Home » » MADIWANI SENGEREMA WAMTOA JASHO RC WA MWANZA

MADIWANI SENGEREMA WAMTOA JASHO RC WA MWANZA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Saturday, November 19, 2011 | 4:16 AM

MADIWANI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wamekataa pendekezo la Mkuu wa mkoa huo, Evarist Welle Ndikilo, kuhusu watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo wanaotuhumiwa kwa ufisadi, kuchukuliwa hatua na Katibu Mkuu wa TAMISEMI, badala yake wanataka Baraza la madiwani ndilo liwashughulikie watendaji hao.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Mwanza, Sitta Tumma, anaripoti kwamba; hatua hiyo imejitokeza juzi wakati wa kikao maalumu kilichoitishwa dhidi ya madiwani wa CCM, kwa ajili ya kujadili mambo mbali mbali, kikao ambacho mgeni wake rasmi alikuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Ndikilo, ambaye alikwenda kutoa ufafanuzi wa barua yake ya kutaka watendaji hao wawajibishwe na Tamisemi, badala ya Baraza la madiwani.

Katika kikao hicho ambacho kinadaiwa kuhudhuriwa na madiwani wapatao 40 wa CCM, kisha kupewa posho ya kuanzia sh. 100,000 kila mjumbe, Mkuu huyo wa mkoa anasadikiwa kuwashawishi madiwani hao kuridhia ushauri wake huo, jambo ambalo lilipingwa vikali na idadi kubwa ya madiwani, wakitaka Baraza ndilo lenye mamlaka ya kuchukuwa hatua dhidi ya watendaji wabovu.

Mvutano huo umekuja kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayodaiwa kubainisha wazi upotevu wa mamilioni ya fedha, huku ripoti hiyo ikiwataja baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo ya Sengerema kuhusika na tuhuma hizo, na madiwani hao wana wasiwasi ofisi ya Katibu Mkuu wa TAMISEMI inaweza kuwalinda watendaji hao, na kushindwa kuwawajibisha.

Oktoba 25 mwaka huu, Baraza la madiwani la wilaya hiyo lililazimika kujigeuza kuwa kama kamati, kwa ajili ya kujadili ripoti hiyo na hatua za kuchukuliwa watendaji wote wanaohusishwa na ubadhilifu huo wa mali za umma, na kwamba baadaye kamati hiyo iliagiza kuitishwa kwa Baraza la madiwani ndani ya siku 21, ambayo imeishia Novemba 15 mwaka huu, bila Baraza kuitishwa.

Kufuatia hali hiyo tata, badala ya kuitishwa kwa Baraza hilo, inadaiwa uongozi uliwaita madiwani wote wa CCM kukutana Novemba 17 katika ukumbi wa ofisi za chama hicho mjini Sengerema, kwa lengo la kujadili na kuridhia ushauri wa Mkuu wa mkoa kwamba ofisi ya Katibu Mkuu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMI\SEMI), iachiwe kazi ya kuwawajibisha watendaji hao (majina tunayo).

Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kwamba, idadi kubwa ya madiwani ilikataa ushauri wa mkuu huyo wa mkoa, na kwamba kinachotakiwa ni Baraza la madiwani lenye mamlaka kisheria kuachiwa kazi hiyo, na si kutaka hoja hiyo kumezwa na mamlaka nyingine.

"Kikao kilikuwa moto kweli. Madiwani wengi wamekataa kabisa ushauriwa na mapendekezo ya RC Ndikilo. Wanataka Baraza la madiwani ndilo liachiwe mamlaka liliyonayo la kuwashughulikia watendaji waliotajwa na CAG kwa ufisadi.

"Diwani wa Kata ya Lugata, Adrian Tizeba alimhoji mkuu wa mkoa kapata wapi mamlaka ya kumeza madaraka ya Baraza la madiwani katika kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji hao?. Ushauri wa RC ulilenga kuchakachua utaratibu na kutaka kuwalinda hawa watu", kilisema chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina.

Licha ya mkuu wa mkoa kuwepo, kikao hicho kilihudhuriwa pia na mkuu wa wilaya ya Sengerema, Ellinas Palagyo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mathew Ndalahwa Lubongeja, mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Jaji Tasinga pamoja na viongozi wengine wa CCM ngazi ya wilaya.

Hata hivyo, chanzo cha habari kimeongeza kwamba, kuna kundi la baadhi ya madiwani wa CCM walikuwa wameandaliwa kwa ajili ya kupingana na kauli za wenzao wanaotaka watendaji hao washughulikiwe na Baraza la madiwani, wakihofia kwamba Baraza hilo litawafukuza kazi, tofauti na jinsi ambavyo lingeshughulikiwa na TAMISEMI.

Imeelezwa kwamba, ndani ya kikao hicho, RC Ndikilo alionekana kuchukizwa na ujumbe mfupi (SMS), alioupata ukidaiwa kuandikwa na mmoja wa madiwani wa wilaya hiyo, ukimtaja kwamba anataka kuwalinda mafisadi, na kwamba baada ya madiwani hao kuonekana kukataa hoja na ushauri wake huo, alilazimika kuaga na kuondoka kikaoni hapo kisha kurejea jijini Mwanza.

Hata hivyo, Ndikilo alipotafutwa na mtandao huu ili aweze kuzungumzia sakata hilo, hakuweza kupatikana mara moja.
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA