Home » » WANANCHI MAFINGA WALIPIA VIWANJA HEWA....

WANANCHI MAFINGA WALIPIA VIWANJA HEWA....

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Monday, April 19, 2010 | 9:38 AM

WANANCHI zaidi ya 700 katika mji wa Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamedai Halmashauri yao ilitumia jina la Rais Jakaya Kikwete kutapeliwa fedha zao za viwanja walivyo lipia toka mwaka 2006 na 2007 katika halmashauri ya wilaya hiyo kitengo cha ardhi bila kuonyeshwa viwanja husika Tanzania daima limebaini.

Katika uchunguzi wa kina uliofanywa na mtandao huu kwa kushirikiana na kipindi cha Morning Talk cha Radio Ebony Fm ,umebaini kuwepo kwa madai hayo ambayo yamepelekea wananchi hao kumwomba Rais Kikwete kuwasaidia kupata haki yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mtandao huu wananchi hao akiwemo Janeth Mtagawa , Salum Kalinga na mjane Anna Sanga walisema kuwa uongozi wa halmashauri hiyo ulitangaza zoezi la upimaji wa viwanja kwa gharama nafuu kwa wakazi wa mji huo kwa zaidi ya miaka miwili sasa wamelipia zoezi hilo ila hakuna kiwanja wanachopimiwa.

Alisema mjane huyo Anna Sanga kuwa kwa upande wake mbali ya kuomba kupimiwa kiwanja hicho bado alikuwa na ardhi yake yenye miti ikiwa na ukubwa wa zaidi ya hekari 10 aliyoachiwa na marehemu mumewe ila ardhi hiyo imechukuliwa na halmashauri bila kulipwa fidia yoyote.

“Kweli huu ni utapeli wa hali ya juu kwani mimi hapa nilipo ni mjane na wao serikali walikuja na kupokonya eneo langu kwa madai kuwa ningelipwa fidia ili eneo hilo litumike kuwagawia wananchi wengine viwanja vya makazi ….japo na mimi walinitaka nilipie fedha ya upimaji wa kiwanja ambacho nilikuwa nikiomba kwa ajili ya kujenga nyumba …..ila ukweli hadi sasa toka nimelipia ni zaidi ya mwaka mmoja sijaonyeshwa kiwanja wala kulipwa fidia ya ardhi yangu …sasa huu si utapeli jamani” alihoji mjane huyo huku akibubujikwa machozi.

Mjane huyo alisema kuwa alilipia kiasi cha shilingi 80,000 kwa ajili ya kupata kiwanja katika eneo la Changarawe mjini Mafinga ambako zoezi hilo la upimaji viwanja lilipaswa kufanyika kati ya mwaka 2006 na 2007 japo hadi sasa hakuna mwananchi aliyeonyeshwa kiwanja chake.

Hivyo alimwomba Rais Kikwete kuweza kusaidia wananchi hao kupata haki zao kutokana na aliyekuwa afisa ardhi wa wilaya hiyo ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi ,wakati akihamasisha wananchi kujitokeza kulipia zoezi hilo la upimaji alikuwa akidai kuwa zoezi hilo linafanywa kwa agizo la Rais Kikwete katika kuboresha miji ili kufikia malengo ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.

Kwa upande Sanga na Mtagawa walisema kuwa wamefuatilia suala hilo la kutapeliwa fedha zao katika ofisi ya ardhi ,ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mufindi na ofisi ya mkurugenzi mtendaji bila mafanikio zaidi ya kuendelea kuzungushwa bila kuonyeshwa viwanja vyao.


Hata hivyo walisema kuwa ni vema mkuu wa wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu na mkuu wa mkoa wa Iringa Mohamed Abdulaziz kuingilia kati suala hilo ikiwa ni pamoja na kukutana na wananchi waliolipia gharama za upimaji wa viwanja na wale wanaodai fidia ya ardhi zao kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika vinginevyo hasira zao wataelekeza kwa chama tawala .

Wananchi hao walisema kuwa tataizo linalokwamisha zoezi hilo kukamilika kwa muda uliopangwa ni rushwa katika ofisi hiyo ya ardhi jambo ambalo linapelekea matajiri kuendelea kupewa ardhi huku masikini wakiendelea kulipia bila kupewa viwanja wala kuonyeshwa.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Limbakisye Shimwela akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Dar es Salaam kuhusiana na malalamiko hayo ya wananchi alikili kuwepo kwa tatizo hilo la wananchi kulipia viwanja bila kugawiwa na kuwa limesababishwa na mabadiliko ya sheria ya umilikishaji ardhi .

Alisema kuwa awali wananchi walikuwa wakigharamia gharama za upimaji wa viwanja na masuala ya fidia yalikuwa yakifanywa na wananchi wenyewe ila kwa sasa kutokana na mabadiliko hayo ya sheria ya ardhi halmashauri ndiyo yenye jukumu ya kulipia gharama zote za fidia .


Mkurugenzi huyo alisema kuwa kutokana na halmashauri hiyo lengo la halmashauri hiyo kupokea fedha hizo kwa wananchi ni kutaka kuwapimia viwanja ila kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo suala hilo likawa gumu kutekeleza japo kwa sasa wanafanya utaratibu wa kukamilisha fidia na ndani ya mwezi huu wananchi waliolipia viwanja wataanza kupewa .

“Mimi kwa sasa nipo jijini Dar es Salaam katika kikao cha bajeti ….ila nimeagiza wenzangu huko kuendelea na mchakato wa kulipa fidia kwa wale wote ambao walikuwa wakidai ili zoezi la upimaji viwanja liweze kufanyika ndani ya mwezi huu ….napenda kuwaomba radhi wananchi wote wenye malalamiko juu ya suala hili”alisema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo afisa ardhi wa halmashauri hiyo Ali Kidwaka alisema kuwa si kweli kama ofisi yake ilifanya utapeli kwa wananchi hao kama wanavyodai na kuwa lengo la halmashauri lilikuwa ni kutoka viwanja kwa wananchi 300 ila idadi ya wananchi waliojitokeza ilikuwa ni zaidi ya wananchi 1100 ndio waliorodhehwa na kulipia gharama za upimaji viwanja.

Alisema kuwa wananchi walitangaziwa kugawiwa viwanja mwaka 2007 na aliyekuwa afisa ardhi kwa wakati huo ambaye alisimamishwa kwa matatizo kabla ya yeye kuteuliwa na katibu mkuu wa TAMISEMI mapema mwaka huu japo yapo mazuri mengi yaliyofanywa na mtangulizi wake na yapo mabaya pia ambayo yote ameyapokea.

Kidwaka alisema kuwa hadi hivi sasa wananchi zaidi ya 700 ndio wanaodai viwanja vyao baada ya kulipia na mchakato wa kukamilisha fidia unaendelea japo gharama za upimaji viwanja zilizotolewa kiasi cha shilingi 80,000 na 60,000 hazilingani na fidia ambazo wenye mali wanadai katika maeneo hayo.

Alisema gharama za upamaji viwanja zilizopokelewa kutoka kwa wananchi hao zaidi ya 1000 ni zaidi ya milioni 60 ila gharama za ulipaji fidia ambazo halmashauri inapashwa kulipia ni zaidi ya fedha hizo na kuwa zoezi hilo limeanza kufanyika ili kuwawezesha wananchi hao kupimiwa viwanja vyao kama walivyolipia.

MWISHO
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA