Home » » MWAKALEBELA ALIVYOPANIA KUREJESHA HESHIMA YA SOKA IRINGA KUPITIA KOMBE LA KRISMASI NA MWAKA MPYA................

MWAKALEBELA ALIVYOPANIA KUREJESHA HESHIMA YA SOKA IRINGA KUPITIA KOMBE LA KRISMASI NA MWAKA MPYA................

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Sunday, January 17, 2010 | 1:23 AM


MASHINDANO ya kombe la Krismasi na Mwaka mpya Iringa ambayo yaliipa heshima kata ya Miyombini Kitanzini inayoongozwa nadiwani wake Grevas Kalolo kuwa bingwa ni mashindano ya kipekee yaliyoanzishwa na kudhaminiwa na katibu mkuu wa shirikisho ya Soka Tanzania (TFF) Frederick Lameck Mwakalebela kama hatua ya kuelekea katika jitihada za kufufua michezo mkoani Iringa.

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Iringa ni mmoja kati ya mikoa iliyosifika zaidi kati ya miaka nyuma kutokana na kuwa na timu zenye wachezaji bora na zilizokuwa zikitoa upinzani mkali katika ligi mbali mbali za kitaifa ikiwemo timu ya Lipuli FC ya Iringa mjini pamoja na timu ya Nazareth Njombe( watoto wa paroko) kutoka wilaya ya Njombe ambazo zote hizi zimekufa na kubaki majina pekee

Hivyo jitihada hizi kubwa za Mwakalebela katika kuwa kuwa na ndoto za kurejesha heshima ya mkoa katika soka zinapaswa kuungwa mkono na kupongezwa na kila mpenzi wa michezo mkoani Iringa .

Mwakalebela mwenye umri wa miaka 40 amezaliwa katika hospitali ya Kibena wilaya ya Njombe na elimu yake ya msingi ameipata Mwanza wakati elimu ya sekondari amesoma Highland Iringa mjini na makazi yake yakiwa Kihesa katika Manispaa ya Iringa na ni mdau mkubwa wa soka la Tanzania ambaye amepania kwa nguvu zote kurejesha heshima ya soka katika manispaa ya Iringa kwa kuanza kufufua timu zilizopo na kuzipa nguvu timu kongwe mjini Iringa.

Katika kuhakikisha mkakati huo na ndoto yake inafanikiwa Mwakalebela ameanza kuonyesha ukereketwa wake katika michezo ndani ya Manispaa ya Iringa kwa kuanzisha mashindano ya aina yake ya kombe la krismasi na mwaka mpya kwa vijana wote wa kata 14 za jimbo la iringa mjini kama njia ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho kikwete hasa katika sekta ya michezo .

Akielezea azma yake katika kuendelea michezo ndani ya Manispaa ya Iringa na mkoa mzima ,anasema kuwa mbali ya kusaidia mikoa mbali mbali kimichezo akiwa kama katibu wa TFF na mdau wa soka nchini amelazimika kurejea nyumbani Iringa kwa kuanzisha kombe hilo la Krismasi na Mwaka mpya ambalo kimsingi litakuwa likichezwa kila mwaka.

Mwakalebela anasema kuwa pamoja na mwaka huu fainali ya mashindano ya kombe hilo yameweza kumalizika baada ya sikukuu hizo mbili kupita kwa mwaka ujao ratiba ya fainali hiyo inakuwa ikifanyika sanjari na sikukuu ya Mwaka mpya ili kureta maana zaidi.

Aidha anasema kuwa katika Manispaa ya Iringa zipo timu zenye wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuchezea timu mbali mbali zilizopo katika ligi kuu ya Voda com japo kukosekana kwa msukumo wa kweli wa michezo kumepelekea wachezaji hao kuishia kucheza katika uwanja wa Samora pekee.

Hivyo anasema kuwa kuanzishwa kwa mashindano hayo kutasaidia kuifanya Manispaa ya Iringa kuwa kituo cha wachezaji bora na timu zenye uwezo mkubwa wa kufanya vyema katika mashindano mbali mbali .

Anasema kwa upande wake akiwa kama mdau wa soka na kiongozi wa TFF amefurahishwa zaidi ya ushindani mkubwa ambao vijana walionyesha katika mashindano hayo.

Hata hivyo anasema kuwa katika mashindano hayo ambayo Miyomboni Kitanzini inayoongozwa na diwani wake Grevas Kalolo iliweza kubeba ubingwa wa kombe pamoja na fedha kiasi cha shilingi 150,000 baada ya kuichapa timu ya Kihesa kwa mabao 2-1 ,kulikuwepo na mvutano mkubwa wa ushabiki wa timu hizo pamoja na ule wa kimchezo.

Kwani anasema kuwa timu hiyo ya Kihesa ambayo ilishika nafasi ya pili na kuondoka na zawadi ya kikombe kidogo na fedha shilingi 100,000 ni timu kutoka kata ambayo amezaliwa ,kata inayoongozwa na diwani Mussa Wanguvu .

Pia anasema mbali ya timu hizo kuonyesha upinzani mkali kama ule wa simba na Yanga kwa Tanzania bado timu nyingine zilizopata kushiriki katika mashindano hayo ikiwemo ya Kitwiru,Ruaha, Kwakilosa, Mivinjeni, Gangilonga, Ilala, Mkwawa , Makorongoni na Mshindo zote zinaweza kuendelea kufanya vyema kwa mkakati huoulioanzishwa na kuendeleza soka mkoa wa Iringa.

Anasema kuwa kupitia kampuni yake ya Vanedrick Tanzania (Ltd) ataendelea kudhamini kombe hilo la krismasi na Mwaka mpya katika Manispaa ya Iringa.

Mwakalebela anasema kuwa suala la michezo ni moja ya ajira nzuri ya vijana iwapo vijana hao watawezeshwa kuanzia ngazi ya chini kama ambavyo kampuni yake hiyo ilivyokusudia katika jimbo la Iringa mjini.

Anasema kuwa kuendesha michezo kuna gharama zake na kuwa lazima mdau wa kweli wa michezo kuepuka kufikiria juu ya gharama kubwa zinazotumika katika kuendeelea soka na badala yake kuangalia haja ya mbeleni ya vijana kuja kunufaika na michezo.

Anasema kuwa kupitia kampuni yake amewezakudhamini mashindano hayo kwa asilimia 100 na kuwa toka mwanzo wa mashindano hadi mwisho amepata kutumia zaidi ya shilingi milioni 15 fedha zilizotolewa na kampuni yake hiyo pamoja na rafiki zake ambao ni wakereketwa wa michezo katika mkoa wa Iringa.


Anasema fedha hizo ndizo zilizoweza kununua vifaa vya michezo pamoja na kuendesha mashindano hayo.
Mwakalebela anasema kuwa wapo baadhi ya wazee na vijana wa jimbo la Iringa ambao wameonyesha kuvutiwa zaidi na jitihada zake hizo katika kuupatia heshima mji na mkoa wa Iringa katika michezo ambao wamemwomba kuwa miongoni mwa wagombea ubunge jimbo hilo la Iringa mjini ushauri ambao ataufanyia kazi pindi muda wa kutangaza kugombea utakapofika.

Kwani anasema kuwa akiwa kama Raia wa Tanzania wenye uwezo wa kuchagua na kuchaguliwa anaamini sifa za kugombea anazo na ataheshimu mawazo ya wengi katika suala hilo .

Hata hivyo anasema kuwa kuanzisha mashindano hayo hakuna uhusiano wowote na yeye kugombea ubunge katika jimbo hilo japo amefanya hivyo kama mwendelezo wake katika kusaidia mikoa mbali mbali hapa nchini katika soka.

Hivyo alisema pamoja na kusaidia mikoa mingine kama Arusha ,Mbeya ,Morogoro bado ameona si busara kama mkoa wa Iringa ambako ni nyumbani kuendelea kuwa nyuma kimichezo wakati kiongozi mzuri ni yule anayeonyesha mfano na nyumbani kwake.

Akielezea kuhusu elimu yake anasema kuwa baada ya kumaliza elimu ya sekondari Highalnds alikwenda kujiunga na kidao cha sita katika shule ya wavulana Songea mkoani Ruvuma na baadae alijiunga na JKT Mafinga ,pia amepata kufundisha shule ya sekondari Ruaha kabla ya kujiunga na chuo cha Mzumbe kwa ajili ya kuchukua digrii ya kwanza ya utawala kabla ya kwenda Botswana na kusoma na kuja kurudi tena Mzumbe kuchukua Mstars ya utawala na kwenda Mtibwa Sugar kuanza ajira.

Hata hivyo anasema kwaka 2006 ndipo alipofanmikiwa kupata kazi TFF kama katibu na kuwa baada ya mkataba wake kumalizima wakati wowote kuanzia sasa hataomba tena na badala yake ataendelea kuwa mdau wa soka na kuelekea nguvu zote katika mkoa wa Iringa ili kuhakikisha hadhi yake katika soka inarejea.

Kwa upande wake chama cha mpira wa miguu mkoa wa Iringa (IRFA) kupitia katibu wake Eliud Mvella Wamahanji mbali ya kumpongeza Mwakalebela kwa kuutazama mkoa wa Iringa kisoka bado kimesema kuwa toka mkoa uanzi kupata wadhamini bado hakuna mdhamini aliyeweza kuufikia udhamini wa katibu mkuu huyo wa TFF katika jimbo la Iringa mjini.

Wamahanji anasema kuwa iwapo wadau wa soka na wadhamini kama Mwakalebela wataendelea kujitokeza katika mkoa wa Iringa upo uwezekano wa timu za Polisi,Lipuli ,Magereza na nyingine kuendelea kusonga mbele.

Bofya hapa
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA