Home » » BARAZA LA MAASKOFU WAHOFIA USALAMA WA KATIBA

BARAZA LA MAASKOFU WAHOFIA USALAMA WA KATIBA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Sunday, December 11, 2011 | 8:47 PM


SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kusaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), limesema kwamba kupitishwa kwa harakaharaka muswada huo inaweza kuipeleka nchi pabaya.

Pamoja na hayo, TEC imesema kitendo cha Serikali kukusanya maoni katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Visiwani Zanzibar peke yake, haitoshi kujenga hoja ya kusaini ama kupitisha muswada huo wa Katiba.Mwandishi wa mtandao huu kutoka Jijini Mwanza, Sitta Tumma anaripoti kwamba; Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Jude Thaddaeus Ruwa'ichi aliyasema hayo jana usiku Jijini Mwanza, muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kilichoandikwa na John Kasembo, na kufanyika katika ukumbi wa Mwanza hoteli.Ruwa'ichi ambaye alihojiwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na suala zima la mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya hapa nchini, alisema, suala la kuundwa kwa Katiba mpya si hiari ya Rais wala kundi na tabaka fulani, bali ni la Watanzania wote.


Akizungumza kwa kutumia neno 'Mbindembinde', Rais huyo wa TEC ambaye pia ni Baba Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza alisema, Rais kabla hajasaini Muswada huo wa Katiba, Watanzania wengi walitaka Muswada huo usisainiwe, na kwamba Mkuu huyo wa nchi alipaswa kusikiliza mawazo ya wananchi wake, na si kuwahi kusaini na kuwa Sheria."Katiba ndiyo mhimili wa taifa lolote duniani.

Kabla ya Rais hajasaini muswada huu, ilitakiwa wananchi wote washirikishwe kutoa mawazo yao kwamba wanataka Katiba ya namna gani!.

"Suala la kuchukuwa maoni kwa mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar pekee, haitoshi kabisa. Na jambo hili la Katiba mpya likipelekwa mbindembinde linaweza kuipeleka nchi hii kubaya, hatutaki tufike huko", alisema Rais huyo wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Ruwa'ichi.Hata hivyo, Ruwa'ichi ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika uzinduzi wa kitabu hicho cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kilichoandikwa na John Kasembo, alieleza kushangazwa na kitendo cha Bunge kupitisha harakaharaka muswada huo.Alihoji kwamba: "Hivi Bunge linashughulikia maslahi ya nani?.

Wabunge wamepewa dhamana na wananchi, hivyo ni lazima wawasikilize wanachotaka, halafu ndicho wakifanyie kazi, na si kuonekana kama ushabiki fulani.


Alipoulizwa kuhusu suala la udini linaloonekana kutumiwa na baadhi ya wanasiasa nchini, Rais huyo wa Baraza la Maaskofu, alikiri kuwepo kwa jinamizi hilo, na kusema ajenda ya udini kwa sasa imekuwa kama kichaka cha watu fulani kuficha maovu yao.Alionya kwamba, iwapo Serikali itaruhusu mijadala ya udini kutawala nchini, basi taifa lipo hatarini kupoteza ustawi wake, kwani Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipiga vita ubaguzi wa kidini, na kamwe watu wasitumie mgongo wa dini kuficha madhambi yao.


Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA