Home » » DR.SHEIN AMALIZA ZIARA YA KIKAZI KICHAMA ZAIDI ,AMPA TANO MBUNGE AMWEKA PABAYA MENEJA WA MAJI

DR.SHEIN AMALIZA ZIARA YA KIKAZI KICHAMA ZAIDI ,AMPA TANO MBUNGE AMWEKA PABAYA MENEJA WA MAJI

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Wednesday, March 17, 2010 | 2:47 PM


MAKAMU Rais Dr.Ali Mohamed Shein leo ametumia ziara yake Kilolo kumpigia debe mbunge huyo ambaye ana hali ngumu kisiasa katika jimbo hilo kutokana na mpinzani wake mkuu aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Venanci Mwamoto kupanga kurejea tena kutetea kiti chake.

Dr.Shein ambaye kabla ya kuanza kuwahutubia wananchi alijikuta akiachwa na viongozi pekee jukwaani baada ya wananchi kukimbia eneo la mkutano kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya dakika 15.

Pamoja na wananchi wachache kurejea katika eneo hilo la mkutano bado Dr.Shein aliweza kutumia muda mwingi kumpamba mbunge Msolla kuwa amefanikisha mradi wa maji Ilula huku wananchi wakipinga mbele yake kuwa hawadanganyiki na mradi huo ambao maji kwa mara ya kwanza yanatoka leo (jana) huku wiki mbili nzima mji mdogo wa Ilula ukiwa hauna maji kutokana na waendeshaji wa mradi huo kuelekeza nguvu yao kujaza tanki kwa ajili ya kuja kuonyesha show mbele ya kiongozi huyo wakati wa ufunguzi wa mradi.

Kutokana na hali hiyo ya udanganyifu wananchi hao walilazimika kumkataa meneja wa mradi wa maji Ilula (ILUWASSA) Edward Shelembi kuwa hawamtaki aotolewe katika nafasi hiyo kwa madai kuwa amekuwa akifanya usanii mwingi katika kutatua kero ya maji katika eneo hilo .

Wananchi hao walimweleza Dr.Shein kuwa kero kubwa katika eneo hilo ni kuhusu upatikanaji wa maji na kuwa kwa mara ya kwanza huduma hiyo ya maji wameanza kuipata leo(jana) huku wiki mbili nzima wamekuwa wakinunua maji kwa shilingi 500 kwa ndoo huku maji ya bomba yakifungwa kwa ajili ya kujaza tanki kwa ajili ya kuonyesha kwa Makamu huyo wa rais.

“Ukweli mheshimiwa Makamu wa Rais kwa mara ya kwanza maji tunaopata leo toka wiki mbili zilizopita wananchi tumekuwa tukitumia maji machafu yasiyo salama kwa afya zetu …sasa tunasema huyo meneja wa maji hatumtaki na ukiweza uondokea naye sasa”

Hivyo walisema kuwa meneja huyo wa mradi wa maji amekuwa akishindwa kusimamia mradi huo huku katibu tarafa ya Ilula Paschal Moto akiwaamusha usiku wa manane kwa ajili ya kwenda kuchimba mifereji ya kusambaza bomba za maji ambayo kutokana na ucheleweshaji wa uwekaji bomba mifereji hiyo imekuwa ikifukiliwa na udongo .

Wananchi hao walisema kuwa meneja huyo wa maji katika eneo hilo amekuwa akipelekea wananchi kupendelea kuibeza serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kuwa hazifanyi kazi kutokana na ubabaishaji mkubwa unaofanywa.

Hivyo walishauri kuwa ili mradi huo uweze kunufaisha wananchi ni vyema kumtoa meneja huyo na kumweka mtaalam zaidi mwenye elimu ya kusimamia maji badala ya huyo wa sasa.

Kwa upande wake katibu tarafa hiyo Motto na meneja huyo Shelembi wakijieleza mbele ya Makamu wa Rais walisema kuwa wanashangazwa na hatua ya wananchi kuwatupia lawama mbele yake.

Motto alisema kuwa yeye alikuwa akiwafuata wananchi usiku kwenda kufukua mitaro ya maji kutokana na mitaro hiyo kufukiwa na tope lililotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha baada ya meneja huyo kuchelewesha kuweka bomba.

