Monday, December 26, 2011

MBUNGE FILIKUNJOMBE ATINGA GEREZANI KULA KRISMAS NA WAFUNGWA

Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kulia akishiriki chakula na wawekezaji wa kichina jana nyumbani kwake Ludewa

MBUNGE wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe ametembelea wafungwa wa gereza la Ludewa na kula nao chakula cha krismas pamoja na kuwapa misaada mbali mbali ikiwemo ya mashuka 200 na kuomba serikali kusaidia uboreshaji zaidi wa magereza hapa nchini.


Mbunge Filikunjombe alitoa msaada huo jumatatu ya Krismas na kuelezea ziara yake katika gereza hilo kuwa ni kutaka kuwafariji wafungwa na mahabusu wa gereza hilo kwa madai kuwa ni wapiga kura wake na wanahitaji kufarijiwa zaidi.

Akizungumza baada ya kutoka kula chakula na wafungwa na mahabusu hao ,mbunge Filikunjombe alisema kuwa zipo changamoto mbali mbali ambazo amepata kuziona katika gereza hilo kutoka kwa askari wake hadi wafungwa hasa katika uboreshaji wa nyumba za watumishi na gereza hilo zaidi.


Kwani alisema kuwa gereza lipo kwa ajili ya kila mmoja hata kama mbunge ama kiongozi wa serikalini na kuwa iwapo wao kama wabunge wasiposaidia kupigia kelele uboreshaji wa magereza nchini ipo siku na wao wanaweza kufikishwa hapo.


Hivyo alisema kuwa kwa upande wake mara baada ya kufika na kula chakula na wafungwa hao pia alipata nafasi ya kuwafariji na kuwasikiliza kero zao na kuwa moja kati ya kero ni juu ya kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi katika wilaya hiyo ya Ludewa ambayo mbali ya kuwa na jengo zuri la mahakama ila haina hakimu .


Aliiomba idara ya mahakama nchini kusaidia kupunguza msongamano wa mahabusu katika gereza hilo kwa kutatua tatizo la uhaba wa hakimu wa wilaya katika wilaya hiyo .

Kuhusu uchakavu wa nyumba za watumishi katika gereza hilo alisema kuwa nyumba nyingi za gereza hilo zimechakaa kutokana na kujengwa muda mrefu na tatizo la mchwa kuendelea kuwa kubwa eneo hilo.

Pia mbunge huyo aliahidi kuwasaidia TV wafungwa wa gereza hilo pamoja na radio ili kuweza kupata haki yao ya msingi ya kupata habari na kuweza kujifariji zaidi wakati wakitumikia adhabu yao.

Mbali ya misaada hiyo pia alikabidhi sabuni ,mafuta ,miswaki na dawa ya meno pamoja na kandambili kwa kila mfungwa na mahabusu wa gereza hilo huku akiwataka pindi wanapotoka gerezani kujiepusha na vitendo vya uharifu ambavyo vimewafikisha hapo.

Wakati huo huo mbunge huyo amepongeza ujio wa wawekezaji wa kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Ltd (TCMR) iliyoshinda zabuni ya kuwekeza katika migodi ya Mchumchuma na Liganga ambayo inakusudia kuanza utekelezaji wa awali wa uzalishaji wa makaa ya mawe, umeme na chuma katika migodi hiyo.

Wataalamu elekezi 20 wa TCMR ambayo ni kampuni mbia wa Shirika la China la Sichuan Hongda Corporation na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) wako wilayani hapa wakindelea na utafiti kabla ya miradi hiyo kuanza rasmi.

Mbunge wa Jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe amesema huu ni wakati muafaka kwa wenyeji na wawekezaji wengine kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuboresha huduma zitakazorahisha utekelezaji wa miradi hiyo.

“Huduma hizo ni pamoja na ujenzi wa nyumba, hoteli za kisasa, na maduka ya bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula,” alisema.

Watalaamu hao wote wachina ambao kati yao ni mmoja tu ndiye anayezungumza lugha ya kingereza wamebobea katika masuala ya umeme, viwanda, michoro, utafiti na ujenzi wa miradi hiyo.

Akizungumza na wanahabari katika eneo linalopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kuzalishia umeme la Nkomang’ombe huko Mchuchuma, Kiongozi wa watalaamu hao, Jiang Mzingnua alisema ujenzi wa mradhi huo wa umeme unatarajiwa kuanza mwaka mmoja na nusu baadaye, baada ya kukamilisha shughuli zote za kitafiti na michoro.

“Baada ya hapo kwa haraka sana tutaanza ujenzi wa mradi wa umeme utakaozalishwa kwa kutumia makaa ya mawe tutakayokuwa tukizalisha katika eneo hili la Mchuchuma,” alisema.

Alisema kwa kuanzia mradi wa umeme wa Mchuchuma utazalisha Megawati 600 ambazo kati yake 300 zitatumika kwa ajili ya kiwanda chao cha chuma kitakachojengwa katika mgodi wa Liganga.

Akiyataja baadhi ya faida watakazozipata wakazi wengi wa wilaya ya Ludewa kutokana na kuwepo kwa miradi hiyo ni pamoja na ajira na uboreshaji wa miundo mbinu na shughuli zingine za kimaendeleo.

Kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, kampuni hiyo inatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi 8,000 watakaotumiwa kufanya kazi mbalimbali za awali katika kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo.

Mzngnua aliyekuwa akiongea kwa lugha ya kichina huku Afisa wao mahusiano Tony Tan akitafsiri wa kingereza alisema kama ilivyo katika mkataba, kampuni hiyo itaboresha miundo mbinu ya barabara kwa kujenga barabara yenye ubora itakayounganisha eneo la Mchuchuma na Liganga.

Monday, December 12, 2011

BREAKINGNEWS...........MAMA AHOJI MAISHA BORA AKOSA JIBU AAMUA KUNYWA SUMU NA WATOTO WAKE

MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Kiponzelo katika wilaya ya Iringa vijijini Huruma Uhakula (27) anywesha sumu na pombe kienyeji watoto wake wawili nae anywa kwa lengo la kujiua kutokana na kile alichodai kuwa ni ugumu wa maisha kila kukicha.
Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Kiponzelo wilayani Iringa vijijini ambapo mwanamke huyo alidai kuwa aliamua kuchukua uamuzi wa kuiteketeza familia yake pamoja nay eye mwenyewe baada ya kuona hali ya maisha bora kwa kila mtanzani kwao inaendelea kuwa ni ndoto ya alinacha.
Mwanamke huyo mwenye familia ya watoto wanne aliwanywesha sumu watoto wawili wa kiume akiwemo motto Rashid Kibuga (7) na Eliya Kibuga (3) huku mtoto kichanga wa mwezi mmoja na dadake wa Gloria Kibuga (12) anayesoma darasa la nne wakisamehewa kunyweshwa sumu hiyo.
Akizungumza katika wodi namba 8 Hospital ya mkoa wa Iringa ambako amelazwa akiwa hoi mwanamke huyo Huruma alisema kuwa alilazimika kufanya unyama huo wa kunywa na kunywesha watoto hao sumu baada ya kuona hali ya maisha ikiendelea kuwa ngumu huku baba wa watoto hao kwa zaidi ya mwezi mmoja hajapata kuonekana nyumbani kuleta fedha za matumizi.
Bi Huruma alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya maisha kuendelea kuwa magumu alilazimika kutumia fedha yake ya akiba kiasi cha shilingi 10,000 ambacho kilikuwa kimebaki kununua pombe na sumu na kuamua kujiua na kuua watoto hao kama njia ya kukwepa maisha ya shida nyingi.
“Hapa nilipo nina moto wa mwezi mmoja na hawa wengine watatu ….ila hali ya maisha nyumbani ni mbaya zaidi na baba wa watoto hata hajali familia yake na mzigo wote nimekuwa nikibeba mimi ….hivyo niliamua kujiua mimi na hawa watoto wa kiume ambao nilijua wazi bila uwepo wangu wangekuja kupata tabu mbele ya safari”
Mtoto Gloria Kibuga akielezea mkasa huo alisema kuwa siku ya tukio mama yake alimtuma kwenda kununua sumu ya panya ya shilingi 7000 na pombe ya shilingi 2000 huku shilingi 1000 aliambiwa anunue viatu aina ya yebo yebo kama zawadi yake ya mwisho kutoka kwake ili aweze kuendelea kuvitumia kwenda shule.
“Mama alinituma kununua sumu hiyo ya panya hadi mara mbili nilienda mara ya kwanza akaniambia kuwa sumu niliyoileta haitoshi nikanunue tena kwa madai kuwa kuna panya mkubwa anataka kumuua ndani ya nyumba …..ila baada ya kununua sumu hiyo nilitumwa kununua pombe na baada ya hapo niliambiwa niende kulala kwa marafiki zangu kama kurudi nirudi kesho asubuhi”alisema mtoto Gloria.

Kuwa kwa kuwa muda wa kulala ulikuwa bado aliamua kwenda porini kutafuta matunda pori aina ya Mikusu kwa ajili ya kuja kula na wadogo zake na majira ya saa 12 za jioni alirejea nyumbani na kukuta mlango ukiwa wazi na baada ya kumwita mdogo wake Rashid alisikia akilia kwa sauti ya chini kuwa anakufa .
Alisema kuwa alipoingia ndani alikuta wadogo zake hao wakitokwa na povu mdomoni na mama yao akiwa hoi hali iliyomlazimu kukimbia kuita watu ambao walifika na kumkimbiza Hospital ya mkoa wa Iringa.
Baba wa familia hiyo Daniel Kibuga (37) alisema kuwa si kweli kama katika familia yake kuna maisha magumu kama mkeo anavyodai na kukiri kutoonekana nyumbani kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na kuwa mjini Iringa kikazi.
Kaimu mganga mfawidhi wa Hospital ya mkoa wa Iringa Dkt George Kabona amethibitisha kupokea wagonjwa hao watatu na kuwa hali zao kwa sasa zinaendelea vizuri baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na madaktari wa Hospital hiyo ya mkoa.

PATA HABARI MPYA HAPA

Sunday, December 11, 2011

BARAZA LA MAASKOFU WAHOFIA USALAMA WA KATIBA


SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kusaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), limesema kwamba kupitishwa kwa harakaharaka muswada huo inaweza kuipeleka nchi pabaya.

Pamoja na hayo, TEC imesema kitendo cha Serikali kukusanya maoni katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Visiwani Zanzibar peke yake, haitoshi kujenga hoja ya kusaini ama kupitisha muswada huo wa Katiba.



Mwandishi wa mtandao huu kutoka Jijini Mwanza, Sitta Tumma anaripoti kwamba; Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Jude Thaddaeus Ruwa'ichi aliyasema hayo jana usiku Jijini Mwanza, muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kilichoandikwa na John Kasembo, na kufanyika katika ukumbi wa Mwanza hoteli.Ruwa'ichi ambaye alihojiwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na suala zima la mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya hapa nchini, alisema, suala la kuundwa kwa Katiba mpya si hiari ya Rais wala kundi na tabaka fulani, bali ni la Watanzania wote.


Akizungumza kwa kutumia neno 'Mbindembinde', Rais huyo wa TEC ambaye pia ni Baba Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza alisema, Rais kabla hajasaini Muswada huo wa Katiba, Watanzania wengi walitaka Muswada huo usisainiwe, na kwamba Mkuu huyo wa nchi alipaswa kusikiliza mawazo ya wananchi wake, na si kuwahi kusaini na kuwa Sheria."Katiba ndiyo mhimili wa taifa lolote duniani.

Kabla ya Rais hajasaini muswada huu, ilitakiwa wananchi wote washirikishwe kutoa mawazo yao kwamba wanataka Katiba ya namna gani!.

"Suala la kuchukuwa maoni kwa mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar pekee, haitoshi kabisa. Na jambo hili la Katiba mpya likipelekwa mbindembinde linaweza kuipeleka nchi hii kubaya, hatutaki tufike huko", alisema Rais huyo wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Ruwa'ichi.



Hata hivyo, Ruwa'ichi ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika uzinduzi wa kitabu hicho cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kilichoandikwa na John Kasembo, alieleza kushangazwa na kitendo cha Bunge kupitisha harakaharaka muswada huo.Alihoji kwamba: "Hivi Bunge linashughulikia maslahi ya nani?.

Wabunge wamepewa dhamana na wananchi, hivyo ni lazima wawasikilize wanachotaka, halafu ndicho wakifanyie kazi, na si kuonekana kama ushabiki fulani.


Alipoulizwa kuhusu suala la udini linaloonekana kutumiwa na baadhi ya wanasiasa nchini, Rais huyo wa Baraza la Maaskofu, alikiri kuwepo kwa jinamizi hilo, na kusema ajenda ya udini kwa sasa imekuwa kama kichaka cha watu fulani kuficha maovu yao.



Alionya kwamba, iwapo Serikali itaruhusu mijadala ya udini kutawala nchini, basi taifa lipo hatarini kupoteza ustawi wake, kwani Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipiga vita ubaguzi wa kidini, na kamwe watu wasitumie mgongo wa dini kuficha madhambi yao.


Saturday, November 19, 2011

NDUGU MDAU KWA HABARI ZA PAPO KWA PAPO INGIA HAPA

MADIWANI SENGEREMA WAMTOA JASHO RC WA MWANZA

MADIWANI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wamekataa pendekezo la Mkuu wa mkoa huo, Evarist Welle Ndikilo, kuhusu watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo wanaotuhumiwa kwa ufisadi, kuchukuliwa hatua na Katibu Mkuu wa TAMISEMI, badala yake wanataka Baraza la madiwani ndilo liwashughulikie watendaji hao.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Mwanza, Sitta Tumma, anaripoti kwamba; hatua hiyo imejitokeza juzi wakati wa kikao maalumu kilichoitishwa dhidi ya madiwani wa CCM, kwa ajili ya kujadili mambo mbali mbali, kikao ambacho mgeni wake rasmi alikuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Ndikilo, ambaye alikwenda kutoa ufafanuzi wa barua yake ya kutaka watendaji hao wawajibishwe na Tamisemi, badala ya Baraza la madiwani.

Katika kikao hicho ambacho kinadaiwa kuhudhuriwa na madiwani wapatao 40 wa CCM, kisha kupewa posho ya kuanzia sh. 100,000 kila mjumbe, Mkuu huyo wa mkoa anasadikiwa kuwashawishi madiwani hao kuridhia ushauri wake huo, jambo ambalo lilipingwa vikali na idadi kubwa ya madiwani, wakitaka Baraza ndilo lenye mamlaka ya kuchukuwa hatua dhidi ya watendaji wabovu.

Mvutano huo umekuja kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayodaiwa kubainisha wazi upotevu wa mamilioni ya fedha, huku ripoti hiyo ikiwataja baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo ya Sengerema kuhusika na tuhuma hizo, na madiwani hao wana wasiwasi ofisi ya Katibu Mkuu wa TAMISEMI inaweza kuwalinda watendaji hao, na kushindwa kuwawajibisha.

Oktoba 25 mwaka huu, Baraza la madiwani la wilaya hiyo lililazimika kujigeuza kuwa kama kamati, kwa ajili ya kujadili ripoti hiyo na hatua za kuchukuliwa watendaji wote wanaohusishwa na ubadhilifu huo wa mali za umma, na kwamba baadaye kamati hiyo iliagiza kuitishwa kwa Baraza la madiwani ndani ya siku 21, ambayo imeishia Novemba 15 mwaka huu, bila Baraza kuitishwa.

Kufuatia hali hiyo tata, badala ya kuitishwa kwa Baraza hilo, inadaiwa uongozi uliwaita madiwani wote wa CCM kukutana Novemba 17 katika ukumbi wa ofisi za chama hicho mjini Sengerema, kwa lengo la kujadili na kuridhia ushauri wa Mkuu wa mkoa kwamba ofisi ya Katibu Mkuu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMI\SEMI), iachiwe kazi ya kuwawajibisha watendaji hao (majina tunayo).

Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kwamba, idadi kubwa ya madiwani ilikataa ushauri wa mkuu huyo wa mkoa, na kwamba kinachotakiwa ni Baraza la madiwani lenye mamlaka kisheria kuachiwa kazi hiyo, na si kutaka hoja hiyo kumezwa na mamlaka nyingine.

"Kikao kilikuwa moto kweli. Madiwani wengi wamekataa kabisa ushauriwa na mapendekezo ya RC Ndikilo. Wanataka Baraza la madiwani ndilo liachiwe mamlaka liliyonayo la kuwashughulikia watendaji waliotajwa na CAG kwa ufisadi.

"Diwani wa Kata ya Lugata, Adrian Tizeba alimhoji mkuu wa mkoa kapata wapi mamlaka ya kumeza madaraka ya Baraza la madiwani katika kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji hao?. Ushauri wa RC ulilenga kuchakachua utaratibu na kutaka kuwalinda hawa watu", kilisema chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina.

Licha ya mkuu wa mkoa kuwepo, kikao hicho kilihudhuriwa pia na mkuu wa wilaya ya Sengerema, Ellinas Palagyo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mathew Ndalahwa Lubongeja, mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Jaji Tasinga pamoja na viongozi wengine wa CCM ngazi ya wilaya.

Hata hivyo, chanzo cha habari kimeongeza kwamba, kuna kundi la baadhi ya madiwani wa CCM walikuwa wameandaliwa kwa ajili ya kupingana na kauli za wenzao wanaotaka watendaji hao washughulikiwe na Baraza la madiwani, wakihofia kwamba Baraza hilo litawafukuza kazi, tofauti na jinsi ambavyo lingeshughulikiwa na TAMISEMI.

Imeelezwa kwamba, ndani ya kikao hicho, RC Ndikilo alionekana kuchukizwa na ujumbe mfupi (SMS), alioupata ukidaiwa kuandikwa na mmoja wa madiwani wa wilaya hiyo, ukimtaja kwamba anataka kuwalinda mafisadi, na kwamba baada ya madiwani hao kuonekana kukataa hoja na ushauri wake huo, alilazimika kuaga na kuondoka kikaoni hapo kisha kurejea jijini Mwanza.

Hata hivyo, Ndikilo alipotafutwa na mtandao huu ili aweze kuzungumzia sakata hilo, hakuweza kupatikana mara moja.

Friday, November 4, 2011

MICHUANO YA KOMBE LA UHAI YAJA

Michuano ya kuwania Kombe la Uhai (Uhai Cup 2011) inayoshirikisha timu za pili (U20) za klabu zote 14 za Ligi Kuu ya Vodacom inatarajia kuanza Novemba 12 mwaka huu katika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boyz) itashiriki michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa ikiwa timu mwalikwa.

Bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba.

Mchezaji bora atapata sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu itapata sh. 300,000. Kila timu inayoshiriki itapatiwa sh. milioni moja kwa ajili ya maandalizi.

Mdhamini pia atagharamia nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi kwa timu ambazo zinatoka mikoani. Michuano hiyo itachezeshwa na waamuzi vijana kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Pia mradi wa Campaign Against Malaria nao utasaidia kwa kutoa jezi kwa timu zote zinazoshiriki michuano hiyo.

Kesho (Novemba 5 mwaka huu) saa 4 asubuhi kutakuwa na mkutano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu zenye timu shiriki na baadaye kufanyika upangaji ratiba.

STARS KUTEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambayo hivi sasa iko kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Chad, kesho (Novemba 5 mwaka huu) saa 5 asubuhi itatembelea Makumbusho ya Taifa.
Ziara yao ni ya kawaida, lakini pia kutakuwa na onyesho la Historia ya Soka Tanzania.

Wachezaji ambao tayari wapo kambini hoteli ya New Africa ni Juma Kaseja, Godfrey Taita, Shabani Nditi, Hussein Javu, Juma Jabu, Ramadhan Chombo, Shomari Kapombe, Nurdin Bakari, Nadir Haroub, Juma Nyoso, Erasto Nyoni, Mrisho Ngasa, Mwadini Ally na Aggrey Morris.

Idrisa Rajab wa Sofapaka ya Kenya tayari naye yuko kambini wakati wachezaji wengine kutoka nje wanatarajia kuwasili leo usiku. Wachezaji wa mwisho kutoka nje tunawatarajia kesho.

MORO UTD, SIMBA ZAINGIZA MIL 5.7
Mechi namba 86 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Moro United na Simba iliyochezwa Novemba 2 mwaka huu Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 5,764,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 1,688 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 10,000 kwa VIP na sh. 3,000 kwa majukwaa mengine. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni asilimia 18 iliyolipwa ni sh. 879,254.

Gharama za awali kabla ya mchezo; kila klabu ilipata sh. 118,160 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 101,280 kutoka mfuko wa jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi.

Nauli ya ndani kwa waamuzi, kamishna na mtathimini wa waamuzi ni sh. 90,000. Posho ya kujikimu kwa kamishna ni sh. 40,000. Gharama ya tiketi ni sh. 1,230,000 wakati usafi na ulinzi ni sh. 500,000.

Baada ya gharama hizo za awali kila klabu ilipata sh. 907,424, gharama za mchezo sh. 302,475, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 151,237), Uwanja sh. 302,475, DRFA (sh. 120,990) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 30,247).

Powered by Sorecson : Creation de site internet

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Wednesday, November 2, 2011

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA WAKURUGENZI WA TPDC NA TIC

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta nchini (TPDC), Yona Killagane, wakati walipokutana kwa mazungumzo Ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam leo Kushoto ni Mkurugenzi Masoko na Uwekezaji wa Shirika hilo, Dismas Fuko
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Ujumbe wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakati walipofika ofisini kwake jijini Ikulu Dar es Salaam leo Picha na muhidin Sufiani-OMR