Home » » SINA UGOMVI NA KILANGO -------SOPHIA SIMBA

SINA UGOMVI NA KILANGO -------SOPHIA SIMBA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Sunday, December 6, 2009 | 8:03 PM


*Simba Mimi na Anne Kilango ni pete na kidole sina ugomvi wowote

*Asema kuna kijikundi cha watu wasio zidi 20 wanaotumika kumpiga Rais Kikwete

*Sijawahi kusema harusi ya Anne Kilango na John Malecela ilifadhiliwa na mtu

*Atolea ufafanuzi jinsi ajali iliyosababisha vifo vya watoto watano ilivyotokea

Na Francis Godwin,Iringa

MWENYEKITI wa umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi Taifa (UWT) ambaye pia ni waziri wan chi ofisi ya Rais utawala bora mama Sophia Simba amesema hata siku moja hajawahi kumtuhumu mbunge wa jimbo la Same Mashariki Anne Kilango kuwa harusi yao ilifadhiliwa na mtu na kudai kuwa yeye hana ugomvi wowote na Kilango bali wao ni marafiki pete na kidole na kuwa vyombo vya habari ndivyo vyenye ugomvi na wao kwa kuwasemea uongo.

Pamoja na kueleza kuwa hajapata kuwa na ugomvi na Kilango pia amesema kuwa ndani ya CCM hakuna mpasuko wowote wala kundi linalompinga Rais Jakaya Kikwete isipo kuwa kuna kijikundi cha watu wasiozidi hata 20 ambacho kimekuwa kikimtumikia mmoja wa vigogo ambaye ana chuki binafsi na serikali ya Kikwete.

Waziri Simba aliyasema hayo jana katika ukumbi wa hoteli ya Ruaha mjini Iringa wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari katika katika mkutano wa pamoja na waandishi hao uliolenga kuelezea lengo la ziara yake mkoani Iringa na hali ilivyo sasa ndani ya UWT ,CCM na Serikali ya awamu ya nne.

Alisema kuwa vyombo vya habari zimekuwa zikiandika na kutangaza kuwa ndani ya UWT kuna malumbano yanaendelea huku baadhi ya vyombo zikidai kuwa yeye kama mwenyekiti na waziri wana ugomvi na mama Kilango jambo ambalo si la kweli na hata siku moja hajapata kugombana na mama Kilango.

Kwani alisema yeye na Kilango ni marafiki wa siku nyingi na ni makada wa CCM wazuri na hata watoto wake yeye na wale wa Kilango ni marafiki wakubwa hivyo hana uhakika kama kweli marafiki kama wao wanaweza kugombana kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari ambazo zimekuwa zikiandika.

“….Sina uhakika kama mimi na mama Kilango tuna ugomvi wowote …kwani mwenzangu ni mbunge tena wa jimbo na mimi ni mbunge wa viti maalum na waziri …..mbali ya hayo pia sisi ni marafiki toka utoto na hata watoto wetu ni marafiki wazuri ….sasa huu ugomvi wetu uko wapi….yawezekana zipo tofauti ndogo ndogo ambazo kimsingi si za Kilango wala Simba bali ni za chama ama serikali ila hatuwezi kusema ni ugomvi…nitaendelea kuongoza wizara yangu na UWT pamoja na kushirikiana na mama Kilango kama mbunge na mwanachama wa UWT hakuna mtu wa kuendelea kutuchonganisha…”

Alisema waziri Simba huku akionyesha tabasamu kwa waandishi wa habari na kuwa wapo baadhi ya watu wa za magharibi ambao wamekuwa wakitumia kijikundi cha baadhi ya watu pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kwa ajili ya kupandikiza chuki kwa watanzania dhidi ya serikali yao .

Hata hivyo alisema kuwa wao kama serikali wamekwisha baini njama hizo zinazofanywa na kijikundi hicho cha watu katika kuishambulia serikali pamoja na CCM na kuwa wale wote wanaotumika katika kikundi hicho wanafahamika na kiongozi wao japo hakuweza kumtaja ila aliwahakikishia waandishi kuwa yupo mfadhili wa kijikundi hicho na sio kwamba hafahamiki.

Pia alisema kuwa hivi karibuni kuna mmoja kati ya viongozi wa vyombo vya habari amepata kunukuliwa na baadhi ya vyombo hapa nchini kuwa vyombo vya habari zinanguvu kubwa na vinaweza kufanya chochote jambo ambalo alilikubali japo alionya kuwa vyombo vya habari zisitumike vibaya ili kuepusha madhara katika Taifa.

Kuhusu tuhuma za ufisadi na kasi ndogo ya serikali kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya Rushwa na Ufisadi alisema kuwa TAKUKURU imekuwa ikifanya kazi yake kwa kuzingatia misingi ya sheria na haiwezi kukurupuka kuwakamata watu bila kuwa na ushahidi.

“Nataka mkumbuke waandishi wa habari inaeleza wazi utendaji wa kazi na kuwa ufisadi wa kufikirika usio na ushahidi hatuna la kufanya dhidi yao kwani nchi yetu sin chi ya kidikteta….hatuwezi kuendesha nchi kwa tuhuma za kufikirika na watu kunyosheana vidole….serikali zote za ccm zimekuwa zikipinga ufisadi na hadi sasa kuna kesi 1578 zinazoendelea toka kesi 58 zilizokuwepo kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005 na kuwa kubwa hapa ni lazima watanzania kujichunguza kwani ufisadi upo ndani ya mioyo ya watu “

Aidha alisema kuwa UWT Taifa inaungana na katibu mkuu wa CCM Yusuph Makamba kwa ufafanuzi wake dhidi ya wale wote wanaojitokeza na kumpinga Rais Kikwete na kuwa kwa upande wao UWT wanaunga mkono kwa nguvu zote utendaji kazi wa CCM na serikali yake chini ya Rais Kikwete na wanaimani kubwa ushindi wake mwaka 2010 utakuwa ni zaidi ya ule wa mwaka 2005 na hao wanaozunguka kulisha umma uongo wataumbuka mbele ya safari .

Pia kuhusu malalamiko ya utendaji kazi wa nguvu unaotumiwa na TAKUKURU hasa mkoani Iringa, waziri Simba alisema hajapokea malalamiko yoyote na kuwa wale wote wanaoilalamikia taasisi hiyo kwa utendaji kazi wa nguvu ni vyema kupeleka malalamiko hayo makao makuu kwa maandishi ili yaweze kushughulikiwa.

Wakati huo huo Simba ametoa pole kwa ndugu wa familia ya watoto watano waliopoteza maisha kwa kugongwa na gari juzi majira ya asubuhi katika kijiji cha Molonga mpakani mwa wilaya ya Njombe na Makete .

Akitolea ufafanuzi juu ya ajali hiyo alisema kuwa pamoja na vyombo vya habari kuripoti kuwa msafara wake ndio ulipata ajali ili ukweli gari hilo halikuwepo katika msafara wake na wakati ajali hiyo inatokea majira ya saa 1 asubuhi yeye na msafara wake ndio walikuwa wakitoka mjini Iringa kwenda kijiji cha Wanging’ombe Njombe na wao wakiwa huko walipigiwa simu kuelezwa juu ya gari hilo lililokuwa na wajumbe kugonga watoto hao na kupelekea wao kusitisha ziara ya kwenda Njombe na kwenda kutoa pole kwa wakazi wa kijiji hicho cha Molonga.

MWISHO
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA