Home » » WAZIRI WASIRA UPO? MAREHEMU IRINGA WAGAWIWA MBOLEA YA RUZUKU ...

WAZIRI WASIRA UPO? MAREHEMU IRINGA WAGAWIWA MBOLEA YA RUZUKU ...

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Friday, April 16, 2010 | 10:13 AM

PAMOJA na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na baraza lake la mawaziri akiwemo waziri wa kilimo,chakula na ushirika Mh.Stephen Wasira kuweka mikakati mizuri ya kuboresha kilimo hapa nchini kwa kutoa pembejeo kwa njia ya vocha za ruzuku kwa wakulima wa hali ya chini ,jitihada hizo zimeonyesha kukwamishwa katika kijiji cha Kibena kata ya Ifunda wilaya ya Iringa vijijini baada uchunguzi wa mtandao huu wa gazeti la Tanzania Daima na kipindi cha morning Talk umebaini ufisadi mkubwa wa pembejeo hizo baada ya viongozi wa serikali ya kijiji kufoji majina ya walengwa na kuweka majina ya watu waliokufa zaidi ya mwaka mmoja uliopita .

Uchunguzi wa kina uliofanywa na mtandao huu kwa ufadhili wa kipindi cha Morning Talk cha Radio Ebony Fm ya mkoani Iringa umeweza kubaini udhadhilifu mkubwa wa pembejeo hizo za kilimo katika kijiji hicho.

Mpango huo wa ugawaji wa pembejeo kupitia vocha za ruzuku ya serikali pamoja na kulalamikiwa mbele ya makamu wa Rais Dk.Ali Mohamed Shein wakati wa ziara yake mkoani Iringa hivi karibuni na kukiwa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa wahusika wa ufujaji wa vocha hizo za pembejeo za ruzuku bado madai ya wakulima kuorodheshwa majina yao bila kupewa pembejeo hizi ni mengi zaidi.

Katika uchunguzi huo wa kina uliofanywa katika kijiji cha Kibena umebaini katika kijiji hicho jumla ya watu 46 waliokuwemo katika orodha ya watu waliotakiwa kupewa pembejeo hizo za ruzuku .

Baadhi ya wajane katika kijiji hicho akiwemo Maria Fuime (70) alisema kuwa kwa upande wake ameshangazwa kusikia katika mkutano wa hadhara jina la marehemu mume wake Yohana Mteve lilasomwa na lipo katika orodha ya wananchi walionufaika na mpango huo wa pembejeo za ruzuku wakati mume wake huyo alifariki dunia toka desemba 2007 na kuzikwa katika kijiji hicho.

Alisema kuwa uongozi wa serikali ya kijiji hicho ukusanya majina ya marehemu zaidi ya 10 na kuyaandika katika ripoti yao ili kuonyesha kuwa pembejeo hizo zilisambazwa kwa usahihi huku walengwa karibu wote wakiwa hawajanufaika na zoezi hilo na hata baadhi ya waliopata ni wale walioambulia mbolea mfuko moja ama miwili pekee.

“Kaburi la mume wangu hili hapa mbele ya nyumba sasa inashangaza kuona jina lake linaendelea kutumika kuibia serikali huku serikali yenyewe ikishindwa kuchukua hatua…. Shamba langu mimi mahindi yamekosa kustawi vizuri kutokana na kukosa mbolea ila watu watu wanageuza wafu kama sehemu ya mitaji yao ”

Mbali ya mjane huyo pia watoto wa marehemu Yohana Mtweve Christina na Shabu wameomba serikali kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika kufanya udanganyifu wa pembejeo hizo na kuwa kilichofanywa na viongozi hao wa kijiji ni kuzunguka katika maeneo ya makaburi na kuandika majina ya watu waliokufa na baadhi yao wakiwemo watoto wadogo na kuyaweka katika orodha ya wananchi walionufaika na mpango huo wa vocha za ruzuku kumbe ni wizi mtupu.

Hata hivyo walisema suala hilo limelalamikiwa kwa viongozi mbali mbali za kata hiyo ila hakuna hatua ilioyochukuliwa dhidi ya wahusika hao.

Mmoja kati ya vibarua katika duka la wakala Ngwale ambaye alipewa jukumu ya kuuza vocha hizo kwa wakulima Abyuta Sanga alisema kuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Gaspar Mleleu na afisa mtendaji wa kijiji Laurian Kidava walikuwa wakitoa maelekezo ya watu wa kupewa pembejeo na baadhi ya watu hao ni wageni wa kijiji hicho ila kutokana na wao kama viongozi kuagiza hakuweza kupinga.

Katibu kata wa CCM kata ya Ifunda Juma Habibu alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa malalamiko juu ya zoezi hilo viongozi wa CCM kata walikutana katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM kikao kilichofanyika Machi 11 mwaka huu chini ya wajumbe watano akiwemo Aujelus Lawa (mwenyekiti CCM kata) , yeye mwenyewe Juma Habibu kama katibu kata CCM, Godson Lyandala (katibu uchumi na fedha kata –CCM) ,Vumila Mwenda (mjumbe) na Kalaleta Fuime (diwani wa viti maalum).

Alisema katika kikao hicho ambacho agenda kubwa ilikuwa ni kujadili tatizo la usambazaji wa mbolea za ruzuku katika kijiji cha Kibena msimu wa mwaka 2009/2010 ambapo walibaini ufisadi huo wa mbolea hiyo.

Hata hivyo alisema mwenyekiti wa kijiji na afisa mtendaji wa kijiji hicho ndio waliohusika na wizi huo wa pembejeo na kuwa baada ya suala hilo kujulikana mtendaji amekimbia kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kitongoji cha KItasengwe katika kijiji hicho cha Kibena Lazaro Kitwange aliiomba serikali kuwakamata viongozi hao na kuwachukulia hatua za kisheria kwani wakulima wote wa kijiji hicho hawajanufaika na mpango huo zaidi ya viongozi hao ambao wamenunua gari la kutembelea na pikipiki kwa fedha za mbolea hiyo ya wizi.

Hata hivyo alisema wananchi wamekuwa wakishindwa kulalamika katika mikutano kutoana na ubabe wa viongozi hao na mwananchi akilalamika hutishwa .

Kwa upande wao viongozi hao hawakuweza kupatikana kuzungumza na mwandishi wa habari hizi japo mwenyekiti wa kijijiji hicho alipopigiwa simu alikataa kueleza chochote kwa madai hana hakika kama kuna ugawaji mbaya wa pembejeo katika kijiji chake.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Fundi Mihayo alikili kuwepo kwa tatizo ya ubadhilifu wa pembejeo katika kijiji hicho na vijiji vingine na kuwa tume inaundwa ili ku chunguzi suala hilo.

Pia alipongeza jitihada za mwandishi wa habari hizi na kwa kufichua ufisadi huo na kuomba vyombo vingine kujitokeza kupambana na ufisadi zaidi.

Kwani alisema lengo la serikali katika mpango huo lilikuwa ni nzuri lenye lengo la kuwakomboa wakulima na kuongeza kasi ya uzalishaji ila baadhi ya watu wachache wamejipanga kukwamisha zoezi hilo .

Uchunguzi wa gazeti hilo katika kijiji hicho majina ya marehemu walioorodheshwa kupewa pembejeo ni pamoja na Norbat Mbinduka, Lameck Ngweta, Simon Mbembati, Masud Mahondo, Abasi Ngweta, Gailan Nzunda, John Kitwange, Martin Lumato , Pasumile Lumato, Yohana Mtweve na Msikose Kihombo .

Huku watoto na wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari ambao majina yao yanaonyesha kupewa pembejeo hizo ni pamoja na Faiza Kilowoko, Rejina Msita anayesoma sekondari ya Lyasa kata ya Ifunda,Hassan Ngulo( Mwembetogwa sekondari),Maria Lalisa (Lyasa sekondari) ,Ano Mgaya, Filbert Chengula(Kawawa sekondari ) Ezekia Kalinga na Aron Chengula ambao ni watoto katika kijiji hicho pia yapo majina ya watu 15 kutoka nje ya kijiji na wilaya hiyo ambao wameorodheshwa katika wanakijiji walionufaika na pembejeo hizo nakala ya majina yote ipo .

......Itaendelea wiki ijayo......
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA