Home » » TANROADS YAJIPANGA KUMDANGANYA RAIS IRINGA

TANROADS YAJIPANGA KUMDANGANYA RAIS IRINGA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Sunday, October 25, 2009 | 5:15 AM

Na Francis Godwin,Iringa
WAKATI Rais Jakaya Kikwete kesho anataraji kuanza ziara yake siku nne katika wilaya za mkoa wa Iringa wakala wa barabara (TANROADs) mkoa wa Iringa lawamani kwa hatua yake ya kujindaa kumdanganya Rais baada ya kuzifanyia marekebisho makubwa barabara zote ambazo msafara wake utapia Tanzania daima limebaini.

Wananchi Kilolo wamwomba Mbunge wao Profesa Peter Msolla kurudia kufikisha kwa Rais kilio chao juu ya kucheleweshwa utekelezaji wake kama alivyoagiza wa kubadili matumizi ya gereza la Kihesa Mgagao kuwa shule ya sekondari.

Kutokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwepo kwa pili pili nyingi za usiku na mchana ambazo zinazofanywa na wakala huyo wa barabara mkoa wa Iringa katika kutengeneza barabara hizo ikiwa ni pamoja na kuziba mashimo mbali mbali yaliyokuwemo katika barabara kuu ya Iringa -Mbeya ambayo kwa wakati wote yalikuwa hayazibwi kwa madia ya kukosa bajeti.

Kutokana na undanganyifu huo unaofanywa na TANROADs mkoa wa Iringa katika barabara hizo baadhi ya wananchi na viongozi wa vyama vya upinzani mkoani hapa na baadhi ya wabunge wa CCM wameeleza kusikitishwa na utendaji kazi wa wakala huyo wa barabara mkoa wa Iringa kwa hatua yake ya kufanya kazi kwa ajili ya kufurahisha viongozi wa kitaifa pekee .

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema ) Mwigongo Kapwani mkoa wa Iringa ,baadhi ya madereva na wabunge wa CCM ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini walisema kuwa barabara hizo kwa muda mwingi zilikuwa katika hali mbaya na kuwa iwapo siku zote zingekuwa zinafanyiwa marekebisho pinda wananchi na wao kama viongozi wanapofikisha malalamiko yao katika ofisi za wakala huyo mkoa wa Iringa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa mkoa wa Iringa kuwa na barabara bora zaidi.

Alisema Kapwani kuwa TANROADs imekuwa ikifanya kazi kwa ajili ya kufurahisha wakubwa badala ya kutimiza wajibu wake na kuwa kama suala ni kutokuwa na bajeti ya kufanya hivyo iweje ndani ya wiki tatu hizi za maandalizi ya ziara ya Rais bajeti imepatikana na maeneo yote korofi kufanyiwa marekebisho .

Hivyo alisema kuwa ni vyema Rais kupitia ziara hii na jinsi ambavyo atakavyo shuhudia marekebisho hayo ya barabara kwa ajili yake kutoa onyo watendaji hao ili siku nyingine kutekeleza majukumu yao bila kusubiri ujio wa viongozi kama ilivyo sasa na wakati mwingine .

"Wananchi wamelalamika sana juu ya ubovu wa hizi barabara ila hakuna jitihada zozote zilizofanyika ....lakini sasa hivi kwa ajili mheshimiwa anakuja barabara zimetengenewa vya kutosha ....sasa tujiulize hawa jamaa wanafanya kazi hadi viongozi wakitaifa wafanye ziara katika maeneo yao ama wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwa kazi walizopewa? alihoji mwenyekiti huyo wa Chadema na kuwa TANROADs mkoa wa Iringa imekuwa ikifanya kazi kwa kusukumwa na sio kutimiza wajibu wake"

Wakati kwa upande wao madereva wa mabasi ya usafiri Kilolo na wale wa Mbeya wamempongeza Rais Kikwete kwa kufanya ziara ndani ya mkoa wa Iringa kwa kipindi hiki cha kuelekea masika kwani sehemu kubwa ya barabara ambazo zilikuwa zikiwapa hofu kubwa zimetengenewa hivyo kwa masika kwao ni mteremko.

Madereva hao John Kalinga (Kilolo) na Samson Sanga ( Mbeya) walisema kuwa barabara ya kutoka Iringa kwenda Kilolo ambayo kwa sasa imetengenewa ndani ya siku mbili hizi ilikuwa katika hali mbaya na kama isingefanyiwa matengenezo ingeweza kusumbua sana masika .

"Barabara ya Kilolo kwa sasa kama lami vile imetengenezwa vizuri kwa ajili ya ujio wa Rais .....ujue upo usemi usemao mgeni njoo wenyeji tupone hii ndiyo hali halisi ambayo imeonekana hapa Iringa sasa"

Bw. Sanga alisema kuwa barabara ya Iringa-Mbeya ambayo ni lami ilikuwa na mashimo mawimbi mengi sana kama maeneo ya Nyororo na Tangangozi ila kwa sasa imerekebishwa na kutosha pamoja na awali barabara hiyo kupigiwa kelele na madereva bila mafanikio .

Kwa upande wao baadhi ya wabunge ambao Rais Kikwete atatembelea wilaya zao wamesema kuwa wao wanapongeza sana Rais kwa ziara yake mkoani Iringa kwani ni moja ya mafanikio makubwa kwao na wananchi ambao watapata nafasi ya kukutana tena na kiongozi huyo wa kitaifa ila bado maendeleo ambayo yamejitokeza kwa sasa ni makubwa ambayo kwa ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Wabunge hao ambao kwa kiasi walitofautiana juu ya utendaji wa TANROADS mkoa wa Iringa walisema kuwa ni kweli kumekuwepo na hali ya kujisahau kwa meneja huyo wa TANROADs mkoa wa Iringa huku baadhi wakisifu utendaji kazi wake na kuwa amekuwa akikwamishwa na bajeti .

Hata hivyo wabunge hao walihoji sababu ya bajeti kubwa ambayo imetumika kwa sasa kutengeneza maeneo korofi ya barabara ambazo msafara wa Rais utapita kutumika sasa wakati maeneo hayo yalikuwa yakisumbua kwa muda mrefu.

Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kumpigia simu meneja wa TANROADS mkoa wa Iringa Paul Lyakurwa kwa ajili ya kupata ufafanuzi juu ya bajeti hiyo iliyotumika kufanya marekebisho barabara hizo hakuweza kupokea simu zaidi ya simu kuita kwa muda mwingi bila kupokelewa.

Hii ni mara ya pili kwa TANROADS mkoa wa Iringa kufanya udanganyifu kama huu pindi wanapofanya ziara ziongozi wa kitaifa mkoani hapa ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni wakati wa ziara ya waziri mkuu ambapo barabara pia zilifanyiwa marekebisho ikiwa ni pamoja na kutumia gharama kubwa kusafirisha watu katika magari ya kukodisha kutoka mjini Iringa kwenda Mazombe katika uzinduzi wa barabara ya TANZAM ambayo ilikuwa ikizinduliwa ukarabati wake na kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi na mkuu wa mkoa wa Iringa Mohamed Abdulaziz kwa vyombo vya habari Rais anataraji kuwasili mkoani hapa leo jioni ambapo atafungua maabara ya kisasa ya Dream Community of sant Egidio pamoja na kupokea taarifa ya wilaya ya Iringa.

Huku kesho atatembelea wilaya ya Kilolo kuzindua rasimi wilaya ya Kilolo pamoja na kufanya mkutano wa hadhara kabla ya kuelekea wilaya ya Iringa kukagua shamba la mifugo la Philips ,kufungua mafunzo ya vijana -ugani katika chuo cha maendeleo ya wananchi Iringa,wakati Octoba 28 ataanya ziara katika wilaya za Mufindi, Njombe na Makete kabla ya kuondoka mkoani hapa Octoba 29 kuelekea mkoa wa Mbeya.

Wakati huo huo waanchi wa Kata ya Ukumbi wamemwomba mbunge wao Prof .Msolla mbaye ni waziri wa mawasiliano Sayansi na Teknolojia kumkubusha Rais Kikwete kuhusu ucheleweshaji wa agizo lake alilolitoa wakati wa ziara yake mwaka jana kuwa gareza la kijiji cha Kihesa mgagao ambalo lilitumika kudai uhuru wa nchi mbali mbali za kusini mwa Afrika kufungwa na kugeuzwa shule ya sekondari .

Wananchi hao walimwomba mbunge huyo kufikisha ombi lao kwa mara nyingine na kueleza kiburi cha magereza mkoa wa Iringa pamoja na wizara ya mambo ya ndani kwa kushindwa kulifunga gereza hilo pmaoja na kuagizwa na Rais kutoka mwaka jana.

Wakati kwa upande wake mbunge Prof.Msolla aliwahakikishia wananchi hao kuwa suala hilo litafikishwa na wasio na hofu juu ya ombi hilo .

MWISHO
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA