Home » » 'LEVE"CCM IRINGA YAHOJI SEKONDARI YA CHUO CHA UALIMU KUKOSA WALIMU

'LEVE"CCM IRINGA YAHOJI SEKONDARI YA CHUO CHA UALIMU KUKOSA WALIMU

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Friday, April 1, 2011 | 2:38 AM

Mary Tesha katibu wa CCM Mkoa wa Iringa

CHAMA cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimeshangazwa hatua ya shule ya mazoezi ya chuo cha ualimu Kleruu katika Manispaa ya Iringa kuwa na tatizo la upungufu wa walimu wakati ni jiko la kupika walimu .

Hali hiyo imejitokeza leo wakati wa ziara ya viongozi wa CCM mkoa wa Iringa kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika maeneo mbali mbali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa .

Pamoja na kupongeza jitihada mbali mbali zinazofanywa na uongozi wa shule hiyo na wananchi wa kata ya Gangilonga katika kuendeleza shule hiyo bado katibu wa CCM mkoa wa Iringa Mary Tesha aliutaka uongozi wa shule ya sekondari Mazoezi Kleruu kueleza sababu ya shule yake kukosa walimu .

Alisema kuwa kimsingi shule hiyo ni sehemu ya nyenzo za kufundishia walimu katika chuo cha ualimu Kleruu na ndio sababu ya serikali kujenga shule hiyo ndani ya majengo ya chuo cha ualimu Kleruu hivyo uongozi wa shule hiyo kulia juu ya tatizo la walimu ni jambo la kushangaza .

“Tumefurahishwa sana na jitihada mbali mbali zinazofanywa na kamati ya ujenzi na wananchi wa kata hii ya Gangilonga pamoja na Manispaa ya Iringa katika kuboresha elimu Manispaa ya Iringa …ila kwa hili la kukosa walimu wa kutosha hapa shule ya sekondari Kleruu tunaomba maelezo ya kutosha” alisema katibu huyo.

Kwani alisema kuwa lengo la ziara ya CCM katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ni kutaka kuona jinsi ambavyo ilani ya CCM ilivyoanzwa kutekelezwa baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2010 ili kuona changamoto mbali mbali zinazokwamisha utekelezaji wa Ilani hiyo na mafanikio ya utekelezaji wa kipindi kifupi ambacho Rais Jakaya Kikwete ameingia madarakani.


Kwa upande wake mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi alisema kuwa Halmashauri hiyo ina jukumu kubwa ya kusimamia kwa umakini utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuwa siku ya kwanza kabisa ya kuanza kwa baraza jipaya la madiwani mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alikabidhiwa Ilani ya CCM kama kitendea kazi namba moja katika kutekeleza ahadi za serikali iliyopo madarakani.

Kwa upande wake mkuu wa shule ya Mazoezi Kleruu Yoram Mponzi alisema kuwa shule hiyo ina jumla ya walimu 17 japo awali kabla ya walimu 12 kwenda masomoni ilikuwa na walimu 28.

Hata hivyo alisema kuwa sababu kubwa iliyopelekea shule hiyo kuwa na upungufu wa walimu ni kutokana na utaratibu mpya wa wizara ya elimu ambapo ulisitisha utaratibu wa shule hiyo kuchagua walimu wanaohitimu katika chuo hicho kufundisha shule hiyo kabla ya kupangiwa walimu na katibu mkuu wa wizara ya elimu.

Pia alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002 ina jumla ya wanafunzi 842 wakiwemo wasichana 412 na wavulana 430 na ina kidato cha 1-IV.

Vyumba vya madarasa vilivyopo ni 16 maktaba ipo japo haijakamilika ,maabara vyumba 2 havijakamilika na chumba kimoja kiko kwenye hatua ya umaliziaji ,matundu ya vyoo vya wanafunzi 16.

Huku matundu ya walimu ya shule hayopo kabisa zaidi ya kutumia yale ya chuo cha ualimu pekee.
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA