa ni serikali ambayo tunasubiri kukabidhiwa dola, tunapendekeza kwamba ni vema tukaanza kutizama uwezekano wa matumizi ya Zero Budgeting ambapo japo ni mfumo ambao unahitaji kazi ya ziada, lakini una faida sana kwani hutizama mipango ya matumizi kulingana na wakati uliopo huku ikifanya rejea ya wakati uliopita.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kwamba Bajeti za Mashirika ya Umma ziwe sehemu ya Bajeti Kuu ya Nchi kwani kuna masuala mengi yanayotekelezwa na Mashirika haya na Wananchi kupitia Bunge hawayajui. Ni vema katika mfumo mpya wa Bajeti tutakaokuwa nao kufuatia mapendekezo ya Spika wa Bunge ambapo kutakuwa na Ofisi ya Bajeti ya Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti, Sheria ya Bajeti (Fiscal Responsibility Act/Budget Act) izingatie suala la kuziweka kama viambatisho Bajeti za Mashirika ya Umma katika Bajeti ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka huu kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha imewasahau kabisa wananchi wa vijijini na haina mkakati wowote wa kuwakomboa watanzania walio wengi wanaoishi huko. Mipango mingi ya kikodi katika sera ya Mapato ya Serikali itasaidia wakazi wa mijini ambao ni asilimia 25 tu ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inapenda kuweka msisitizo kwamba Tanzania bado ni nchi ya Wakulima maana robo tatu ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo hawajui hizi hadithi za Uchumi kukua tunazoimba na kupewa sifa kila siku. Hawa ni watu milioni 30 ambao hawana Maji, hawana Umeme, mazao yao hayafiki sokoni maana hawana barabara nzuri, shule wanazosoma watoto wao hazina walimu maana wanakimbia mazingira magumu. Hawa Watanzania wa chini milioni 30 (The Bottom 30M) tunaowawakilisha hawana bima mazao yakiharibiwa na wala hawana pensheni wanapokuwa wamezeeka na kupoteza nguvu za kufanya kazi. Hawa ‘The Bottom 30M’ bado wanaishi maisha walioshi babu zetu. Hawa Watanzania milioni 30 tumewasahau. Tunajenga Mataifa mawili ndani ya nchi moja, moja la mafukara (wanavijiji) na moja la wanaojiweza (wamijini).

Mheshimiwa Spika, Kama tunataka kujibu kitendawili cha kuwa na Uchumi unaokua kwa kasi lakini haupunguzi umasikini inabidi kuelekeza nguvu zetu vijijini walipo Watanzania wengi. Kukuza Uchumi wa Vijijini kwa kuwekeza kwenye misingi ya kujenga uchumi imara ndio njia pekee ya kutokomeza ufukara wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani mwaka huu ni Bajeti ya Ukombozi wa mwananchi. Licha ya kwamba tunahitaji ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi. Changamoto sasa ni namna gani ukuaji huu wa uchumi unawafikia wananchi milioni thelathini wa Vijijini na kuboresha maisha yao.

Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliwasilishwa Bungeni na Serikali na kupata pongezi nyingi sana kutoka kwa waheshimiwa wabunge lakini cha kushangaza Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kuutekeleza kwa vitendo mpango huu wa Taifa. Mwaka wa kwanza Mpango haukuwekewa fedha kwa kuwa ulikuwa wa Mpito. Mpango unahitaji angalau shilingi trillion Nane kila mwaka ili uweze kutekelezwa. Mpango ulipata shilingi trillion moja tu mwaka 2011/12.

Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bunge liliazimia namna ya kuhakikisha tunapata fedha za kuendeleza nchi yetu sisi wenyewe, naomba kunukuu ukurasa wa 92 kifungu cha 4.3.1 katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano toleo la kiswahili kama ifuatavyo ‘kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka’ mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, KWA KUWA katika makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/13 Serikali imetenga asilimia sifuri ya Mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia Bajeti ya Maendeleo. Serikali hii imeshindwa kusimamia ahadi zake yenyewe kama inavyoonekana katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Serikali hii ya CCM imeshindwa kuheshimu Uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(c ) madaraka ya Bunge ni pamoja na ‘Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo”. Bunge liliidhinisha Mpango kwa mujibu wa ibara tajwa ya Katiba.

Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bajeti ya mwaka 2012/13 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi haikukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama ambavyo ulipitishwa na Bunge, HIVYO BASI,

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iiondoe (withdraw) Bungeni Bajeti iliyoileta ili ikatayarishwe upya ili ikidhi matakwa (compliance) ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na kusainiwa na Rais wa nchi.

Mheshimiwa Spika Naomba Kuwasilisha

………………………………………………….

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Waziri wa Fedha na Uchumi Kivuli

18.06.2012

SURA YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2012/2013.

MAPATO

%

SHILINGI MILIONI

A

Mapato ya ndani

57.63

8,714,671

i)mapato ya kodi (TRA)

8,070,088

ii)Mapato yasiyo ya kodi

644,583

B

Mapato ya Halmashauri

362,206

C

Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)

5.57

842,487

D

Mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo na ya kisekta

15.30

2,314,231

E

Mikopo ya ndani

10.78

1,631,231

F

Mikopo yenye masharti ya kibiashara

8.25

1,254,092

JUMLA YA MAPATO YOTE.

15,119,644

MATUMIZI

E

Matumizi ya Kawaida

71.06

10,591,805

(i) Deni la taifa

2,745,056

(ii) Mishahara

3,781,100

(iii) Matumizi Mengineyo

4,065,649

Wizara

3,311,399

Mikoa

49,701

Halmashauri

704,549

H

Matumizi ya Maendeleo

(i)Fedha za ndani

2,231,608

(ii)Fedha za Nje

2,34,231

Jumla ya matumizi ya maendeleo

29.94

4,527,839

JUMLA YA MATUMIZI YOTE.

15,119,644

TOFAUTI KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI

Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani2012/2013

Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013

Kukuza uchumi vijijini.

Mwelekeo na malengo ya Serikali hauleweki, hatua zilizochukuliwa ni koboresha uchumi wa mijini.

Njia mbadala zinazotekelezeka za kupunguza mfumuko wa bei.

Kuwa na njia zilezile zilizoshindwa mwaka wa fedha uliopita za kupunguza mfumuko wa bei.

Kunufaika na mapato ya mitaji “Capital gains” kwa kutoza kodi kwa mali za kampuni zilizopo nchini kwa mauzo yanayofanyika nje ya nchi na hivyo kupanua wigo wa TRA kutoza kodi

Kutoza hisa kwa mauziano ya hisa pekee kwa mauziano yanayofanyika nje. Hisa inapunguza wigo wa TRA kutoza kodi.

Kupanua wigo wa kodi ya tozo la ujuzi (SDL)kwa kuijumuisha serikali na mashirika ya umma na kupunguza mzigo kwa sekta binafsi pekee.

Kupitia upya SDL bila kuonyesha namna itakavyofanyika.

Kupunguza misamaha ya kodi kutoka 3% ya sasa hadi 1% ya pato la taifa.

Kurudia ahadi zilezile za mwaka jana za kupitia upya misamaha ya kodi bila kuleta mrejesho wa kile walichokifanya.

Kuboresha kodi sekta ya madini ili kupelekea taifa kupata nagalau 25% ya mazuo ya madini nje kama mapato ya serikali.

Kutokuwa na hatua yoyote ya kuongeza mapato ya Serikali kutoka katika sekta ya madini.

Kulipa kima cha chini cha mshahara kuanzia shilingi 315,000.

Kulipa shilingi 170,000 kama kima cha chini.

Kulipa pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea

Kutokuwa na mfumo wa pensheni kwa wote.

Kushusha kiwango cha chini kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) kutoka 14% hadi 9% ili kumpunguzia mfanyakazi makali ya maisha na kutoza kodi zaidi kwa watu wenye kipato kikubwa

Kubaki na kiwango kilekile cha chini cha kodi ya 14% na kubakiza mfumo ule ule wa kodi ya Mapato unaomfanya Masikini alipe zaidi ya Tajiri.

Kuziba mianya kwa makampuni ya simu kukwepa kutokulipa kodi ya mapato.

Kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi na hivyo kumwongezea gharama mwananchi.

Kuondoa mikopo ya kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa madeni

Kuendelea mikopo na hivyo kuongeza deni la taifa. mingi ya kibiashara.

Kutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyoelekezwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

Kutenga asilimia sifuri ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo na hvyo kutokutekeleza mpango wa taifa .

Utegemezi wa Bajeti 21.3%

Utegemezi wa Bajeti 42.37%

JEDWALI LA ULINGANISHO WA ASILIMIA KWA BAJTEI MBILI

UPINZANI

ASILIMIA

SERIKALI

ASILIMIA

Mapato ya ndani

78.70

Mapato ya ndani

57.63

Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)

5.57

Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)

5.57

Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y a

kisekta

15.30

Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y a

Kisekta

15.30

Mikopo ya masharti ya kibiashara ya ndani

0

Mikopo ya masharti ya kibiashara ya ndani

10.78

Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje.

0

Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje.

8.25

Matumizi ya Kawaida

59.22

Matumizi ya Kawaida

71.06

Matumizi ya Maendeleo

40.78

Matumizi ya Maendeleo

29.94

Matumizi ya maendeleo fedha za mapato ya ndani

36.06

Matumizi ya maendeleo fedha za ndani

0

Matumizi ya maendeleo fedha za nje

12.39

Matumizi ya maendeleo fedha za nje

29.94

‘Licha ya kwamba tunahitaji ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi. Changamoto sasa ni namna gani ukuaji huu wa uchumi unawafikia wananchi milioni thelathini wa Vijijini na kuboresha maisha yao.’ Zitto Kabwe, Waziri Kivuli wa Fedha, Tanzania.(KUPA HABARI MPYA BOFYA HAPA

Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA