Home » » MWAKALEBELA WA TFF SASA NI WA CCM ATANGAZA RASMI KUMPOKEA UBUNGE MONICA MBEGA IRINGA MJINI

MWAKALEBELA WA TFF SASA NI WA CCM ATANGAZA RASMI KUMPOKEA UBUNGE MONICA MBEGA IRINGA MJINI

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Tuesday, June 15, 2010 | 7:47 AM


KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela ametangaza kumvaa na kumng’oa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Monica Mbega katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Monica Mbega ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amekuwa Mbunge wa wa kuchaguluiwa Jimbo la Iringa Mjini kwa awamu ya pili mfululizo hivi sasa na kati ya mwaka 1995 na 2000 alikuwa mbmunge wa viti maalumu.

Akitangaza nia yake hiyo mbele ya waandishi wa habari wa nyumbani kwake Wilolesi mjini hapa leo Mwakalebela ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Michezo ya VANNEDRICK (T) Ltd alisema anataka kutumia uzoefu alioupata kwenye medani ya soka kuwatumikia wananchi wa jimbo la Iringa.

Mwakalebela aliyezaliwa miaka 40 iliyopita, alisema ni haki yake kikatiba kuchagua na kuchaguliwa kuwaongoza watanzania wenzake bila kujali dini wala makabila yao.

”Nikiwa mwanCCM, mzaliwa wa Iringa ninawiwa kuchangia harakati za maendeleo za jimbo hili kwa kuomba uwakilishi kupitia CCM, na uwezo namaarifa ya kubonyue kitufe kwa ajili ya maendeleo ya jimbo la Iringa ninayo kwa kushirikiana na wakazi wa jimbo la Iringa na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi” alisema.

Alisema endepo atafanikiwa kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea wake na hatimaye kuwa Mbunge wa jimbo hilo, atatumia maarifa yake yote kuhakikisha jimbo la Iringa linakuwa na vipaumbele vitakavyosaidia kuwaondolea wananchi wake umasikini.

Mwakalebela ambaye ni msomi mwenye shahada ya pili katika masuala ya utawala wa rasilimali watu alisema katika uchaguzi huo kauli mbiu yake itakuwa Maendeleo Kwanza itakayokwenda sambamba na kauli mbiu ya kitaifa ya Kilimo Kwanza.

Alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuvutwa na nia njema ya kuwatumikia watanzania akiwa mbunge wa jimbo la Iringa Mjini ambapo atashirikiana na taasisi mbalimbali, NGOs na CBOs.

Alisema kuwa kutokana na kufanya kazi katika sehemu mbalimbali na kuona utendaji wake una mafanikio makubwa, ari hiyo imemvuta zaidi kulitumikia jimbo hilo na kuongeza kuwa uzoefu ambao ameuonesha katika sehemu anazozifanyia amependa kuutumia ili kushirikiana na wananchi wa jimbo la Iringa kuleta maendeleo.

Alisema kuwa ili maendeleo yenye mwelekeo yapatikane jimboni humo makundi yote ya wazee, vijana, akina mama na watoto yanatakiwa yaunganishwe na kiongozi mwenye mtazamo yakinifu utakao kuwa na manufaa kwa jamii nzima bila kubagua kundi fulani, na kuongeza kuwa kwa kulizingatia hilo ameona kuwa anaweza kuwa msaada kwa wana Iringa endapo watamchagua.

Aliongeza kuwa mkoa wa Iringa unazo rasilimali nyingi pia unavivutio vingi vya utalii na kuwa kama vitatangazwa na kukaribisha wawekezaji wengi ambapo kwa kushirikiana na wakulima, wafanyabiashara, vikundi mbalimbali vya wazee, akina mama, walemavu, vijana pamoja na wajasiliamali, wataunganishwa katika mtandao wenye muhimili wenye mafanikio makubwa kwao na kwa taifa.

Alisema atatumia michezo kama 'working tool' yake ya kuyaunganisha makundi yote ya wazee, akina mama, vijana, watoto na watu wa rika zote katika kuhamasisha maendeleo na akongeza kwamba wazee wasiposhirikishwa katika shughuli za kuongoza nchi na kuleta maendeleo mafanikio yatakuwa ni mabaya.

Alisema kuwa uzoefu mkubwa wa kuwaongoza wananchi ameupata katika sehemu mbalimbali ambazo amefanya kazi ikiwa ni pamoja na nchini Botswana alikokuwa akifanya kazi kama mshauri wa masuala mbalimbali yakiwemo yakiuchumi, kiwanda cha sukari cha Mtibwa na sasa kwa muda wa miaka minne amekuwa ni Katibu wa TFF.

Alisema kuwa uzoefu huo pamoja na kujuana na watu kutoka mashirika, watu pamoja na taasisi mbalimbali hivyo vyote vitamsaidia kuhakikisha wananchi wa jimbo la Iringa wanashirikiana na kuwa kitu kimoja katika kupambana na umasikini ili kuwa na mwelekeo mmoja wa kunyanyua uchumi.

Mwakalebela ametangaza nia yake akiwa pamoja nawanafamilia wenzake ambapo baba yake Mzee Wilfred Makalebela alisema ametoa baraka zote kwa mwanae katika nia yake ya kugombea ubunge ili ashirikiane na wananchi wa jimbo la Iringa kuleta maendeleo endelevu.

Alisema kuwa amepata elimu katika sekondari ya Highlands kidato cha kwanza hadi Nne na sekondari ya Tosamaganga kidato cha tano hadi sita na baada ya kumaliza shahada yake katika Chuo Kikuu cha Mzumbe alifundisha sekondari ya Ufundi ya Ruaha na kwenda kufanya kazi Botswana kwa miaka sita.

Mwisho;
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA