Home » » WAZIRI BENDERA, NAYE AKERWA NA UJENZI WA MAGHALA NDANI YA UWANJA WA SAMORA IRINGA

WAZIRI BENDERA, NAYE AKERWA NA UJENZI WA MAGHALA NDANI YA UWANJA WA SAMORA IRINGA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Wednesday, February 24, 2010 | 3:07 AM

HATUA ya wamiliki wa Uwanja wa Samora mjini hapa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa kujenga maghala ya kuhifadhia chakula ndani ya uwanja huo imezidi kupokewa tofauti na viongozi wa serikali baada ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, kuwaunga mkono wadau wanaopinga jambo hilo.

Bendera ameungana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupinga ujenzi huo ndani ya uwanja huo pasipo kuwatumia wataalamu, ambapo alishauri CCM mkoa kuacha mara moja kufanya mambo kienyeji katika eneo hilo, ambalo litakuja kutoa madhara makubwa kwa taifa, japo walionyesha kumpuuza waziri mkuu baada ya kushindwa kuvunja maghala hayo, ambayo yameanza kubomoka.

Pamoja na waziri mkuu kupinga ujenzi huo, baadhi ya viongozi wengine waliofanya hivyo kwa nguvu zote hata kugombana na CCM ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Said na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Theresia Mmbando, ambaye alifikia hatua ya kukifikisha chama hicho mahakamani.

Katika kikao chake na wadau wa mchezo wa riadha Mkoa wa Iringa, kilichofanyika ukumbi wa Manispaa ya Iringa jana, wadau hao walihoji sababu ya CCM kuendelea kuharibu viwanja vya michezo kwa kuanzisha matumizi mengine nje ya ramani, huku serikali ikitaka kufufua michezo mbalimbali.

Walisema sehemu kubwa ya viwanja vya michezo vilivyo chini ya CCM vipo katika hali mbaya na kuwa hata jitihada za serikali iliyopo madarakani za kufufua michezo zinakwamishwa na wasimamizi wake wa ilani, kutokana na kuendelea kuvuruga viwanja vya michezo.

Hivyo, waliiomba serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, kuweka mkakati wa kulinda viwanja wa michezo, badala ya kuendelea kutenga bajeti ya michezo bila kuwepo miundombinu.

Kwa upande wake, Waziri Bendera alisema kuwa kamwe Tanzania haiwezi kupiga hatua katika michezo iwapo viwanja vitakuwa katika hali mbaya.

Alisema ni vema CCM kama wamiliki wa viwanja vya michezo kwa kushirikiana na wadau kuendelea kuviboresha ili kuwa katika hali nzuri na kuepusha matumizi yanayokwenda kinyume na taratibu za kimichezo.

Aidha, Bendera alimpongeza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa hatua yake ya kuandika waraka maalumu unaotaka viwanja vyote vya michezo kuheshimiwa.

KUMBUKA UNAWEZA KUSOMA HABARI HII NDANI YA GAZETI LA TANZANIA DAIMA LA ALHAMISI HII

Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA