Home » » RAIS JAKAYA KIKWETE AMALIZA ZIARA YAKE IRINGA

RAIS JAKAYA KIKWETE AMALIZA ZIARA YAKE IRINGA

Written By mzee wa matukiodaima habari bila uoga on Thursday, October 29, 2009 | 10:41 AM


Na Mwandishi Maalum, Makete, Iringa


Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana Jumatano, Oktoba 28, 2009, ametoa pikipiki aina ya Bajaj kwa mama mlemavu mmoja wa kijiji cha Lupalilo, Wilaya ya Makete, Mkoani Iringa, Bi. Sarah Mageni Sanga, ili kumsaidia usafiri.

Aidha, Rais Kikwete amemkabidhi mama huyo mjane risiti ya benki ya sh milioni mbili, ili zimsaidie katika kupanua duka lake dogo ili aweze kujipatia mahitaji yake ya maisha kwa uhakika zaidi. Fedha hizo zimewekwa kwenye akaunti yake katika Benki ya NMB.

Rais ametoa msaada huo kwa mama huyo wakati aliposimama kwenye kijiji hicho cha Lupalilo jioni ya leo, akiwa njiani kwenda mjini Makete, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mkoa wa Iringa. Ziara hiyo ya siku nne inamalizika kesho, Alhamisi, Oktoba 22, 2009.

Bi. Sanga ametokwa na machozi wakati anapokea msaada huo wa Rais mbele ya umati wa wanakijiji wenzake pamoja na watoto wake wawili akimwambia Rais Kikwete:

“Mungu akubariki na akujalie uendelee kuwa na moyo wa namna hii, ili uweze kuwasaidia wengine wenye ulemavu na wajane kama mimi.”

Mama huyo amefiwa na ndugu zake wote pamoja na mume wake, na hivyo pamoja na ulemavu wake wa miguu, anaishi na watoto wote wa ndugu zake ambao anawatunza.

Anaishi na watoto sita, wawili wa kwake na wanne wa marehemu ndugu zake. Mtoto wake wa kwanza yuko kidato cha tatu na wa pili yuko darasa la saba na wote wawili ni watoto wa kike.

Akimkabidhi mama huyo msaada huo mbele ya duka lake dogo, Rais Kikwete amesema kuwa alipata habari za mama huyo wiki iliyopita kwenye Kipindi Maalum kiitwacho Sharaja kwenye Televisheni ya Taifa ya TBC1.

“Niliangalia kipindi kile, nimwona mama huyu anatembea kwa kutambaa na nikasikia jinsi ndugu zake wote walivyofariki kwa maradhi haya, na nikawaelekeza washauri wangu kuniandalia msaada huu. Kwa kuwa nilijua nakuja huku, niliamua kuukadhi mimi mwenyewe kwako,”amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete pia amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Makete, Hawa Ng’humbi kuhakikisha ama anampatia mama huyo dereva wa kuendesha Bajaj hiyo, ama kuhakikisha kuwa mama huyo anafundishwa mwenye kuendesha.

Rais pia amemkabidhi Mkuu wa Wilaya huyo hati zote zinazokamilisha miliki ya Bajaj hiyo kwa Bi. Mageni ikiwamo risiti ya ununuzi, kadi ya pikipiki, usajili wa pikipiki hiyo, shughuli ambazo kwa jumla zimegharimu sh milioni nne.

Rais amezikahakiki hati zote kabla ya kuzikabidhi akiwachekesha wanakijiji kwa kusema: “Hebu kwanza nizihakiki hati hizi. Nchi yetu imekuwa na wajanja wengi ambao wanaweza kuja kukuletea matatizo baadaye.”

Kuhusu msaada wa sh milioni mbili, Rais amesema kuwa ametoa fedha hizo kumwezesha Bi. Sanga kupanua duka lake, kusomesha watoto wake, na kuendesha shughuli zake nyingine kwa uhakika zaidi.

“Na fedha hizi tayari zimewekwa kwenye akaunti yako ya Benki ya NMB, tawi la Mkwawa, mjini Makete,” amesema Rais Kikwete.


Mwisho
Share this article :

Post a Comment

 
blog designer Hoseaplatnum
Copyright © 2013. MATUKIO DAIMA - All Rights Reserved
Template Created by Hoseaplatnum Published by Francis Godwin
Proudly powered by FREE COMMUNITY MEDIA