Huku meneja Shelembi akijitetea mbele ya Dr.Shein kuwa si kweli kama yeye ni kikwazo katika mradi huo na kuomba msafara wa Makamu wa Rais kupitia ofisini kwake ama kutuma maofisa wake ili kuweza kuonyeshwa hujuma mbali mbali ambazo zimekuwa zikifanywa katika mradi huo.

"Mheshimiwa kiongozi kweli mimi nimekuwa nikijituma sana kukamilisha mradi huu ila kuna hujuma mbali mbali ambazo wananchi wamekuwa wakizifanya kutaka kukwamisha mradi huu ....hivi huwezi amani watu wamekuwa wakikata bomba na kuziba ili maji yasitoke na ushahidi huo ninao hata kama utatuma mtu kuja pale ofisini kuna vitu mbali mbali vilivyokutwa katika mradi huo ambavyo ni hujuma"


Shelembi alisema kwa upande wake amekuwa akijitahidi sana katika Utekelezaji wa maradi huo na pale aliposhindwa kuonekana kijijini hapo ni kutokana na kupata safari ya kikazi kwenda mkoani Morogoro.

Pamoja na wananchi hao kunyesha kutokuwa na imani na viongozi wao huku baadhi yao wakimtupia lawama mbunge wa jimbo hilo Prof.Msolla ambaye ni waziri wa mawasiliano ,sayansi na Teknolojia kuwa amekuwa akilalamikiwa mara kwa mara juu ya uzembe kero ya maji katika eneo hilo ,bado makmamu wa rais Dr.Shein aliweza kugeuza ziara hiyo ya kikazi mkoani Iringa kuwa ni ziara ya kampeni kwa CCM baada ya kuanza kwa kumpigia debe mbunge Msolla utaratibu ambao hajapata kutumia wilaya yoyote kati ya wilaya nne kati ya tano alizopata kufanya ziara mkoani Iringa.

Dr.Shein ambaye mwaka 2005 alipata kufiki katikia jimbo hilo la Kilolo na kufanya mkutano uliohudhuriwa na wanafunzi wengi ,mkutano uliokuwa maalum kwa ajili ya kumaliza mgawanyiko uliotokana na kura za maoni katika jimbo hilo kati ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Mwamoto na Prof.Msolla jana ameonyesha kugeuza uwanja huo wa shule ya sekondari Ilula kuwa ni uwanja wa Kampeni za CCM baada ya kuanza kuwashawishi wananchi kuendelea kumchagua mbunge Msolla.

“Ndugu zangu mwaka 2005 nilipata kufika katika jimbo hili kwa lengo la kumpigia kampeni Rais Jakaya Kikwete,mbunge Profesa Msolla na madiwani ….ila sasa nimekuja kwa ajili ya kuona maendeleo yaliyoletwa na mbunge wenu japo binafsi nimefurahishwa sana na jitihada za mbunge wenu na nawaombeni mzidi kujenga imani na mbunge wenu Msolla”

Kuhusu ombi la wananchi hao kutaka meneja wa maji kuondolewa alisema kuwa kwa upande wake amepokea malalamiko yao na kuwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kufanyia kazi suala hilo .

Hata hivyo moja kati ya mambo yanayoonyesha kuwa Makamu wa rais amepokelewa kichama na kufanya shughuli za kampeni zaidi katika jimbo hilo la Kilolo ni baada ya kumpa nafasi mbunge wa jimbo hilo Prof.Msolla ambaye pia ni mjumbe wa NEC kufunga mkutano huo kwa kujinadi zaidi ya dakika 20 katika jukwaa hilo lililopambwa na bendela za CCM huku akishindwa kujizuia kueleza yaliyo ndani ya moyo wake kuhusu mwelekeo wa hali ya kisiasa ndani ya CCM.


"Kweli mheshimiwa makamu wa Rais hali ya upinzani kutoka katika vyama vingi wilaya ya Kilolo hakuna wa kutisha ila upinzani mkubwa upo ndani ya CCM yenyewe ....wapo wana CCM ambao wanapinga kazi zote zinazofanywa na mimi mbunge badala ya kupongeza japo huu mimi ninapambana nao kimya kimya"

Dr.Shein amemaliza ziara yake ya kikazi mkoani Iringa jana kwa kumalizia katika jimbo hilo la Kilolo na leo asubuhi anataraji kufanya majumuisho ya ziara yake mjini Iringa.

MWISHO

Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA