Home » » MADEREVA SITA WA MABASI KUFIKISHWA MAHAKAMANI ,DEREVA WA KAMPUNI YA SUMRY HIGH CLASS ATOROKA ASAKWA NA POLISI

MADEREVA SITA WA MABASI KUFIKISHWA MAHAKAMANI ,DEREVA WA KAMPUNI YA SUMRY HIGH CLASS ATOROKA ASAKWA NA POLISI

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Friday, February 19, 2010 | 3:40 AM


SAKATA la abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea mikoa ya kusini na maeneo ya nje ya nchi za kusini mwa Tanzania kufanya fujo jana ,jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani mkoani Iringa limewakamata madereva sita na kumsaka dereva mmoja wa basi la Kampuni ya Sumry High Class Efrehem Mwakapalala.

Pia jeshi la polisi mkoani Iringa limeeleza kusikitishwa na hatua ya abiria hao kufanya fujo kama njia ya kupinga madereva hao kukamatwa na kuwaonya kuacha tabia ya kushabikia mwendo kasi unaofanywa na madereva na kuwa kufanya hivyo ni kosa .

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa (ACP)Evarist Mangalla alimweleza mwandishi wa habari hizi jana kuwa kutokana na vurugu hizo zilizotokana na madereva kuvunja ratiba ya Sumatra jumla ya madereva sita ndio waliokamatwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani kilichoongozwa na mkuu wa usalama barabarani mkoa (RTO) Kedmund Mnubi.

Aliwataja madereva waliokamatwa kuwa ni Kasim Siulanga wa basi la kampuni ya Sumry High Class lenye namba za usajili T 658 ABCT),Habibu Suleiman( kampuni ya New Force namba T 777 ADR),Kasim Mangalla (Abood lenye namba T 277 ATH),Omary Mohamed (Basi lenye namba T 447 AAZ kampuni ya Hood),Omary Ally ( Hood namba T 242 ARU) na Ibrahim Omary ( Happy National namba T 181 AQP) .

Hata hivyo alisema kuwa madereva wote waliokamatwa ni wale wa mabasi ya Tunduma na Kyela mkoani Mbeya na kuwa wanatuhumiwa kwa kuendesha mabasi yao kwa mwendo kasi kinyume ya ratiba ya Sumarta.

Kamanda huyo alisema kimsingi ratiba ilikuwa ikiwataka madereva hao kufika eneo la ukaguzi wa Magari (Check point ) la Igumbilo mjini Iringa majira ya saa 7.45 ila wao walifika saa 7.30 kwa pamoja katika eneo hilo jambo ambalo linaonyesha wazi mabasi hayo yalikuwa yakifukuzana toka yalikotoka .

Pia alisema jeshi la polisi linasikitishwa na hatua ya abiria kuunga mkono mwendo kasi unaofanywa na madereva hao japo polisi wanafanya kazi hiyo kwa ajili ya usalama wao.

Alisema hata fujo hizo ziliweza kuchochewa na madereva wenyewe ambao walishindwa kuondoa magari yao katika eneo hilo mara baada ya kuruhusiwa kuendelea na safari huku basi likiwa na dereva mmoja.

Alisema kuwa madereva hao ambao waliachiwa juzi kwa dhamana wanataraji kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kwa kosa hilo la kuendesha kwa mwendo kasi huku dereva wa Sumry yeye atafikishwa kwa makosa mawili likiwemo la kukimbia akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Kwa mujibu wa sheria ya sumatra ya mwaka 2007 kifungu namba 18 A,C inatoa adhabu ya faini shilingi 200,000 hadi 500,000 ama jela mwaka mmoja kwa dereva atakayebainika kuvunja ratiba ya Sumatra.
Habari hii itachapwa katika gazeti la Tanzania Daima
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA