Home » » UKOSEFU WA SOKO LA MAHINDI LUDEWA PINGO KWA WANAWAKE NA WATOTO

UKOSEFU WA SOKO LA MAHINDI LUDEWA PINGO KWA WANAWAKE NA WATOTO

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Friday, August 12, 2011 | 5:24 AM


TATIZO la soko la mazao wilaya ya Ludewa mkoani Iringa ni chanzo wanawake na watoto kuendelea kunyanyasika kutokana na baadhi ya wanaume kujinufaisha zaidi kwa kukimbia familia zao kwa kisingizio cha kwenda kutafuta soko la mazao nje ya wilaya hiyo .


Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari za mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) katika kata hiyo ya Mavanga wilaya ya Ludewa ambayo ni moja kati ya kata zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao la mahindi kwa wingi unaonyesha kuwa wanaume wa kata hiyo wamekuwa wakijinufaisha na ukosefu wa soko la mazao katika kata hiyo kwa kusafirisha mazao nje ya wilaya hiyo na kutumia vibaya fedha za mauzo ya mazao hayo mjini kwa anasa.


Sarah Samson ni mwanamke mkazi wa kijiji cha Mavanga wilaya ya Ludewa anasema kuwa amekuwa akitunza watoto zaidi ya watano ambao ameachiwa na mme wake aliyetoweka kijiji hapo kwa zaidi ya miezi miwili sasa na magunia 50 ya mahindi kwa madai ya kwenda kuyauza kwa wafanyabiashara wa wilaya ya Njombe.

“Mateso yote haya nimekuwa nikiyapata kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika katika kata yetu na kama kungekuwa na soko hata mimi ningeweza kwenda kuuza mazao badala ya kumwachia mwenzangu kujinufaisha binafsi kwa mazao tuliyolima pamoja”

Mwanamke huyo anasema kuwa kila mwaka wakati wa mavuno mwenzake amekuwa akihama nyumba na kwenda kuishi mjini hadi pale fedha za mauzo ya mahindi zinapomalizika ndipo anaporejea kijijini .

Anasema kuwa katika kata yao zao kuu la biashara ni mahindi ila kutokana na kukosekana kwa soko la kuuzia zao hilo wakulima wamekuwa wakiendelea kulima kilimo cha mazoea kama njia ya kudumisha utamaduni wa mabibi na mababu ambao walikuwa wakilima kilimo hicho .

“Tulitegemea kuona serikali inasaidia kutunusuru na tatizo la ukosefu wa soko la uhakika la mazao kwetu sisi wananchi wa pembezoni mwa miji kwa maana ya wakulima ambao ndio tegemeo kubwa la uchumi wa Taifa la Tanzania …ila pamoja na kuwepo kwa ahadi nyingi za serikali katika kuendeleza kilimo na wakulima ila bado kwetu huku vijijini kilimo si ukombozi kutokana na kulima mazao ambayo yamekuwa yakiozea nje ya nyumba zetu kwa kukosa soko na hata kama tunabahatika kupata wanunuzi ni wale wanaokuja kununua kwa bei yao wenyewe”

Hata hivyo anasema kuwa katika wilaya ya Ludewa bado wakulima wamekuwa wakitumikishwa katika kilimo kwa kulipia gharama za mbolea ya ruzuku bila kupata faida kutokana na mazao wanayovuna kukosa wanunuzi na kama wanunuzi wanajitokeza ni wale wanunuzi wenye kutafuta kujinufaisha zaidi wao badala ya kumjali mkulima .

Sarah anasema kuwa pamoja na kulima na kupata mazao mengi zaidi ila bado amekuwa akiishi maisha ya tabu na watoto kutokana na kutokuwepo kwa soko la uhakika la mazao katika kata hiyo na kujikuta kila mwaka akilima mazao kwa ajili ya kumwezesha mume wake kutoka nje ya kata hiyo kwenda kujinufaisha kwa fedha za mazao hayo huku watoto wakikosa elimu kwa uhaba wa fedha.

Hata hivyo anasema kuwa kwa watoto wake wawili ambao wamefaulu mtihani wa darasa la saba amelazimika kuwaingiza katika orodha ya watoto wasio na uwezo ambao wanasomeshwa na mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe .

“Uwezo wa kufanya kazi ikiwemo ya kulima tunayo na tumekuwa tukilima kwa juhudi zote na kuvuna mahindi ambayo mwisho wa siku yamekuwa yakioza kwa kukosa soko na hata kama yanapata wanunuzi wa jumla ni wale ambao wamekuwa wakinunua gunia wakati mwingine kwa shilingi 5000 hadi 10000 fedha ambazo hazitoshi kuendesha maisha ya sasa”

Huku John Nkera mkazi wa Ludewa akidai kuwa sababu ya wanaume kukimbia familia zao na kwenda mijini ni kutokana na serikali kushindwa kuboresha masoko kwa wakulima hao hali inayopelekea baadhi yao pindi wanapokwenda kuuza mazao kujikuta wakihamia kwa muda mjini hadi pale wanapomaliza fedha za mauzo ya mazao yao ndipo hurejea kijijini jambo ambalo ni sawa na unyanyasaji katika familia zao.

Hata hivyo anasema kuwa wapo wanawake ambao wameachika ama kukimbia nyumba zao kutokana na kuchboshwa na tabia za baadhi ya wanaume ambao wamekuwa wakiwageuza punda kwa kuwatumikisha kulima na baada ya mavuno fedha zimekuwa zikiishia katika anasa mjini .

Akielezea kuhusu ubovu wa miundo mbinu katika kata hiyo anasema kuwa ubovu na ukosekanaji wa miundo mbinu ya uhakika vijijini ni chanzo cha wakulima kuendelea kugeuzwa watumwa wa wafanyabiashara katika kilimo .

Pia anasema kuwa yapo masoko yaliyojengwa na serikali kwa ajili ya wakulima toka mwaka 2008 ila masoko hayo yameshindwa kutumika kutokana na ujenzi wake kutozingatia mahitaji halisi ya wakulima ambao walikuwa wakihitaji masoko ya mazao na sio ya mboga mboga kama yalivyojengwa katika maeneo mengi ya wilaya ya Ludewa .

Anasema kuwa kwa sasa wakulima wamekuwa wakisafirisha mazao yao hadi mjini Ludewa umbali wa zaidi ya kilometa 50 ili kusafirisha mazao hayo kwenda wilayani Njombe ambako ni mwendo wa kilometa zaidi ya 200 kwenda kutafuta soko la uhakika la mazao hayo ambayo hata hivyo wamekuwa wakiuza kwa hasara kutokana na kutojua vema soko la mazao hayo mjini Njombe.

Hata hivyo anasema kuwa wapo wanawake ambao wameachika ama kukimbia nyumba zao kutokana na kuchboshwa na tabia za baadhi ya wanaume ambao wamekuwa wakiwageuza punda kwa kuwatumikisha kulima na baada ya mavuno fedha zimekuwa zikiishia katika anasa mjini .

Anasema kuwa serikali imekuwa ikihimiza wakulima kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya biashara kama kilimo cha mahindi na hata kusambaza pembejeo za kilimo za ruzuku ila wakati wa mavuno serikali tena imekuwa ikiwapiga marufuku wakulima kusafirisha mazao yao njue ya nje na kuwataka kuuza mazao hayo ndani ya nchi ambako soko lake limekuwa ni lile la kuwakandamiza wakulima na kuwanufaisha wafanyabiashara pekee.

“Hivi tunataka kuiuliza serikali leo kuwa ipo kwa ajili ya kumkomboa mkulima wa pembezoni ama ipo kwa ajili ya kuwanufaisha wafanyabiashara wa mijini ambao wamekuwa wakifika kununua mazao yetu kwa bei ya kutupwa ….tunauza gunia moja la mahindi kwa shilingi 5000 hadi 10000 wakati mbolea mfuko tunanunua zaidi ya shilingi 20,000 …hivi kweli serikali inaposema kilimo kwanza ni kwa manufaa ya mkulima ama wafanyabiashara “alihoji na kuiomba serikali kufanya utafiti ili kuona kama mkulima anavyonyanyasika kwa kilimo .

Nkwera anasema kuwa hivi sasa wakulima wa Tanzania tumegeuka kuwa watumwa katika nchi yetu kwa kuwatumikia wenye fedha bila sisi wenyewe kutambua kutokana na kulima kwa shida kubwa na mazao kuja kuyauza kwa bei ya kutupwa

Anasema kuwa wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Iringa imekuwa ikiongoza kwa kilimo cha mahindi kama ilivyo kwa wilaya ya Njombe ila wakulima wa wilaya ya Ludewa kutokana na kuwepo pembezoni zaidi ya barabara kuu ya lami wameendelea kuwa kulima bila mafanikio ya kiuchumi huku sehemu kubwa ya walima ambao wanaishi mashambani wameendelea kuishi katika nyumba za nyasi huku nje ya nyumba zao wamelundika mazao ya kutosha yasiyo ya soko .

“Mkulima wa wilaya ya Ludewa ameshindwa kabisa kujikwamua kiuchumi kwa kutumia kilimo cha zao la mahindi pamoja na kuwa kilimo cha mazao hili ndicho kinachowakomboa wakulima wa wilaya nyingine za mkoa wa Iringa ….ila kwetu wakulima wa Ludewa hadi sasa tunakwama kujinasua katika dimbwi la umasikini …hivi leo tujiulize serikali yetu imekuwa ikitangaza maisha bora kwa kila mtanzania na hata kuhimiza kila mwenye uwezo wa kufanya kazi kufanya kazi sasa sisi wakulima pamoja na kuitikia wito wa serikali kwa kufanya kazi na kujitahidi kutafua maisha bora ila bado serikali imekuwa ni kikwazo kwa kushindwa kutuwekea mazingira bora ya kuuzia mazao yetu na hata wakulima tunapotafuta njia ya kuuza mazao nje serikali imekuwa ikizuia kufanya hivyo”

Anasema kuwa kukosekana kwa soko la uhakika la kuuzia mazao yao ni moja kati ya sababu ya wanawake na watoto kuendelea kunyanyasika katika familia zao kutokana na baadhi ya wanaume kuendelea kuhama vijiji vyao na kuhamia mijini kwa kisingizio cha kwenda kutafuta soko la mazao na mwisho wa siku kilimo kimegeuka kuwa hatari katika ndoa zilizo nyingi kwa wakulima wa vijinini.

Huku mganga wa kituo cha afya Ibumi Victoria Haule akidai kuwa wakulima wa kata ya Ibumi wameshindwa kabisa kuchangia huduma ya bima ya afya kutokana na kushindwa kuuza mazao yao kama walivyotegemea na kuwa serikali ilitegemea kwa kipindi cha mavuno kama sasa wananchi wengi wangeweza kujiunga na mfuko wa bima ya afya ila imekuwa tofauti baada ya wananchi 7 pekee ndio wamepata kujiunga na mfuko huo kati ya wananchi zaidi ya 10000 waliotegemewa katika kijiji cha Ibumi pekee.

Anasema kuwa kwa kawaida wananchi wa Ludewa wamekuwa wakitakiwa kuchangia mfuko huo wa bima ya afya kiasi cha shilingi 10,000 kwa kila familia kwa mwaka ili kuachana na utaratibu wa kuchangia shilingi 3000 kwa kila wanapofika kutibiwa kwa kila siku ila bado kikwazo cha soko la mazao yao kimefanya wakulima hao kushindwa kuchangia mfuko huo.

Pamoja na wananchi hao kushindwa kuchangia mfuko huo wa bima ya afya bado wameshindwa kukamilisha kulipa deni la umeme wa mionzi ya jua ambao Zahanati ya kata hiyo ya Ibumi ilifungiwa kwa mkopo kwa makubaliano ya kulipa deni hilo la shilingi milioni 1 baada ya mavuno ila hadi sasa upo uwezekano wa zahanati hiyo kukosa huduma hiyo ya umeme baada ya kushindwa kulipa deni la shilingi 750,000 zilizosalia pamoja na makubaliano ya mwisho yalikuwa ni juni mwaka huu.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) anasema kuwa ufumbuzi wa kilio cha wakulima wa Ludewa ni serikali kufungua milango ya ununuzi wa mahindi katika vituo vya Shauri Moyo,Mlangali na Ludewa na kuwa iwapo vituo hivyo vitaanza kufanya kazi wakulima wa wilaya ya Ludewa watanufaika na kilimo cha zao hilo la mahindi.

Filikunjombe katika moja kati ya maswali yake bungeni alimwomba waziri wa kilimo na chakula kusikia kilio cha wakulima wa wilaya ya Ludewa kwa kufika katika vituo hivyo kununua mahindi ya wakulima hao kama njia ya kuwakomboa wakulima wa wilaya hiyo ambao kimsingi wamekuwa wakijituma zaidi katika uzalishaji wa mazao ya chakula ila kikwazo kwao ni soko.

Mbunge huyo anasema kuwa kwa muda sasa wakulima wa wilaya ya Ludewa wameendelea kukosa soko la uhakika la mazao ya mahindi huku serikali ikiwazuia wakulima hao kujitafutia soko la mahindi nje ya nchi .

Anasema kuwa kituo cha serikali cha ununuzi wa mahindi (GSR) kilichopo makambako wilaya ya Njombe ni kituo ambacho kipo mbali zaidi na wakulima wa wilaya ya Ludewa ambao hata wakijaribu kusafirisha mazao yao hadi Makambako bado miundo mbinu ya wilaya hiyo ni ya shida kutokana na kutokuwepo kwa barabara ya uhakika inayowezesha usafiri kufikika kwa urahisi hadi vijiji vya pembezoni zaidi na makao makuu ya wilaya ya Ludewa.

Kwa maoni na ushauri 0754 026 299 /0712 750199

MWISHO

Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA