Home » » MAANDAMANO YA WAKULIMA WA CHAI LUPEMBE NJOMBE YAISHIA MIKONONI MWA POLISI

MAANDAMANO YA WAKULIMA WA CHAI LUPEMBE NJOMBE YAISHIA MIKONONI MWA POLISI

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Monday, March 22, 2010 | 5:36 AM


ZAIDI ya wakulima wa chai 60 kutoka tarafa ya Lupembe wilaya ya Njombe mkoani Iringa leo wamekwa chini ya ulinzi wa askari wa kutuliza ghasia (FFU)wakituhumiwa kutaka kufanya mauwaji ya watu 50 kama njia ya kushinikiza mwekezaji wa kiwanda cha Lupembe Tea Factory Nawab Mula kufungua kiwanda hicho .

Pamoja na wakulima hao kudaiwa kufanya maandamano yasiyo na kibali kwa kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 70 kutoka kijiji cha Lupembe hadi makao makuu ya wilaya hiyo kwa lengo la kukutana na mkuu wa wilaya ya Njombe Charles Gisuli bado jeshi la polisi lilifanikiwa kuzuia maandamano hayo na kupokonya simu zaidi ya 40 za waandamanaji hao kwa ajili ya kiusalama .

Mmoja kati ya askari wa FFU wilaya ya Njombe ambaye alishiriki kuwazuia waandamanaji hao ambaye hata hivyo hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji wa juu ya jeshi la Polisi alisema kuwa kukamatwa kwa wakulima hao ni kutokana na hatua yao ya kufanya maandamano yasiyo na kibali na kuwepo kwa taarifa ya wao kuja kufanya fujo na mauwaji katika ofisi ya mkuu wa wilaya.

Alisema askari huyo kuwa wasamaria wema kutoka Lupembe walituma ujumbe mfupi wa maneno katika simu ya mkononi wakieleza juu ya makusudi ya waandamanaji hao katika ofisi ya mkuu wa wilaya.

"Tulipokea meseji inayosema kuwa waandamanaji hao wamepanga kuja kufanya mauwaji ya watu 60 katika mji wa Njombe hasa ofisi ya serikali ... kutokana na hali hiyo sisi tulipewa maagizo na mkuu wa polisi wilaya (OCD) ili kwenda kunusuru hali hiyo huku tukiwa tumejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kupambana na wakulima hao"

Hata hivyo alisema baada ya kufika eneo la mto Ruhuji umbali wa mita kama 100 hivi kufika ofisi ya mkuu wa wilaya walifanikiwa kuzuia maandamano hayo na kuwapekua waandamanaji wote na kukutwa watupo hawana silaha yoyote kinyume na taarifa zilizofikishwa polisi.

Hivyo alisema kilichofanyika na kuchukua simu wa waandamanaji wote kwa muda na baada ya kuteuliwa wawakilishi wao kwa ajili ya kukutana na mkuu wa wilaya na kupewa majibu walirejeshewa simu zao na kuachiwa.

Kwa upande wao wakulima hao wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuachiwa huru na jeshi la Polisi walisema kuwa kukamatwa kwao kumetokana na njama zilizopangwa na kundi la pili linalopinga kiwanda hicho kufunguliwa ili wao waendelee kunufaika na usafirishaji wa chai ya wakulima kwenda Kiwanda cha Kibena Njombe alisema Charlesy Mgina .

Alisema kuwa awali mkuu wa mkoa wa Iringa Mohamed Abdulaziz katika kikao chake na wakulima wa chao pamoja na mwekezaji kilichofanyika tarehe 27 mwezi uliopita aliagiza kamati ya watu 6 iundwe ili kuamua mtu wa kuendesha kiwanda hicho kati ya mwekezaji na ushirika wa wakulima wa chai tarafa ya Lupembe (MVYULU) na majibu yalipaswa kutolewa tarehe 20 mwezi huu jambo ambalo halikufanyika hadi walipoamua kufuata majibu hayo makao makuu ya wilaya.

Hivyo alisema hatua ya wao kufanya maandamano hayo ilikuwa ni kutaka kujua majibu ya kamati hiyo ya mkuu wa mkoa ambayo imechelewa kutoa na kuomba uongozi wa wilaya kuwasiliana na mkuu wa mkoa ili kuruhusu kiwanda kifunguliwe kama ambavyo mahakama ya ardhi ambayo ilivyo agiza kiwanda hicho kifunguliwe toka septemba 27 mwaka jana amri ambayo haijatekelezwa.

Mgina alisema kuwa katika maandamano hayo wakulima hao waliongozwa na timu ya viongozi sita akiwemo Eliuta Mfugale , Nathan Hongoli , Michael Kiputa, Meshack Masasi na Lucy Nyarusi ambao walikutaka na mkuu wa wilaya na kuahidiwa kuwa suala hilo litatolewa maamuzi keshokutwa machi 24.

Viongozi wa waandamanaji hao Nathan Hongoli , Michael Kiputa na Lucy Nyarusi walisema kuwa mkuu wa wilaya ya Njombe ametumia busara kubwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo ambapo alifanya mawasiliano na mkuu wa mkoa na kuwataka wakulima hao kurejea kijijini hadi kesho ambapo mkuu wa mkoa atafika wilaya ya Njombe na kulitolea ufumbuzi suala hilo.

Pia walisema simu zote zilizochukuliwa na askari polisi zilirejeshwa na kuwa hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi kwa sasa zaidi ya kuwekwa chini ya ulinzi kwa masaa zaidi ya manne kituo cha polisi Njombe.

Aidha walisema kabla ya kukamatwa na polisi walivamiwa porini na kundi la vijana zaidi ya saba ambao waliziba barabara kwa magogo kama njia ya kuzuia maandamano hayo kuja mjini Njombe zoezi ambalo halikufanikiwa baada ya kupambana nao kwa zaidi ya nusu saa.

"Maandamano yetu tulianza majira ya saa 8 usiku na majira ya saa 11 alfajiri ndipo tulipovamiwa na kundi la vijana ambao wanadaiwa kutumiwa na wasafirishaji wa chai ili kukwamisha ufunguzi wa kiwanda hicho ...katika tukio hilo kioo cha gari kilivunjwa japo hakuna mtu aliyejeruhiwa "
Alisema Februali 27 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa tarafa ya Lupembe mkuu wa mkoa aliitisha mkutano wa viongozi wa vyama vya msingi vya wakulima hao na mwekezaji wa kiwanda hicho ili kuwapatanisha na baada ya kufikia muafaka walikubaliana kiwanda hicho kilichofungwa baada ya kufungwa kwa miaka miwili sasa .

Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo Edmund Urio aliwataka wakulima hao kuteua watu sita tu watakao kwenda kumuona mkuu wa wilaya ambao watafikisha ujumbe waliotaka kuupeleka na baada ya kuchaguana watu hao waliongozana na OCD Urio


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya njombe Bw. Charles Gishuli alikiri wakulima hao kukamatwa na polisi wakiwa njiani kuelekea ofisini kwake na kuongeza kuwa alipewa taarifa na mkuu wa polisi wa wilaya hiyo ambaye alimweleza kuwa wakulima hao hawakufuata taratibu za kuwaona viongozi wa serikali kama sheria zinavyoagiza.

“Lakini amenifahamisha kuwa baada ya kuwachunguza polisi ilibaini walifanya hivyo kwa kutokujua taratibu na kwamba maandamano yao yalikuwa ya amani na zaidi walichotaka kwangu ni kujua kwanini serikali iliahidi kufungua kiwanda Machi 20 lakini haikuwa hivyo pia walitaka kujua nini hatima ya chai yao inayomwagwa chini” alisema

Hata hivyo alisema baada ya kuwasiliana na mkuu wa mkoa alimjibu kuwa tarehe iliyokuwa imeahidiwa haikutekelezeka kwa kuwa alipata safari ghafula na kwamba amerudi juzi Jumapili na kuahidi kuwa atakutana na kamati ya watu 6 inayowakilisha wakulima hao pamoja na mwekezaji kesho (machi 23) ili kiwanda hicho kifunguliwe.

Kiwanda cha Lupembe Tea Factory kilichokuwa kikiendeshwa kwa ubia kati ya mwekezaji Dhow Merchantile na Chama kinachounganisha vyama 9 vya wakulima kiitwacho Muungano wa vyama vya wakulima Lupembe (MUVYULU) ambapo kwa pamoja waliunda kampuni ya Lupembe Tea Estates Ltd kiliingia mgogoro baada ya viongozi wa chama cha MUVYULU kuanzisha vurugu Agosti 1 mwaka juzi vurugu ambazo zilisababisha kiwanda kufungwa.

Kiwanda hicho kilikuwa kikinunua chai ya wakulima wadogowadogo wapatao 6,000 ambapo tangu kifungwe chai yao imekuwa ikimwagwa chini kutokana na kukosa mahala pengine pa kuuza chai yao hali inayokwamisha maisha yao kiuchumi.

Mwisho.

Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA