Home » » TRAFIC MAKAMBAKO WAWAKWAMISHA ABIRIA WA BASI LA SABCO TOKA RUVUMA KWENDA DAR ES SALAAM KUONDOKA

TRAFIC MAKAMBAKO WAWAKWAMISHA ABIRIA WA BASI LA SABCO TOKA RUVUMA KWENDA DAR ES SALAAM KUONDOKA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Wednesday, March 31, 2010 | 2:22 AM


ASKARI wa usalama barabarani Makambako wilaya ya Njombe mkoani Iringa leo wamezuia basi la kampuni ya Sabco lililokuwa likitoka Ruvuma kwenda jijini Dar es Salam lenye namba za usajili T 418 ATH Scania kuendelea na safari kutokana na uchakavu wa taili za basi hilo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi eneo la stendi ya Makambako ambapo abiria hao wamekwama ,baadhi ya abiria wa basi hilo akiwemo Christina Komba na John Haule walisema kuwa wameendelea kukwama katika eneo hilo baada ya askari wa usalama barabarani kuchomoa namba za gari hilo hadi mmiliki wa basi hilo atakapofunga taili mpya.


Alisema Komba kuwa pamoja na wao kama abiria kupongeza hatua ya jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani mkoani Iringa kwa kusimamia vizuri sheria kwa lengo la kunusuri maisha ya abiria ila bado wanaulalamikia uongozi wa kampuni hiyo kwa kushindwa kuwabadilishia basi jingine ili wao waweze kuendelea na safari.

Alisema kuwa baadhi ya abiria katika basi hilo ni wale wanaokwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matatizo mbali mbali wakiwemo wagonjwa ambao wanakwenda katika hospitali ya Taifa kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya kiafya.

Hivyo hatua ya uongozi wa kampuni hiyo kuwakimbia abiria na kuwatwelekeza katika stendio hiyo bila kuwatafutia usafiri mwingine ni moja ya unyanyasaji mkubwa ambao wameliomba jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani na viongozi wa Sumatra mkoa wa Iringa kuweza kuchukua hatua zaidi kwa kampuni hiyo.

Aidha kwa upande wake Haule alisema kuwa bado askari wa usalama barabarani katika mkoa wa Ruvuma na stendi kuu ya Njombe ambako basi hilo limepita wanapaswa kuchunguzwa zaidi kutokana na kuliacha basi hilo kupita bila kuliona tatizo hilo kubwa la uchakavu wa mataili yake.

"Tunashindwa kujua utendaji kazi wa askari wa usalama barabarani katika maeneo ambayo basi hili limepita na askari wamekagua na kutoona tatizo ...sasa tunapokamatwa hapa Makambako kuwa taili ni kipara tunajiuliza kama Makambako wameona tatizo hilo na askari hao wameruhusu ni hatua gani zinachukuliwa kwa askari walioruhusu basi hilo kupita" alihoji abiria huyo.

Kwa upande wake mmoja kati ya wafanyakazi wa basi hilo ambaye hata hivyo hakupenda kutaja jina lake kwa kuhofia ajira yake alisema kuwa matatizo kama hayo yanachangiwa na mmiliki mwenyewe ambaye amekuwa akiliona tatizo hilo na kutolifanyia kazi zaidi ya kungojea faida pekee.

Hivyo alisema bado kuna uwezekano mkubwa wa basi hilo kuendelea kukaa katika stendi ya Makambako bila tatizo hilo kutafutiwa ufumbuzi kutokana na wao kutokuwa na uwezo wa kununua mataili hiyo mawili ambayo yanagharimu zaidi ya shilingi 700,000

Pia alisema kuwa askari polisi wa mkoa wa Ruvuma na kituo cha stendi ya Njombe wanapaswa kuchukulia hatua kwa kuruhusu basi hilo kuendelea na safari pamoja na kuliona kosa hilo.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa (RTO) Kedmund Mnubi alimweleza mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kuwa kukamatwa kwa basi hilo ni moja kati ya utendaji kazi wa kikosi hicho .

Hivyo alisema kimsingi uchakavu wa taili mbili za nyuma upande wa kulia katika basi hilo ungeweza kusababisha maafa zaidi kwa abiria iwapo zingepasuka kutokana na uchakavu wake.


Mkuu huyo alipongeza utendaji kazi wa askari wake kituo cha Makambako kwa kubaini tatizo la kuzuia basi hilo na kuwa kwa sasa anafanya mawasiliano na RTO wa Ruvuma ili kujua hatua sababu ya askari wake kushindwa kuzuia basi hilo kutoka katika stendi kuu ya Songea kutokana na uchakavu huo wa taili.


Kuhusu askari wa stendi ya Njombe alisema kuwa pamoja na kuwa vipo vituo vya ukaguzi wa mabasi ya abiria ila bado anachunguza sababu za askari waliokuwepo stendi hapo kushindwa kuona tatizo hilo.

Mnubi alisema upo uwezekano mkubwa wa basi hilo kufutwa barabarani iwapo mmiliki wake atashindwa kutekeleza maagizo ya usalama barabarani katika kufunga taili mpya kwa mujibu wa sheria.

Itachapwa gazeti la Tanzania Daima kesho
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA