Home » » MBUNGE FILIKUNJOMBE ATINGA GEREZANI KULA KRISMAS NA WAFUNGWA

MBUNGE FILIKUNJOMBE ATINGA GEREZANI KULA KRISMAS NA WAFUNGWA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Monday, December 26, 2011 | 10:25 PM

Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kulia akishiriki chakula na wawekezaji wa kichina jana nyumbani kwake Ludewa

MBUNGE wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe ametembelea wafungwa wa gereza la Ludewa na kula nao chakula cha krismas pamoja na kuwapa misaada mbali mbali ikiwemo ya mashuka 200 na kuomba serikali kusaidia uboreshaji zaidi wa magereza hapa nchini.


Mbunge Filikunjombe alitoa msaada huo jumatatu ya Krismas na kuelezea ziara yake katika gereza hilo kuwa ni kutaka kuwafariji wafungwa na mahabusu wa gereza hilo kwa madai kuwa ni wapiga kura wake na wanahitaji kufarijiwa zaidi.

Akizungumza baada ya kutoka kula chakula na wafungwa na mahabusu hao ,mbunge Filikunjombe alisema kuwa zipo changamoto mbali mbali ambazo amepata kuziona katika gereza hilo kutoka kwa askari wake hadi wafungwa hasa katika uboreshaji wa nyumba za watumishi na gereza hilo zaidi.


Kwani alisema kuwa gereza lipo kwa ajili ya kila mmoja hata kama mbunge ama kiongozi wa serikalini na kuwa iwapo wao kama wabunge wasiposaidia kupigia kelele uboreshaji wa magereza nchini ipo siku na wao wanaweza kufikishwa hapo.


Hivyo alisema kuwa kwa upande wake mara baada ya kufika na kula chakula na wafungwa hao pia alipata nafasi ya kuwafariji na kuwasikiliza kero zao na kuwa moja kati ya kero ni juu ya kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi katika wilaya hiyo ya Ludewa ambayo mbali ya kuwa na jengo zuri la mahakama ila haina hakimu .


Aliiomba idara ya mahakama nchini kusaidia kupunguza msongamano wa mahabusu katika gereza hilo kwa kutatua tatizo la uhaba wa hakimu wa wilaya katika wilaya hiyo .

Kuhusu uchakavu wa nyumba za watumishi katika gereza hilo alisema kuwa nyumba nyingi za gereza hilo zimechakaa kutokana na kujengwa muda mrefu na tatizo la mchwa kuendelea kuwa kubwa eneo hilo.

Pia mbunge huyo aliahidi kuwasaidia TV wafungwa wa gereza hilo pamoja na radio ili kuweza kupata haki yao ya msingi ya kupata habari na kuweza kujifariji zaidi wakati wakitumikia adhabu yao.

Mbali ya misaada hiyo pia alikabidhi sabuni ,mafuta ,miswaki na dawa ya meno pamoja na kandambili kwa kila mfungwa na mahabusu wa gereza hilo huku akiwataka pindi wanapotoka gerezani kujiepusha na vitendo vya uharifu ambavyo vimewafikisha hapo.

Wakati huo huo mbunge huyo amepongeza ujio wa wawekezaji wa kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Ltd (TCMR) iliyoshinda zabuni ya kuwekeza katika migodi ya Mchumchuma na Liganga ambayo inakusudia kuanza utekelezaji wa awali wa uzalishaji wa makaa ya mawe, umeme na chuma katika migodi hiyo.

Wataalamu elekezi 20 wa TCMR ambayo ni kampuni mbia wa Shirika la China la Sichuan Hongda Corporation na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) wako wilayani hapa wakindelea na utafiti kabla ya miradi hiyo kuanza rasmi.

Mbunge wa Jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe amesema huu ni wakati muafaka kwa wenyeji na wawekezaji wengine kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuboresha huduma zitakazorahisha utekelezaji wa miradi hiyo.

“Huduma hizo ni pamoja na ujenzi wa nyumba, hoteli za kisasa, na maduka ya bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula,” alisema.

Watalaamu hao wote wachina ambao kati yao ni mmoja tu ndiye anayezungumza lugha ya kingereza wamebobea katika masuala ya umeme, viwanda, michoro, utafiti na ujenzi wa miradi hiyo.

Akizungumza na wanahabari katika eneo linalopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kuzalishia umeme la Nkomang’ombe huko Mchuchuma, Kiongozi wa watalaamu hao, Jiang Mzingnua alisema ujenzi wa mradhi huo wa umeme unatarajiwa kuanza mwaka mmoja na nusu baadaye, baada ya kukamilisha shughuli zote za kitafiti na michoro.

“Baada ya hapo kwa haraka sana tutaanza ujenzi wa mradi wa umeme utakaozalishwa kwa kutumia makaa ya mawe tutakayokuwa tukizalisha katika eneo hili la Mchuchuma,” alisema.

Alisema kwa kuanzia mradi wa umeme wa Mchuchuma utazalisha Megawati 600 ambazo kati yake 300 zitatumika kwa ajili ya kiwanda chao cha chuma kitakachojengwa katika mgodi wa Liganga.

Akiyataja baadhi ya faida watakazozipata wakazi wengi wa wilaya ya Ludewa kutokana na kuwepo kwa miradi hiyo ni pamoja na ajira na uboreshaji wa miundo mbinu na shughuli zingine za kimaendeleo.

Kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, kampuni hiyo inatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi 8,000 watakaotumiwa kufanya kazi mbalimbali za awali katika kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo.

Mzngnua aliyekuwa akiongea kwa lugha ya kichina huku Afisa wao mahusiano Tony Tan akitafsiri wa kingereza alisema kama ilivyo katika mkataba, kampuni hiyo itaboresha miundo mbinu ya barabara kwa kujenga barabara yenye ubora itakayounganisha eneo la Mchuchuma na Liganga.
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA